• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Wanyama fiti kuchezea Spurs dhidi ya Aston Villa

Wanyama fiti kuchezea Spurs dhidi ya Aston Villa

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache baada ya kukosa kupata klabu mpya katika kipindi cha uhamisho nchini Uingereza, Victor Wanyama anasemekana yuko fiti kwa mechi ya Tottenham Hotspur ya kufungua Ligi Kuu ya msimu 2019-2020 dhidi ya Aston Villa itakayosakatwa leo Jumamosi saa moja na nusu usiku uwanjani Tottenham.

Ujumbe kwenye mtandao wa Twitter wa Tottenham kuhusu hali ya Wanyama unasema kuwa viungo Wanyama na Muingereza Eric Dier “wamejiunga na wachezaji wengine kwa mazoezi makali.”

Ripoti zaidi zinasema kuwa nahodha huyu wa Harambee Stars, ambaye Spurs inatamani sana kuuza ama kukopesha kwa klabu nyingine, yuko sawa baada ya kupona jeraha la goti.

Wolves, West Ham, Brighton, Burnley, Southampton, Everton na washiriki wapya wa EPL, Sheffield United, walikuwa katika orodha ya klabu zilizoaminika kutaka huduma za Wanyama katika kipindi cha uhamisho cha mwaka 2019 kilichoanza Mei 17 na kutamatika Agosti 9.

Hata hivyo, kufikia siku ya mwisho ya shughuli hiyo, hakuna klabu kutoka nchini Uingereza ilikuwa imetafuta huduma zake.

Wanyama alikosa maandalizi ya Tottenham ya msimu mpya zikiwemo mechi za kirafiki dhidi ya miamba wa Ujerumani Bayern Munich (Julai 31), Waitaliano Juventus (Julai 21) na Inter Milan (Agosti 4) na Manchester United (Julai 25) kutokana na kuongezewa likizo baada ya Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri na jeraha la goti.

Magoti

Majeraha ya magoti yamekuwa yakimsumbua Wanyama na kuisukuma Spurs kutafuta viungo Tanguy Ndombele kutoka Lyon na Giovani Lo Celso kwa mkopo kutoka Real Betis katika kipindi cha uhamisho.

Katika mchuano huu wa 164 kati ya klabu hizi mbili, Tottenham itatumai kuendeleza ubabe wake hadi ushindi nne mfululizo.

Spurs ilichabanga Villa nyumbani 3-1 na ugenini 2-0 katika Ligi Kuu ya msimu 2015-2016 na kuilima 2-0 kwenye Kombe la FA mwaka 2017.

Tottenham imepoteza dhidi ya Villa mara moja pekee katika mechi 17 zilizopita ambayo ilikuwa 1-0 uwanjani White Hart Lane mwezi Aprili 2015.

Spurs imeshinda Villa mara tisa kati ya mechi 10 zilizopita ikifunga mabao 24 na kufungwa matatu pekee.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Sifa kedekede kwa kazi nzuri

MACHO KWAO: Manchester City waanza safari ya kutetea taji...

adminleo