Alia kujua watoto si wake
Na BENSON MATHEKA
NDENDERU, KIAMBU
JOMBI wa hapa alitokwa na machozi mkewe alipomfahamisha kuwa hakuwa baba mzazi wa watoto wake watano.
Inasemekana kuwa jamaa alimuoa mwanadada huyo miaka sita iliyopita akiwa na mtoto mmoja na walikuwa wakiishi kwa amani.
Mkewe alizaa watoto wengine wanne na jamaa akawa akitia bidii kutunza familia yake.
“Jamaa alihakikisha watoto wake wamepata malezi mazuri. Alikuwa akijinyima starehe nyingi na alikuwa mume na baba wa kupigiwa mfano eneo hili,” alisema mdokezi.
Inasemekana miezi michache iliyopita alianza kuugua na ikawa vigumu kufanya kazi.
“Alilazwa hospitalini akiwa katika hali mahtuti lakini mkewe hakuenda kumjulia hali. Alishughulikiwa na ndugu yake hadi akapona. Siku aliyoondoka hospitalini, alishangaa kufika kwake nyumbani na kupata mkewe akiwa na mwanamume mwingine,” alisema mdokezi.
Duru zinasema kuwa mkewe hakushtuka wala kumkaribisha nyumbani. Aliondoka na kumsindikiza mwanamume huyo na kumuacha jamaa ambaye alimpigia ndugu yake simu na kumweleza aliyopata kwake.
Kulingana na mdokezi wetu, mkewe alirudi siku iliyofuatia na mumewe alipomuuliza kwa nini alikuwa akimdharau kwa kualika mwanamume kwake. Duru zinaeleza kuwa mkewe alimkemea na kumwambia kuwa huyo ndiye baba halisi wa watoto wake.
Mkewe alimwambia ajitayarishe kuwa akimuona mwanamume huyo mara nyingi kwa sababu ndiye baba wa watoto wake. Jamaa hakuamini masikio yake. Kwa sababu hakuwa na nguvu baada ya kuugua kwa muda, alitokwa na machozi.
Alihamia kwa ndugu yake ambaye alimshauri amteme mwanamke huyo. Kwenye kikao cha familia, mwanadada alisisitiza kuwa jamaa hakuwa baba wa watoto wake.
Alisema alikuwa akimtumia jamaa kumsaidia kulea watoto na kwa sababu hakuwa na nguvu za kufanya kazi baada ya kuugua, hakuwa na thamani yoyote kwake.
Siku hiyo, alihama nyumba ya jamaa huyo na haikujulikana iwapo alienda kuishi na mwanaume huyo mwingine.