• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
SIHA NA AFYA: Je, maboga aina ya ‘butternut’ ni salama kwa watoto?

SIHA NA AFYA: Je, maboga aina ya ‘butternut’ ni salama kwa watoto?

Na SAMMY WAWERU

KWA kawaida watoto wenye umri mdogo hulishwa chakula laini hasa kilichopondwapondwa.

Ndizi, mapapai, na maboga ni miongoni mwa chakula kinachopendekezwa.

Ni jukumu la mzazi, hasa nina kuhakikisha mwana anakula mlo kamilifu akiwa na umri mdogo ili kuimarisha viungo vyake vya mwili, ikiwa ni pamoja na kukua.

Katika maboma au familia nyingi, maboga maarufu kama ‘malenge’ ndiyo hulishwa sana kwa watoto wadogo.

Mbali na watoto, madaktari hushauri wagonjwa kuyala kwa wingi, hasa mbegu zake zilizosheheni madini aina ya Zinki.

Mbegu zake pia zinasagwa na kuchanganywa na unga wa ngano kupika chapati.

Aidha, maboga yamesheheni Protini na madini kadhaa kama vile Chuma, Kopa, Maginizia, Manganizi na Zinki.

Mbegu zake zinasemekana kusaidia kuepushia mlaji zaidi ya magonjwa 10 kama; ugonjwa wa moyo, Saratani, Kisukari na uvimbe.

Mbegu zenyewe zinasemekana kusheheni mafuta ya Omega-3, ambayo ni miongoni mwa mafuta muhimu mwilini.

Zao hili limegawanywa kwa makundi mawili, maboga asili na butternut-madogo kuliko yale asilia.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya afya, maboga asilia ndiyo bora na salama kulisha watoto.

“Ninachofahamu maboga asilia hayakuzwi kwa dawa kwa sababu ni vigumu kuathiriwa na magonjwa ama wadudu,” anaeleza mtaalamu Bi Ann Njeri.

Isitoshe, yanapandwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimohai ambapo hayatiwi fatalaiza wala mbolea yoyote yenye kemikali.

“Yanapandwa kwa mbolea ya mifugo au kuku, ambayo imeiva sambamba (decomposed manure),” anaeleza mtaalamu James Murage wa kutoka Safari Seeds; kampuni ya kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za mboga, nyanya na maboga.

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyu, yanachohitaji ni matunzo ya maji pekee baada ya upanzi.

Bw Murage anasema butternut hukumbwa na changamoto nyingi hususan athari za magonjwa na kushambuliwa na wadudu.

“Changamoto hizo zinadhibitiwa kwa kupulizia dawa za aina mbalimbali,” anasema.

Mbali na kupanda zao hili kwa mboleahai, anakiri mazao bora yanapatikana kwa kutunza miboga kwa fatalaiza ya kuinawirisha.

‘Butternut’ ni maboga madogo yakilinganishwa na yale asilia.

Rose Wanjagi, mkazi wa Kiambu anasema amelea watoto wake kwa kuwalisha maboga asilia.

“Tangu nitahadharishwe na daktari kuhusu ‘butternut’, niliacha kulisha watoto wangu. Yale asilia ndiyo bora na yanaimarisha afya ya mtoto,” anadokeza Rose ambaye ni mama wa watoto wawili.

Watoto hulishwa yale mwororo, yaliyoiva na kupondwapondwa. Maboga yanaweza kupikwa kwa kuchanganya na ndizi na viazi. Pia, huchemshwa, yanatiwa chumvi na kutumika kama kitafunio wakati wa staftahi.

Ni muhimu kutilia maanani maelezo ya madaktari pamoja na ushauri wa wataalamu wa masuala ya afya.

Kwa jumla, wasomi hawa wanahimiza mazao kuzalishwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimohai.

  • Tags

You can share this post!

Wachezaji wawili waliopatikana na hatia ya ubakaji...

Arsenal yaziba nyuma EPL iking’oa nanga leo usiku

adminleo