Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nahisi uchungu kila nikikojoa

August 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DKT FLO

Hujambo,

Kwa juma moja sasa napata uchungu mwingi kila nikikojoa. Jana, niligundua matone ya damu kwenye mkojo pia. Haya yote yalianza baada ya kushiriki ngono na msichana fulani bila kinga katika sherehe fulani. Je, huenda yeye ndiye amenisababishia haya? Nifanyeje? Naona aibu ya kwenda hospitalini.

SK

Mpendwa SK,

Kuna uwezekano mkubwa kwamba ulipata maambukizi baada ya kushiriki ngono.

Maambukizi ya mfumo wa njia ya kupitisha mkojo yaweza kusababisha uchungu unapokojoa na maumivu ya tumbo.

Unahitaji uchunguzi utakaofanyiwa kwenye mkojo ili kutambua kiwango cha maambukizi, na wakati mwingine huenda ukajua sababu kamili ya maambukizi hayo.

Tiba yaweza kuwa kupitia sindano au kumeza tembe.

Aidha, kunywa maji mengi kwa sababu unapokojoa mara nyingi kwa siku, bakteria inayosababisha maambukizi haya pia inasafishwa.

Ni muhimu vilevile kwa yeyote ambaye umeshiriki naye ngono bila kinga hivi karibuni kupata matibabu ili kuzuia maambukizi mapya.

Katika siku zijazo, kumbuka kutumia kinga kwa sababu maambukizi ya kila mara yanaweza kusababisha matatizo mabaya kama vile mrija wa mkojo kuwa mwembamba kwa sababu ya mkusanyiko wa makovu (urethral stricture) ambapo itakuwa vigumu kupitisha mkojo.

******

Mpendwa Daktari,

Naitwa Juma. Mwaka huu nimepata tiba mara mbili dhidi ya amoeba. Kwa kawaida mimi hutumia dawa zote kuambatana na ushauri wa daktari. Yaweza kuwa nilipewa dawa mbaya au amoeba haitokomei kabisa baada ya kutibiwa?

Juma

Mpendwa Juma,

Amoebiasis ni maambukizi yanayosababishwa na kimelea kinaachoitwa Entamoeba histolytica.

Kimelea hiki kwa kawaida hufikia tumbo au matumbo kupitia chakula au maji ya kunywa yaliyo na maambukizi.

Ikiwa viwango vya vimelea ni vingi sana mwilini, matokeo yatakuwa kuendesha, kutapika, maumivu ya tumbo na wakati mwingine damu kwenye kinyesi. Mara nyingi hutibiwa kwa urahisi kwa kutumia dawa zinazotumiwa kwa wiki moja.

Dawa hizi zinapaswa kuanza kutumiwa baada ya uchunguzi kufanyiwa kwenye kinyesi kuangalia ikiwa kina kimelea hicho.

Inawezekana kupata maambukizi mengine hata baada ya kutibiwa endapo utakula chakula au kunywa maji yenye maambukizi. Ili kuzuia, hakikisha unanawa mikono kila mara, unakula chakula kilichopikwa vyema na kusafisha vyema chakula chochote kinacholiwa kikiwa kibichi kama vile matunda na mboga.

******

Uso wangu haunifurahishi kwa sababu umetawaliwa na chunusi ambazo nimegundua kwamba huja na kwenda. Sasa nimekuwa nikijikuna kwa matumaini kwamba zitatokomea. Je, kuna mbinu asili ambazo naweza kutumia kukabiliana na chunusi, vilevile madoa meusi?

Almasy

Mpendwa Almasy,

Chunusi hujitokeza kila mara hasa usoni na ambazo huishia kuwa madoa.

Hali hii hutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya kiwango cha homoni, maambukizi na kiwango cha mafuta halisi yanayozalishwa na ngozi (sebum).

Kuna uwezekano wa baadhi ya watu kukumbwa na chunusi zaidi ya wengine, na kwa baadhi ya watu, hali hii huwakumba msimu fulani kama vile wakiwa katika umri wa kubalehe, wakati wa ujauzito, na nyakati mbalimbali za mwezi, hasa wakiwa na mfadhaiko.

Tatizo kuu linalotokana na chunusi ni madoa meusi. Nawa uso mara mbili kwa siku; asubuhi na usiku kabla ya kwenda kulala. Tumia sabuni na taulo nyepesi.

Usisugue uso wako unaponawa kwa sababu tayari ngozi katika sehemu hii ni nyepesi. Kunywa maji mengi, matunda na mboga, vile vile ufanye mazoezi.

Usiwe na mazoea ya kufinya chunusi kwani hii husababisha madoa meusi.

Aidha, ni jambo la busara kutafuta ushauri kutoka kwa daktari wa ngozi ambaye atakushauri kuhusu dawa za kutumia ili kudhibiti hali hii. Kwa watu wengi, huchukua muda kabla ya kupata dawa inayofaa, kwa hivyo kuwa na subira.