Rais Kenyatta awataka viongozi kuiga mfano wa Laboso
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa kisiasa kuiga mfano wa marehemu Gavana wa Bomet Joyce Laboso ambaye alimtaja kama kiongozi mtumishi.
Rais amesema Jumamosi kwamba marehemu Laboso alitumikia familia yake, wapigakura wake na Wakenya kwa roho ya kujitolea na akafanikiwa kwa njia ambayo ilionekana na Wakenya wote.
“Alikuwa mkarimu na aliyejitolea kuwasaidia watu wa Sotik, Bomet na Wakenya kwa ujumla. Hakuwa mtu mwenye majivuno bali mnyenyekevu na ndiyo maana alipendwa na watu wote. Alitangamana na watu wote kwa furaha. Nyote hapa mwafaa kuiga mfano wa kiongozi huyu tunayempumzisha leo (Jumamosi),” amesema Rais Kenyatta
Katika maisha yake ya kisiasa, marehemu Laboso, Rais Kenyatta akasema, alihudumu kama Mbunge wa Sotik kwa mihula miwili, Naibu Spika na Gavana wa Bomet.
Rais amesema hayo wakati wa ibada kabla ya kumzika Laboso nyumbani kwake katika eneo la Fort Tenan, Koru, Kaunti ya Kisumu.
“Marehemu Laboso ni kiongozi ambaye hakuonyesha uchu wa kutumia vibaya afisi yake kwa kujilimbikizia mali bali mtumishi wa wananchi aliyefanya hivyo kwa uadilifu,” kiongozi wa nchi amesisitiza.
Abonyo asifiwa
Kiongozi wa taifa amemiminia sifa mumewe marehemu Laboso, Dkt Edwin Abonyo, kwa kuunda familia yenye mshikamano licha ya wawili hao kutoka jamii mbili zenye mila, tamaduni na imani tofauti.
“Nakupongeza Dkt Abonyo kwa kupuuzilia mbali baadhi ya mila na tamaduni zilizopitwa na wakati na kujenga familia thabiti na ya kupigiwa mfano,” akasema Rais Kenyatta.
Ibada hiyo imefanyika katika Shule ya Upili ya Kandege na kuhudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, waliokuwa makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi miongoni mwa viongozi wengine kutoka pembe zote nchini.