• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:16 AM
Ratiba ya Raga ya Dunia msimu mpya yatangazwa

Ratiba ya Raga ya Dunia msimu mpya yatangazwa

Na GEOFFREY ANENE

RATIBA ya Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande ya msimu 2019-2020 imetangazwa.

Msimu wa wanaume utaanzia mjini Dubai katika nchi ya Milki za Kiarabu mnamo Desemba 5-7, 2019 na kuzuru Cape Town nchini Afrika Kusini (Desemba 13-15), Hamilton nchini New Zealand (Januari 25-26, 2020), Sydney nchini Australia (Februari 1-2), Los Angeles nchini Marekani (Februari 29-Machi 1), Vancouver nchini Canada (Machi 7-8), Hong Kong nchini Uchina (Aprili 3-5), Singapore nchini Singapore (Aprili 11-12), London nchini Uingereza (Mei 23-24) na kufikia tamati mjini Paris nchini Ufaransa (Mei 30-31).

Duru za Dubai, Cape Town, Hamilton, Sydney, Hong Kong na Paris pia zitaenda sambamba na Raga ya Dunia ya wanawake ambayo itaanzia mjini Glendale nchini Marekani mnamo Oktoba 5-6, 2019.

Duru nyingine ya wanawake itasakatwa mjini Langford nchini Canada mnamo Mei 2-3, 2020.

Kenya imekuwa ikishiriki duru zote za Ragha ya Dunia ya wanaume tangu msimu 2002-2003. Ilikamilisha msimu uliopita wa 2018-2019 katika nafasi ya 13 kwa alama 37.

Ilihitaji kuingia robo-fainali kuu katika duru ya kufunga msimu jijini Paris kukwepa kuangukiwa na shoka.

Shujaa ya kocha Paul Murunga itashindania alama za msimu 2019-2020 dhidi ya Fiji, Amerika, New Zealand, Afrika Kusini, Uingereza, Samoa, Australia, Ufaransa, Argentina, Scotland, Canada na Uhispania zilizokamilisha msimu uliopita katika nafasi 12 za kwanza mtawalia.

Wales, ambayo ilimaliza msimu huo katika nafasi ya 14, pamoja na Ireland, ambayo imepandishwa daraja, zinakamilisha orodha ya mataifa 15 yatakayoshiriki duru zote 10 za wanaume.

Lionesses, ambayo ni timu ya wanawake ya Kenya, haijawahi kuwa timu inayoshiriki duru zote za Raga ya Dunia ya wanawake.

Imewahi kushiriki duru za Clermont nchini Ufaransa mwaka 2016 na Dubai mwaka 2018 kwa kualikwa.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nimempenda mwanamume kupitia simu na...

Wachezaji wawili waliopatikana na hatia ya ubakaji...

adminleo