Makala

Msimu wa ligi kuu za soka Ulaya watarajiwa kusisimua biashara nchini

August 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

HUKU Ligi kuu za kandanda hasa Ulaya zikitarajiwa kuanza rasmi msimu mpya wiki chache zijazo, wawekezaji katika sekta za burudani wameelezea matumaini yao kuwa watapata faida ikizingatiwa wateja ambao ni mashabiki wanatarajiwa kufurika.

Kuna baadhi ya wamiliki biashara hizo ambao wamezindua hoteli na pia baa wakilenga biashara ya ligi hizi na ambazo zile hufuatwa sana hapa nchini ni pamoja na ile ya Uingereza (EPL) ile ya Uhispania (Laliga) na ile ya Ujerumani (Bundesliga).

Hali ni kali kibiashara kiasi kwamba, hata wauzao miraa na muguka kando na kuuza maji, njugu, peremende na kadhalika, wengine walio na wateja wa ‘nguvu’ wamepachika runinga katika majumba yao ya kibiashara wakisubiri mavuno ya msimu wa soka.

Wengi wanafurahia hali kwamba mwaka huu ulikuwa mzuri kwa kuwa wengi hawajamaliza kuhesabu faida za kupeperusha michuano ya Afcon 2019 na sasa ‘msimu halisi’ wa soka unaingia Agosti hii na kuendelea hadi Mei 2020.

Kuna wale ambao wako na upana wa kimawazo kuhusu kabumbu na utawapata wakifuatilia ligi kama za Uturuki, Iraq na labda Bosnia Herzegovina huku wengine wakijua hata mtingaji mabao bora zaidi katika ligi za Israel, Urusi na hata Montenegro.

Lakini hayo yote yakiwa ni tisa, la kumi ni kwamba, kuna wale wanaomiliki biashara na majumba ya kamari na ubashiri wa matokeo ya mechi ambao huu ni wakati ambapo wako mbioni kuimarisha mitambo yao ya Intaneti bila malipo kwa wateja wao (WiFi) na pia mitambo ya kunasa mawimbi ya kupeperusha ligi kuu hizo.

Kwa utani, mmiliki wa jumba la video Murang’a Bw Joseph Kibe anasema kuwa Wakenya wangepanga maandamano hapa nchini ya kudai haki yao ya kutazama EPL na wapanga ratiba wa ligi hiyo washinikizwe iwe kuwa kila timu kubwa itachuana na nyingine mara tatu kwa siku ili faida kwa ‘wawekezaji’ zibakie imara na hela ambazo husemwa kuwa ni sabuni ya roho, nyoyo za wengi zing’are hapa nchini.

“Nitajiunga na maandamano hayo. Punda wa Kenya hawezi akachoka kwa kutazama mechi hata 20 kwa siku; hasa wakati Arsenal, Manchester United, Chelsea, Liverpool, Real Madrid, na Barcelona zikicheza. Hata zicheze mara 50 kwa siku ndiyo itakuwa raha kwetu,” anasema.

Walioelezea mtandao wa Taifa Leo kuhusu mavuno kibaba ambayo hutwaliwa katika msimu wa soka duniani ni pamoja na wahudumu wa baa, mikahawa na majumba ya video, huku wahudumu wa baa pia wakionekana kusisimka.

Wauzaji televisheni na vijisanduku vya kunasa miale ya upeperushaji katika mfumo wa dijitali – vizimbuzi – hawajaachwa nyuma, wakielezea kuwa “biashara zetu zimepata pumzi ya uhai ndani ya ligi hizi zenye ufuasi nchini.”

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Marabou Lounges Bw Bob Kinyua (pichani), ligi hizi ziko na uwezo wa kuzolea mwekezaji mpya takriban Sh3 milioni kama faida pekee katika kipindi hicho cha mwaka mmoja wa uhai wa msimu mmoja.

“Wateja hufurika katika biashara zilizo na televisheni zinazopeperusha michuano ya EPL na walevi huwa na uteja wa hali ya juu, wenzao wa kunywa vileo visivyolewesha wakifuata na ikitokea mtu anahisi njaa akiwa ndani ya biashara hizo, huwa anaagiza chakula,” anasema Kinyua.

Anasema kuwa kuna mipira mikubwa ambayo huwa na uvutio wa ajabu na ambayo “utakosa kupeperusha ukiwa labda huna umakinifu wa kibiashara.”

“Kama hapa kwangu, nimeweka televisheni nane kwa kila biashara na huwa naweka mechi zote zinazojumuisha timu kubwa ili wateja wajigawe kulingana na ushabiki wao. Mimi langu ni kuwa mshirikishi wa mashabiki kutosheka na kutulia na huku wahudumu wangu wakiwa mbioni kuuza vileo na chakula,” anasema.

“Utapata kuwa katika siku za kawaida baa ya wastani huhitaji wahudumu kama wanne hadi sita. Lakini katika harakati za kuhakikisha unavutia wateja na kuwadumisha katika msimu wa soka, ni lazima uongeze wengine wa ziada wa kuhakikisha wateja hawakosi kuhudumiwa kwa wepesi, na pia hawatoroki na bili zao,” anasema.

Anasema kuwa biashara ya mauzo katika mikahawa yake na baa huongeza faida kwa asilimia 52 katika msimu wa soka.

Bw Kibe naye hajaweka baa au mkahawa bali amejenga jumba kubwa la video katika Mji wa Maragua ulioko Kaunti ya Murang’a anasema kuwa “ligi hiyo ikienda likizo kungojea msimu mwingine, biashara yangu huporomoka kiutenda kazi kwa asilimia 70.

“Ninabaki tu nikionyesha mikanda ya video ya kivita, mapenzi, upelelezi na habari. Kwa kawaida biashara ya aina hiyo hunasa tu wasiokuwa na pa kwenda mtaani. Lakini msimu mpya wa soka ukiingia, hata mimi hujipata nimeingiwa na joto la pato,” anasema.

Anasema kuwa ada zake huwa ni Sh20 kwa mipira midogo kwa maana ya mechi za kiwango cha chini huku timu kubwa inapojitosa uwanjani, ada hiyo hupanda hadi Sh50.

“Katika ukadiriaji wa ada, mimi hujua kuwa ikiwa mteja wangu alienda kutazama mchuano katika baa, angejipata anatumia Sh200 na zaidi, kwa mkahawa atumie kiwango cha chini cha Sh100. Mimi huwanasa kwa kuwapa afueni kuwa, hawahitajiki kujinunulia kitu ndani ya jumba langu. Akilipa tu ada ya kiingilio, atulie mpaka mpira uishe,” anasema.