Mpango wa Mathare Flames kutwaa taji msimu huu
Na JOHN KIMWERE
KAMPENI za kufukuzia taji la Super Eight Premier League (S8PL) msimu huu zinaendelea kuwasha moto huku mahasimu wakuu wakitoana kijasho.
Mathare Flames FC awali ikifahamika kama Zamalek FC ni kati ya vikosi vinavyotesa wapinzani wengine wakitafuta ubingwa wa taji hilo.
Kocha wake, Julius Katenge Mativo anasema ”Licha ya wanasoka wengi kusepa mwaka 2017 nashukuru naendelea kukuza wengine ambao wamepania kuonyesha weledi wao ili kuibuka wafalme wa ngarambe ya muhula huu.”
Mbio za kipute cha msimu huu zimeshuhudia vita vya kufa mtu baina ya mabingwa watetezi, Jericho Allstars, Meltah Kabiria FC, Mathare Flames, Githurai Allstars inayoshiriki mara kwanza bila sahau wasomi wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya (TUK).
”Bila kujipigia debe wachana nyavu wangu wameamua kujituma mithili ya mchwa kupigania taji la msimu huu,” anasema na kuongeza kuwa hawana hofu kabisa wala hawawezi kupuuza wapinzani wengine.
Anadokeza kwamba wamepania kutawazwa mabingwa wa migarazano ya msimu huu baada ya kuibuka mbili bora mara mbili kabla ya kumaliza nafasi ya 13 muhula uliyopita. Anaamini kikosi chake kimekaa vizuri kuvuruga ndoto za wapinani wengine hata hivyo anakiri kuwa kipute hicho bado ni wazi ambapo timu yoyote inaweza kutoka chini na kutawazwa mabingwa.
Mathare Flames chini ya nahodha, Jacob Bashir imekata tatu bora kwa alama 32, moja mbele ya Githurai Allstars baada ya kila moja kupiga mechi 18.
Nao mabingwa watetezi, Jericho Allstars ambayo hunolewa na kocha, Thomas Okongo ingali kifua mbele kwa kukusany pointi 36, nne mbele ya Meltah Kabiria FC. Ofisa mkuu wake, Moses Wambia Njoroge anasema kuwa wacheaji hao tayari wameonyesha wazi kuwa wanalenga kutinga upeo wa juu katika soka.
Mathare Flames iliyopatikana katika mtaa wa Mathare Area 4, Nairobi ilianzishwa mwaka 2004 na kujitwika jukumu la kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi mitaani.
Mathare Flames imenoa makucha ya wachana nyavu wengi tu ambapo baadhi yao hushiriki soka la kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya kama Derick Johana Omondi ambaye husakatia IF Brommapojkama nchini Sweden.
Pia wapo wengine zaidi ya wanane ambao hupigia klabu za Ligi Kuu ya KPL akiwamo Alphonce Ndonye (Mathare United), Robinson Kamura Mwangi (AFC Leopards) na Bernard Ongoma (Ulinzi Stars) zote Ligi Kuu ya KPL.
Kadhalika imepalilia Kennedy Otieno-Spitfire FC(Ligi ya Taifa Daraja la Pili), James Mandela na Julius Gitau wote-Naivas FC (Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza) na Victor Oduor Kwena-Bidco United(Supa Ligi ya Taifa-NSL),
Mathare Flames inajumuisha wachezaji hawa: James Hassan, Kevin Ochieng, Alfred Omulo, Gilbert Otieno, Samson Ambei, Jacob Bashir (nahodha), David Okeyo, Raphael Kamau, Vincent Masime, Haron Omwenga, Meshack Bwire, Wisdom Obina, Joshua Okena, Abdullah Ekeno na Alfonce Musyoka. Pia wapo Felix Juma, Eric Ochieng, Gladson Hardson, Feissal Kedir na James Omondi.
”Katika mpango mzima hatuna la ziada mbali tumepania kuendeleza mtindo wetu kunoa wanasoka chipukizi mitaani ili miaka ijayo kuibuka kati ya wachezaji watajika duniani,” meneja wake, Cainain Webere anasema.
”Bila kuweka katika kaburi la sahau napongeza Extreme Sports ya Hussein Mohamed ambayo huandaa mechi za kipute hicho,” ofisa mkuu huyo alisema.
Kipute cha S8PL kimetoa fursa kwa wachezaji kutambuliwa uwezo na kusajiliwa kuchezea timu za ligi za juu hpa nchini.