Forlan astaafu rasmi kucheza soka ya dunia
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
ALIYEKUWA mshambuliaji hodari wa Manchester United na timu ya taifa ya Uruguay, Diego Forlan ametangaza kustaafu baada ya kusakata soka kwa miaka 21.
Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 40 na ambaye aliwahi kuchezea klabu za Villareal, Atletico Madrid na Inter Milan, alitoa habari hizo kupitia kwa ukurasa wa mtandao mmojawapo wa kijamii.
Aliandika: “Baada ya miaka 21 nimeamua kustaafu kama mchezaji wa kulipwa. Nitaendelea kukumbuka miaka hiyo yote, lakini huenda nikapata kingine cha kufanya hivi karibuni. Shukrani kwa wote walioniunga mkono kwa muda huo wote.”
Forlan alijiunga na Manchester United akitokea Independiente ya Argentina, Januari 2002 kwa kitita cha Sh1 bilioni. Alisubiri hadi mwezi Septemba ndipo akafunga bao la kwanza, kabla ya baadaye kufunga mabao 17 katika mechi 98.
Ingawa hakuweza kung’ara sana alipokuwa Old Trafford, aliibukia kuwa mchezaji muhimu wa Villareal na Atletico.
Kadhalika aliifungia Uruguay mabao 36 katika mechi 112, mbali na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Copa America mnamo 2011.
Forlan alitwaa tuzo ya Golden Ball wakati wa fainali za Kombe la Dunia za 2010- ambako Uruguay ilitinga hatua ya nusu-fainali.
Vivyo hivyo alichezea klabu za Penarol, Mumbai City na pia Kitchee nchini Hong Kong.
Luis Suarez ambaye walicheza naye pamoja katika safu ya ushambuliaji katika timu ya taifa, amempongeza kwa kumsaidia kukuza kipaji chake. “Sitawahi kukusahau kutokana na mchango wake maishani mwangu. Nakupenda sana,” akasema.