Makala

KINA CHA FIKIRA: Umilisi wa Kiswahili u katika kuyamudu mambo ya msingi

August 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

HATUNA budi kurudi kwa mambo ya msingi.

Mambo ya msingi yakitupita hata tujaribu vipi kujishaua hatuwezi kuwa weledi wa lugha.

Kwa kweli tatizo kubwa linalokumba matumizi ya lugha ya Kiswahili ni kupuuzwa kwa mambo ya msingi.

Na msingi wa uthabiti halisi wa umilisi wa Kiswahili hautegemei mizinga na makombora na majabali na mabuldoza.

Watu wanajitaabisha bure kutafuta ujuzi usio na tija wa maneno makubwa makubwa.

Wanashindwa kabisa na mambo ya msingi, mambo yanayotakiwa na kila mtumizi wa lugha.

Mnamo Jumapili bibi mmoja kaniuliza, Je, Kiswahili ni kigumu? Mimi nilimwambia hakuna lugha ngumu wala rahisi; hutegemea utashi wa mtu. Nilimuuliza iwapo Kisomali au Kirusi ni rahisi au kigumu akashindwa cha kusema.

Ingawa nilimpa jawabu la kifalsafa, kwa kweli, jawabu lenye kubabaisha, sikuacha kuwazia kwa nini ananiuliza hivyo, mtu aliyewahi kupitia katika mfumo wa elimu ambamo Kiswahili ni somo la lazima kwa zaidi ya miaka 14.

Naam, aliniuliza hivyo kwa nini? Kwa sababu watu tuliopewa jukumu la kumfundisha Kiswahili tulipanda akilini mwake kasumba ya makombora, mizinga, mabuldoza na majabali.

Ukitaka kujua kwamba mambo ya msingi tuliyapuuza kabisa kwa nini si aghalabu watu kutumia viambishi awali mwafaka katika maneno ya msingi kabisa.

Mathalani, unaweza kudhani yule bibi aliniuliza swali je, Kiswahili ni kigumu kwa Kiswahili safi. Wapi ng’o! Aliniuliza ni *Kiswahili ngumu? Kadondosha kiambishi cha awali ‘ki-’ ambacho ndicho kitakiwacho kukamilisha sarufi hapa.

Badala ya kufundishwa mambo ya msingi kabisa kuhusu matumizi ya kiambishi awali ‘ki-’ pahali kinapopaswa kuwa na kutokuwa, bibi huyu labda alibebeshwa mzigo mzito wa kukariri vikembe vya farasi, nyani, nyoka, vyura na vya treni au simu tamba.

Yamkini kakoseshwa mambo madogo ya msingi yanayofanya lugha iwe lugha na ivutie isemwapo.

Kutosisitiza mambo ya msingi ndiko sababu ya watu kusema mambo ya ajabu kama vile *“madada, mababa, mamama, mbaba, mmama, mndugu, mdada, mkaka.”

Kuna haja gani kubaini laptop inaitwaje kwa Kiswahili iwapo wezi tunawaita ‘waezi’? Kuna haja gani kujua website inaitwaje kwa Kiswahili iwapo hatuwezi kubainisha tofauti kati ya pilipili mboga (ambayo si kali ambayo wengine huiita pilipili hoho) na pipili hoho (ambayo ndiyo hasa iliyo kali sana)?

Kuna haja gani kuzijua istilahi za isimu kama foni, fonimu, alofoni, na sajili, ilhali hutuna habari iwapo ni kosa kusema *miezi mbili au *miaka nne?

Hilo ndilo janga tulilo nalo la kuwalazimishia vitu vya vyuoni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuwabebesha mzigo wasiopaswa kuubeba.

Ukiwasikia baada ya miaka 14 ya ufundishwaji wa Kiswahili, unahisi kipindi chote hicho kilikuwa kama kifungo kirefu cha jela. Hisia za wanafunzi ni kwamba kufundishwa Kiswahili ni kama kufungwa jela na kuongezwa viboko na kazi ngumu. Wakigeukia Sheng wamo kusaka uhuru.