Habari

Kuna manufaa Mwangi Wa Iria kutumia Sh1bn 'kuimarisha' mavuno ya mahindi?

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

KWA miaka minne sasa mfululizo, serikali ya Kaunti ya Murang’a imekuwa ikitoa ufadhili wa Sh250 milioni kila mwaka, kujumuika katika Sh1 bilioni hadi sasa, katika kufadhili wakulima wake wazidishe mavuno ya mahindi.

Katika ufadhili huo, amekuwa akitoa mbegu, fatalaiza na dawa za kupambana na magonjwa na wadudu kwa takribani wakulima 300,000 wa kaunti hiyo.

Mei 2019 akizindua awamu ya msimu wa kwanza wa 2019 wa upanzi wa mahindi ambapo alitoa vifaa hivyo alisema kuwa alikuwa akilenga kaunti ivune magunia Milioni moja ifikapo Agosti mwaka huu.

Sasa, afisa wa ustawishaji kilimo cha nafaka katika kaunti ya Murang’a, James Miriti anasema kuwa uwezo kamili wa kaunti hii wa mavuno ya mahindi Agosti ni magunia 50, 000 pekee. Hiyo ina maana kuwa Kaunti itakosa lengo lake la mavuno kwa magunia 950, 000 hii ikiwa ni asilimia 94.

“Mavuno hayo yatafeli kwa kiwango hicho kwa kuwa mvua ilikosekana kabisa na pia kukazuka athari hasi za dudu la fall army worm, ugonjwa wa Maize lethal necrosis disease na pia uvamizi wa tumbili katika mimea,” asema Bw Miriti.

Alisema kuwa Kaunti iko na wakulima 300,000 ambao kwa kila mmoja ukadiriaji ulikuwa mavuno ya magunia 3.5, hali ambayo kwa sasa kwa wengi ni ndoto na watakaovuna, wakiwa na uwezo wa bahati ya kutinga magunia 50,000.

Bw Miriti anasema kuwa usaidizi wa Kaunti ungeelekezwa kwanza katika uafikiaji wa maji ya unyunyiziaji akionya kuwa “hali ya hewa katika kaunti imekuwa hasi kwa miaka mingi sasa hali ambayo ufadhili wa Sh1 bilioni wa serikali ya kaunti umeishia kuwa tu wa kuzamisha pesa.”

Wa Iria alisema “ni jukumu la kila gavana wa hapa nchini kuweka mikakati ya kuwahami wakulima wa kwake na ujuzi na uwezo wa kukuza chakula cha kutoshelesha mahitaji ya Kaunti na hatimaye kubakisaha kingine cha kushirikisha biashara.”

Wa Iria akiwa katika harakati za kutoa fatalaiza ya bure kwa wenyeji hakuchelea kila wakati kusema kuwa “utepetevu wa serikali za Kaunti na ambazo zimetwikwa wajibu wa kusimamia kilimo ndio kiini cha mahangaiko ya njaa mashinani.”

Wa Iria alisema kuwa mradi huo sasa utakuwa wa kila mwaka kuongeza miaka miwili sasa ambayo umekuwa ukiendeshwa na serikali yake.

Alisema kuwa changamoto ya ukosefu wa mvua ya kutosha itakabaliwa na utoaji maji ya kutosha ya kushirikisha kilimo cha unyunyiziaji mimea maji.

Alisema kuwa serikali za Kaunti zilipendekezwa na Wakenya ili kuzima “muundo mbinu wa utata wa kutafuta maendeleo kutoka Nairobi. Ni jukumu letu kama magavana kuwapa Wakenya manufaa ya mfumo wa ugatuzi kupitia kutatua shida zao kutoka makao makuu ya Kaunti.”

Wa Iria alisema kuwa ikiwa kila gavana atatambua uwezo wa eneo lake kuhusu kilimo biashara na kisha atoe ufadhili unaofaa, “basi masuala ya aibu kama Wakenya kulia njaa katika karne hii ya 21 yatakuwa tumeyazika katika kaburi la sahau.”

Kwa sasa, takwimu zinamuashiria kama aliyeota ndoto ya mchana, akatumia rasilimali nyingi kufadhili ndoto hiyo na kwa sasa matokeo ni hatari ya njaa na mito ya unga ya mahindi ya bei rahisi katika Kaunti hii ya ‘mbunifu Mwangi wa Iria.’