• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Lionesses kuwaangusha miamba kwenye raga Afrika Kusini

Lionesses kuwaangusha miamba kwenye raga Afrika Kusini

Na MWANDISHI WETU

KOCHA Felix Oloo atapania kuwategemea pakubwa wanaraga Sheila Chajira, Vivian Akumu na Naomi Amuguni ili kuweka hai matumaini ya timu ya taifa ya Lionesses katika raga ya wachezaja 15 kila upande nchini Afrika Kusini.

Kikosi hicho kiliondoka nchini wikendi jana kuelekea Afrika Kusini kwa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2021. Michuano hiyo ya mchujo itaandaliwa kati ya Agosti 9-17 katika uwanja wa Bosman, Johannesburg.

Kenya wamepangwa kupepetana na wenyeji Afrika Kusini, Uganda na Madagascar katika jitihada za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini New Zealand.

Chajira anarejea katika kikosi cha Lionesses kwa mara ya kwanza tangu Aprili alipopata jeraha la kifundo cha mguu wakati wa michuano Hong Kong 7s iliyoshuhudia Kenya ikizimwa na Brazil kwenye nusu-fainali.

Ukubwa wa tajriba ya Chajira katika majukwaa ya raga ya raga ya kimataifa ni miongoni mwa mambo yanayomwaminisha zaidi Oloo kuwa kikosi chake kitatia fora.

Katika sehemu ya maandalizi yao ya kivumbi cha kufuzu kwa Kombe la Dunia, Lionesses walishiriki fainali za Elgon Cup mwaka 2019 na kuibuka washindi kwa kuzoa jumla ya alama 77-18 dhidi ya Uganda mwishoni mwa mechi mbili za mchujo mbele ya mashabiki wao wa nyumbani na ugenini.

Kufungua kampeni

Lionesses watafungua kampeni zao dhidi ya Madagascar mnamo Agosti 9 kisha kuchuana na Uganda Lady Cranes kwa mara ya tatu mwaka huu mnamo Agosti 13.

Watafunga mechi zao dhidi ya Afrika Kusini mnamo Agosti 17. Mshindi wa kivumbi hicho atajikatia tiketi ya Kombe la Dunia moja kwa moja huku nambari mbili akilazimika kushiriki mchujo mwingine dhidi ya mojawapo ya timu za Amerika Kusini ili kufuzu.

You can share this post!

SOKA MASHINANI: Athena FC yalenga kupiga hatua zaidi...

Oliech ajumuishwa katika kikosi cha Gor Mahia michuano ya...

adminleo