Makala

BIASHARA PEVU: Mapato ya haraka katika zao la ‘zucchini’ yatakufanya urudie tena

August 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

ZUCCHINI ni viungo vya aina yake katika mapishi ambapo huongeza ladha kwenye mlo.

Kiungo hiki ambacho kinajumuishwa kwenye kundi la mboga, kimesheheni aina mbalimbali ya Vitamini, madini kama vile Manganese na Potassium ambayo ni muhimu katika kudhibiti shinikizo la damu (BP).

Wataalamu wa masuala ya lishe wanasema zucchini huwa na maji yake ya ndani kwa ndani, ambapo ikiliwa kama mboga husaidia kuimarisha usagaji chakula mwilini.

“Wenye mazoea ya kula kiungo hiki ni nadra kuwa na matatizo ya tumbo kama vile kusokotwa kwa kuwa mamumunya husaidia kukabili shida za aina hiyo. Pia, hushusha kiwango cha sukari mwilini hasa kwa wanaougua Kisukari,” anafafanua muuguzi na mtaalamu Leah Gitahi.

Sawa na karoti, Bi Gitahi anaeleza kwamba zao hili huimarisha uwezo wa kuona kutokana na kusheheni kwake Vitamini C na Beta-Carotene.

Isitoshe, yana Fiber na inaaminika kuwa kiwango chake cha mafuta ni cha chini mno, suala linalosaidia ueneaji sambamba wa damu mwilini. Mafuta yanapozidi mwilini, huziba mishipa jambo linalosababisha ugonjwa wa moyo na hata kushindwa kupumua.

Huchukua kati ya siku 45 hadi 60 kuvunwa, baada ya upanzi.

Kulingana na Bw Patrick Kamuni, mtaalamu kutoka Ken Agro Suppliers Ltd – kampuni ya kuuza mbegu, ni kwamba gharama ya kukuza zucchini ni nafuu ikilingalinishwa na mimea mingine.

Mdau huyu anasema mbegu zake hazihitaji kupandwa katika kitalu, ila hupandwa moja kwa moja shambani.

“Hayahitaji miche, hupandwa moja kwa moja, kazi ikiwa kuyatunza pekee na kuvuna,” anasema Bw Kamuni.

Kuna aina mbili za zucchini; ya kijani na manjano.

Hupandwa katika eneo tambarare (open field) au katika kifungulio/hema.

Bw Peter Mugo anayefanya kilimo hiki katika Kaunti ya Kajiado anasema magonjwa sugu ni; early na late blight, husababishwa na baridi ya majira ya asubuhi na jioni.

“Wadudu ninaoshuhudia ni viwavi, vipepeo na nzi wa matunda (fruit fly). Nzi huidunga mimea yake na kusababisha ioze na kufanya ikataliwe sokoni,” anaeleza Bw Mugo, akisema kuna haja ya mkulima kupata ushauri wa dawa bora kukabili magonjwa na wadudu.

Kukuza kwenye hema

Mtaalamu Patrick Kamuni anasema ekari moja inahitaji sacheti ya gramu 500 za mbegu za zucchini.

Gramu 100 hugharimu kati ya Sh3,200 na Sh3,400.

Aidha, hustawi maeneo yenye joto na kupokea kiwango cha mvua ya kutosha.

“Maji ni kiungo muhimu katika kustawisha kilimo chake. Yasiyopokea mvua ya kutosha, mkulima atumie mfumo wa kunyunyizia maji mashamba,” anahimiza Bw Kamuni.

Eneo la upanzi linapolimwa, ufanye udongo uwe mwepesi na mwororo.

Andaa mashimo, nafasi kati yake iwe karibu sentimita 45. Laini ya mashimo hadi nyingine iwe na kimo cha sentimita 60.

Weka mbolea au fatalaiza kwenye mashimo yale, ichanganye sambamba na udongo uliotolewa shimoni. Rejesha mchanganyiko huo, halafu upande mbegu na kuzifunika kwa udongo kiasi.

“Nyunyizia maji kwa kipimo, ingawa pia kuna wanaomwagilia mashimo maji kabla ya upanzi,” anashauri Kamuni.

Kifuatacho, ni matunzo kwa njia ya kunyunyizia maji. Mbegu huchipuka ardhini kati ya siku ya tano hadi wiki moja baada ya upanzi.

“Wakati jua limeangaza au msimu wa kiangazi, mimea hii inyunyiziwe maji asubuhi na jioni,” ahimiza mtaalamu Kamuni.

Palilia kuondoa makwekwe.

Wiki ya tatu, mimumunya huanza kuchana maua dalili kuwa utundaji unabisha hodi. Katika kiwango hicho, mkulima anahimizwa kuitia fatalaiza yenye madini ya Nitrogen, Potassium na Calcium (NPK).

Bw Kamuni anasema fatalaiza hiyo husaidia katika uundaji wa mboga zenyewe au zucchini.

Huo pia ni wakati muhimu kwa mkulima kuanza kutafutia mazao yake soko.

Siku ya 45 huanza kuvuna, na kulingana na Patrick Kamuni ekari moja ina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 25-30 za zucchini.

Aghalabu, kilo moja huuzwa Sh30.