KILIMO: Ukuzaji wa vitunguu saumu
Na SAMMY WAWERU
KWA mwaka Kenya huagiza karibu asilimia 80 ya vitunguu saumu kutoka China.
Hili hasa linatokana na upungufu wa zao hili nchini, ikizingatiwa kuwa ni wakulima wachache mno wanaovikuza.
Hii ina maana kuwa, ni zao linaloadimika katika masoko.
Eneo la Kiawara, katika barabara kuu ya Nyeri-Nyahururu, ndilo linafahamika nchini katika uzalishaji wa vitunguu saumu.
Mahitaji ya vitunguu hivi yanatokana na faida zake kiafya. Kulingana na wataalamu wa masuala ya afya, vimesheheni Vitamini kama vile; Vitamini C na Vitamin B6.
“Vitamini ni kinga bora dhidi ya magonjwa ibuka. Tunahimiza watu kula vyakula vilivyosheheni madini haya,” anasema mtaalamu Juliet Mwanga.
Mdau huyu pia anasema vitunguu hivi ni kiini kizuri cha Potassium, Calcium na Phosphorous.
Pia, vina madini ya Copper na Manganese.
Mbali na manufaa yake kisiha, vitunguu saumu vina tija tele kimapato kwa wanaovikuza.
Bw Timothy Mburu amekuwa akivipanda eneo la Naromoru, Kieni, Kaunti ya Nyeri, kwa karibu miaka minne mfululizo na ana kila sababu ya kutabasamu kwa ajili ya hatua ambazo vimempigisha kimaendeleo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwanazaraa huyu ni kwamba alianza kama utafiti, kwani kuna dhana kuwa eneo la Mlima Kenya halina udongo wala hali bora ya anga kuvizalisha.
Kwenye mahojiano na Bw Mburu katika shamba lake kijiji cha Gitinga, alisema mwaka 2015 alinunua kilo moja ya mbegu za vitunguu saumu akazipanda eneo lenye ukubwa wa mita 5 kwa 5, mraba. Aidha, aliuziwa kwa Sh500.
“Miezi minne baadaye, nilivuna kilo 40. Lengo hasa lilikuwa kutafiti iwapo Mlima Kenya inaweza kuzalisha vitunguu saumu, na nilibaini ina uwezo,” akaambia Taifa Leo.
Alisema utafiti pia ni kielelezo kuwa Kenya ina udongo na hali bora ya anga kuzikuza kwa wingi.
Mburu hakuuza mazao aliyopata, na anasema aliyarejesha, kama mbegu, kwenye thumni (1/8) ekari mnamo 2016.
Ni shughuli za kilimo anazofanya kufikia sasa.
Wataalamu wa kilimo wanasema vitunguu saumu vinastawi maeneo yaliyo kati ya mita 500-2000 juu ya ufuo wa bahari (altitude).
Aidha, udongo unapaswa kuwa wenye rutuba na usiotuamisha maji.
Asidi ya udongo, pH, inapaswa kuwa kati ya 4.5-8.3 ingawa hata 6.5 hadi 6.7 pia inafanikisha kilimo chake. Vinanawiri katika katika maeneo yenye kiwango cha joto, nyuzi 24-30 za sentigredi.
Kulingana na Bw Mburu, kinachofanya wakulima kushindwa kuzalisha vitunguu hivi ni ukosefu wa maarifa ya namna ya kuvipanda. Anasema hufeli kuanzia aina ya mbegu zifaazo kupanda.
Anaeleza kwamba vitunguu saumu huchukua muda wa miezi mitatu kuwa tayari kwa mavuno, baada ya upanzi, na ili kupata mbegu bora, mkulima anapaswa kuvipa mwezi mmoja zaidi kuvivuna.
“Wakati huo vitakuwa vimekomaa,” anadokeza Mburu.
Anafafanua kuwa vinapovunwa miezi mitatu baada ya upanzi, huwa vingali na kwamba mbegu za aina hiyo si bora katika upanzi.
Hata hivyo, changamoto hii inasemekana kusababishwa na wazalishaji wa mbegu.
“Itaangaziwa wanaozalisha mbegu wakiitikia kuzipa muda zikomae ili wakulima wapate zile bora kuendeleza kilimo chake,” anasema Bw Meshack Wachira, mtaalamu kutoka Novixa International Ltd.
Emmah Wanjiru, kutoka kampuni ya kilimo ya H.M Clause, anasema kinafelisha wakulima wengi ni kuwepo kwa pembejeo; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, duni na bandia.
“Kuna pembejeo nyingi sana duni sokoni, zingine zikiwa bandia. Ni jukumu la mkulima kuzinunua katika maduka ya kilimo yaliyoidhinishwa na taasisi husika,” anahimiza Wanjiru.
Kando na mbegu za saumu kuwa zimekomaa, zinapaswa kuwa salama dhidi ya changamoto kama wadudu na magonjwa.
Bw Wachira pia anashauri wakulima kununua mbegu kwa kampuni zilizoidhinishwa pamoja na wakulima waliobobea. Mbegu zake ni vitunguu vilivyoachwa kukomaa shambani. Mburu anasema kilo moja inagharimu kati ya Sh450 hadi Sh500.
Mkulima huyu kwa sasa anavipanda kwenye nusu ekari. Mbali navyo, hukuza viazimbatata, kabichi na maharagwe asili. Ana bwawa, ambalo limemuzesha kukumbatia mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kwa mifereji.
Mbegu za vitunguu saumu, vipande vidogo vilivyodondolewa kutoka kwa vilivyokomaa, hazikuzwi kwenye kitalu ili kupata miche. “Vitunguu saumu vinahitaji umakinifu wa hali ya juu, havitaki usumbufu wowote, hivyo basi mbegu zake hupandwa moja kwa moja,” asema Bw Mburu.
Anaeleza kwamba shamba linapolimwa, huandaliwa vipande maalum maarufu kama ‘beds’. Ni vipande ambavyo udongo umeinuliwa na kufanywa uwe mwororo. Anasema kimoja kinapaswa kuwa na kimo cha mita 1 kwa 1, mraba.
Mkulima huyu wa aina yake huandaa mitaro yenye urefu wa inchi 6 kuenda chini, na kupanda mbegu za vitunguu saumu mita nne kutoka moja hadi nyingine. Mbolea huitia baada ya palizi ya kwanza, wiki mbili baada ya upanzi.
Mburu hufanya kilimo chake kwa kutumia mboleahai, aina ya mboji-kinyesi cha mifugo na kuku, kilichochanganywa na majani na matawi, kisha kikapewa muda kuiva.
Anasema vitunguu hivi vinahitaji mbolea kwa wingi ili viweze kuunda sambamba. Pia, vinahitaji kutiwa mbolea ya kisasa yenye madini ya Potassium na Calcium. Mboleahai imesheheni Nitrojini, madini muhimu zaidi kwa mimea.
Changamoto zinazofika vitunguu hivi ni ugonjwa wa early na late blight, pamoja na ukungu. Wadudu ni vithiripi, mkilima akihimizwa kufuata maelekezo ya mtaalamu au wataalamu kukabili changamoto hizo.
Mbali na kuwa mkulima tajika, Mburu pia ni mtaalamu wa masuala ya zaraa na anasema nusu ekari iliyotunzwa vyema ina uwezo kuzalisha tani nne.