• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Kulala taa zikiwaka hatari kwa uzani wa wanawake

MAZINGIRA NA SAYANSI: Kulala taa zikiwaka hatari kwa uzani wa wanawake

Na LEONARD ONYANGO

UNENE kupindukia ni shida ambayo imekumba idadi kubwa ya wanawake humu nchini. Wengi wao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kwa lengo la kutatua tatizo hilo.

Utafiti uliofanywa na Stepwise kuhusu Magonjwa Yasiyoambukizwa (DCD) unaonyesha kuwa, asilimia 27 ya watu nchini Kenya ni wanene au wanene kupindukia.

Utafiti huo unaonyesha wanawake wanene kupindukia ni asilimia 38 ikilinganishwa na asilimia 17 ya wanaume.

Nao utafiti uliofanywa na Chuo cha Göttingen cha Ujerumani kwa ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya Kutafiti Vyakula (IFPRI), ulibaini kwamba ongezeko la watu wanene kupindukia nchini Kenya linasababishwa na kuwepo kwa vyakula vingi vinavyouzwa katika maduka makuu.

Asilimia 47.1 ya wanawake katika maeneo ya Kati na Nairobi ni wanono kupindukia, kulingana na utafiti huo.

Kati ya asilimia 30 na 40 ya wanawake kutoka kanda za Pwani, Mashariki na Nyanza ni wanene kupita kiasi. Wanawake kutoka maeneo ya Bonde la Ufa, Magharibi na Kaskazini Mashariki wana uzani wa kadri.

Wanawake wanene zaidi ni wale wako kati ya umri wa miaka 40 na 49 wakifuatiwa na wenzao wa umri wa miaka 30 na 39.

Asilimia 12 ya wasichana wa kati ya umri wa miaka 15 na 19 pia ni wanene kupindukia nchini Kenya.

Unene kupindukia husababisha maradhi ya kansa, moyo na hata kuathiri uzazi wanapokuwa wajawazito.

Wataalamu wa afya wanahimiza watu kula lishe bora na mazoezi kama njia mojawapo ya kupunguza uzito au unene.

Uhusiano baina ya unene na mwangaza

Utafiti uliochapishwa katika jarida la Chama cha Wataalamu wa Matibabu nchini Amerika, JAMA Internal Medicine Journal, unaonyesha kwamba kuacha stima zikiwa zimewaka unapolala usiku kunaweza kusababisha unene kupindukia.

Kulingana na wanasayansi waliofanya utafiti huo, kulala bila kuzima televisheni au taa za umeme kunatosha kufanya wanawake kuwa wanene kupindukia.

Huo ndio utafiti wa kwanza kuelezea uhusiano uliopo baina ya unene na mwangaza wa umeme.

Wanasayansi hao walihusisha jumla ya wanawake 43,722 katika utafiti huo.

Wanawake hao wa kati ya umri wa miaka 35 na 74 hawakuwa wajawazito. Wote hawakuwa na historia ya maradhi ya kansa au moyo wakati wa kufanyika kwa utafiti huo.

Waliulizwa ikiwa walilala huku taa zikiwaka au walizima. Kadhalika, waliulizwa ikiwa wanapolala usiku huwa wanazima televisheni au wanaiacha imewaka.

Kwa kutumia taarifa hizo, wanasayansi waliweza kutathmini uhusiano uliopo baina ya mwangaza usio wa asili (umeme) na ongezeko la uzani.

Matokeo yalitofautiana kulingana na wingi wa mwangaza ndani ya chumba.

Kwa mfano wanawake waliolala na kuacha koroboi au mshumaa ukiwaka, hawakuongeza uzito.

Wanawake waliolala usiku bila kuzima televisheni waliongeza uzani kwa kilogramu tano.

Waliolala lakini mwangaza unamlika vyumba vyao kupitia dirishani kutoka nje pia waliongeza uzani kwa kiasi kidogo.

Wanasayansi hao walisema kuwa matokeo kuhusu uzani yalikuwa sawa bila kujali umri, rangi, aina ya chakula walichokula, ikiwa wanafanya mazoezi au la, kuwa na watoto nyumbani au la.

Chandra Jackson, mmoja wa watafiti hao kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Sayansi ya Afya na Mazingira, Amerika (NIEHS) alisema kuwa wanawake wanaoishi mijini ambapo kuna umeme ndio wameathiriwa zaidi.

Tafiti zilizowahi kufanywa hapo awali zilisema kuwa mwangaza usio wa kiasili kama vile umeme au taa za mitaani huzuia ubongo kutoa homoni zinazojulikana kama ‘melatonin’ zinazoleta usingizi haswa usiku.

Homoni hizo ndizo husababisha watu kulala na kuamka wakati ufaao.

Upungufu wa homoni hizo huathiri ubora wa usingizi na kukosesha mwili fursa ya kurekebisha sukari mwilini hivyo kumfanya mwathiriwa kunenepa.

“Mwili wa binadamu unapendelea mazingira yaliyo na mwangaza wa asili wa jua wakati wa mchana na giza usiku. Hivyo, kuwepo kwa mwangaza usio wa asili usiku kunaathiri homoni za usingizi katika ubongo na kusababisha mwathiriwa kuwa mnene kupita kiasi,” akasema Jackson.

Mtafiti Mkuu Young-Moon Park alisema utafiti huo unatoa changamoto kwa wanawake kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanaepuka kuwa wanene.

“Ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta kupita kiasi na kutofanya mazoezi vimetajwa kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya unene kupindukia. Lakini utafiti huu umetoa sababu nyingine na kuna haja ya kuepuka kulala usiku taa zikiwaka. Watu wanafaa kulala gizani bila kuwepo kwa mwangaza,” akasema.

Unapolala gizani, ubongo hutoa homoni za kutosha ambazo husaidia mwili kurekebisha kiwango cha sukari mwilini usiku.

Homoni hizo pia hurekebisha mafuta mwilini na kuongeza nguvu kinga za mwili ambazo hukabiliana na maradhi kama vile kansa na shinikizo la damu.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nahisi uchungu kila nikikojoa

Baadhi ya vijana wa Angaza Youth wazuru Ufaransa kupitia...

adminleo