Miguna aitaka Jubilee imuombe radhi mara 21!
Na VALENTINE OBARA
MWANAHARAKATI wa upinzani aliyetimuliwa nchini na Serikali ya Jubilee, Dkt Miguna Miguna sasa anataka serikali imwombe msamaha mara 21 kwa jinsi alivyofurushwa.
Kwenye kesi mpya aliyowasilisha katika Mahakama Kuu, ambapo ameshtaki maafisa 25 wa serikali, Dkt Miguna anataka mahakama iagize kwamba msamaha huo uchapishwe kwenye magazeti matatu ya kitaifa kwa siku saba mfululizo.
Vilevile, anataka serikali iagizwe kumlipa ridhaa kwa uharibifu uliofanywa nyumbani kwake alipokuwa akitafutwa.
Dkt Miguna alikuwa mmoja wa wanachama wakuu wa Muungano wa NASA waliokuwa wakaidi zaidi dhidi ya utawala wa Jubilee kabla Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Alihusika pakubwa katika shughuli ya kumlisha kiapo Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ndipo serikali ikadai alikuwa nchini kiharamu kwa vile ni raia wa Canada.
Maafisa wakuu wa serikali ambao ameshtaki upya wanajumuisha Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki, aliyekuwa Mkurugenzi wa Uhamiaji na Usajili wa Watu Gordon Kihalangwa, Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) George Kinoti na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet.
“Mnamo Desemba 2017, washtakiwa walishirikiana kuunda genge…lililoagizwa kufuatilia mienendo yangu kinyume cha sheria, kuchunguza nyumba yangu na kunijeruhi, kunitesa kwa nia ya kuniua,” akadai wakili huyo.
Alilalamika kwamba wakati mwingi alipokamatwa, serikali ilimchukulia kama mhalifu na kumwaibisha mbele ya umma ilhali hakuwa na hatia yoyote.
Kulingana naye, washtakiwa pia walishirikiana kukaidi maagizo ya mahakama yaliyotaka aachiliwe huru alipokamatwa mapema mwaka wa 2018, wakazidi kumfunga katika seli chafu bila mahitaji muhimu ikiwemo chakula na maji.
Mnamo Machi 26, 2018, Dkt Miguna alijaribu kurudi nchini lakini akazuiliwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) ambako anadai alifungiwa chooni na akakosa kuoga wala kupiga mswaki kwa siku tatu.