GUMZO LA SPOTI: Liverpool yapata kizibo cha Mignolet
Na MASHIRIKA
MARSEYSIDE, UINGEREZA
LIVERPOOL wanatarajiwa kumsajili kipa Adrian San Miguel wa West Ham United ili kuchukua nafasi ya Simon Mignolet ambaye ameyoyomea Ubelgiji kuvalia jezi za kikosi cha Club Bruges kilichomshawishi kwa Sh830 milioni.
Adrian, 32, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na West Ham almaarufu ‘The Hammers’ kutamatika mwishoni mwa msimu jana. Katika kipindi cha miaka sita ambapo amewadakia West Ham, Adrian amewajibishwa mara 150 tangu asajiliwe kutoka Real Betis mnamo 2013.
Kipa huyu mzawa wa Uhispania anatarajiwa kuwa msaidizi rasmi wa Alisson Becker ambaye aliweka rekodi ya kuwa mlinda-lango ghali zaidi duniani tangu akamilishe uhamisho wake kutoka AS Roma kwa kima cha Sh8.4 bilioni mnamo 2017.
Ujio wa Adrian utamfanya kuwa kipa wan ne wa Liverpool ambao tayari wanajivunia huduma za chipukizi Sepp van den Berg na Harvey Elliott kambini mwao hadi kufikia sasa.
Kwingineko, Barcelona wamekamilisha mchakato wa kumsajili beki Junior Firpo kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Real Betis. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 22 alirasimisha uhamisho wake kwa kima cha Sh3.6 bilioni.
Chipukizi
Firpo aliwajibishwa na Betis katika jumla ya michuano 29 msimu jana na pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Uhispania cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 ambacho kilitawazwa mabingwa wa Euro mnamo Juni 2019.
Zaidi ya Firpo, Barcelona wanajivunia pia kuwasajili wachezaji Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid, Frenkie de Jong kutoka Ajax Amsterdam, kipa Neto kutoka Valencia na beki Emerson kutoka Atletico-MG.
Wiki jana, Barcelona waliagana na fowadi wao chipukizi Malcom aliyeyoyomea Urusi kuvalia jezi za Zenit St Petersburg kwa kima cha Sh4.8 bilioni. Kutua kwa Malcom nchini Urusi kuliwaweka Everton ambao pia walikuwa wakimvizia katika ulazima wa kumsajili chipukizi wa Juventus na Italia, Moise Kean kwa mkataba wa miaka mitano. Kean alifunga mabao manane kutokana na mechi 21 alizochezea Juventus msimu jana.