• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
SHINA LA UHAI: Changamoto ya majitaka katika miji yetu

SHINA LA UHAI: Changamoto ya majitaka katika miji yetu

Na BERNARDINE MUTANU

KIJIBARIDI kikali, manyunyu, ardhi iliyoloa maji na msongamano wa makazi ndio mandhari ninayokumbana nayo katika mtaa duni wa Katwekera, Kibera, ila hayo hayakunasa jicho langu kama mtiririko wa maji machafu yaliyokuwa yakibubujika chini ya mwamba mkabala wa kijiji hicho.

Ni bomba lililo wazi la maji taka ambayo yanapitia katika vijiji kadhaa vikiwemo Kisumu Ndogo, Lindi, Siranga, Soweto, Makina, Kianda na Laini Saba.

Maji hayo hutiririka na kujiunga na Mto Nairobi (Nairobi River) na kuishia katika Bwawa la Nairobi (Nairobi Dam).

Ni hapa ninakutana na Joshua Mungai, baba ya watoto watano akiwa amekalia mwamba huo huku akipekua kamba za plastiki atakazouza kujipatia pato.

Anaeleza kuwa ameishi Kibera kwa miaka 40 na ameshuhudia maji hayo yakibadilika kutoka maji safi hadi kugeuka ‘kijito cha maji machafu’.

“Maji yaliyokuwa safi na tuliyokuwa tukitumia yalichanganyika na maji taka na hayafai tena kwa matumizi ya nyumbani,” aeleza.

Kando ya bomba hilo ni mifereji ya maji safi ambayo husambaza maji kwa wakazi wa eneo hilo.

Vitongoji duni

Hii ni sura unayokumbana nayo katika kitongoji duni cha Kibera na maeneo mengine jijini Nairobi ambayo hayana mfumo wa kupitisha maji taka na kinyesi na ambamo baadhi ya wakazi (asilimia nne) bado huenda haja katika eneo wazi.

La kusikitisha ni kuwa Bw Mungai hana uhakika ikiwa maji yaliyo miferejini ni safi, hasa kutokana na hali kwamba hupita karibu na bomba hilo la majitaka.

Lakini anachokifahamu fika ni yanakoelekea maji hayo; katika Mto Nairobi, umbali wa kilomita moja au mbili.

Anaeleza maji hayo hupitia katika vijiji vya Soweto (Mashariki and Magharibi), Makina, Kianda, Mashimoni and Laini Saba na hatimaye kuishia katika Bwawa la Nairobi.

Tofauti na maeneo mengine yaliyounganishwa na mfumo wa kupitisha maji machafu au yana matangi (septic tanks), vitongoji duni mjini havina mfumo huu, yasema Bodi ya Kudhibiti Huduma za Maji-WASREB.

Baadhi ya wakazi wa jiji kuu wakiwa kando ya Nairobi River mnamo Juni 16, 2019. Picha/ Lucy Wanjiru

Kwa kawaida, uchafu huo unafaa kusafirishwa hadi katika kituo cha kusafisha maji machafu kabla ya kuachiliwa kutiririka na kujiunga na mito au mikondo ya maji.

Lakini miezi kadhaa iliyopita, kulizuka mdahalo mkali mtandaoni baada ya lori la kubeba majitaka (exhauster), kunaswa kwenye kamera likimwaga uchafu huo kando ya barabara ya Northern Bypass.

Na sio hilo pekee, malori mengine pia yamepigwa picha yakimwaga maji machafu katika mito au mabomba ya kupitisha maji ya mvua.

“Hata eneo la Ruai, ambako malori hayo yanafaa kumwaga uchafu huo, ni sehemu moja tu kati ya tisa ambayo hutumika, mengine nane yaliharibika na kufungwa kwa sababu za kiusalama,” akasema waziri msaidizi katika Wizara ya Maji na Usafi Kaunti ya Nairobi, Winnie Guchu wakati wa warsha kuhusu Usafi na Maji majuzi, mjini Nakuru.

Akaongeza: “Ni eneo moja tu lililosalia Njiru, na Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Mazingira (NEMA) inataka kulifunga pia. Lakini swali ni je, wakifunga, malori ya kusafirisha maji machafu yatamwaga wapi? Shughuli bado zinaendelea humo sio sababu ni salama, ila ni hakuna eneo lingine. Tunahitaji maeneo mengine ya kumwaga maji taka. Pesa zipo lakini tumekosa ardhi kwa sababu wamiliki wa mashamba wanapinga ujenzi huo kwenye ardhi yao.”

Isitoshe, kituo cha kusafisha majitaka cha Kariobangi kilifungwa mwaka 2018 ili kikarabatiwe hivyo majitaka yote ambayo yalikuwa yakipitia huko, yanatiririka moja kwa moja hadi Mto Nairobi.

La kushangaza ni kuwa si Nairobi pekee ambayo ina mfumo mkubwa zaidi wa kupitisha maji taka nchini (asilimia 50) inayokabiliwa na changamoto hii, hali ni hiyo hiyo maeneo mengine nchini.

Kwa jumla, mfumo wa kupitisha maji taka nchini ni asilimia 16 pekee, ambapo ni miji 32 pekee kati ya 215 katika kaunti 26, ambayo ina mifumo ya kisasa ya kupitisha maji taka kulingana na ripoti ya 11 kuhusu Maji na Usafi 2017/2018 (Impact Report) iliyotolewa hivi majuzi na WASREB.

Kaunti zilizo na mfumo mkubwa zaidi wa kupitisha maji taka ni Nairobi (asilimia 50), Kisumu (asilimia 49), Laikipia (asilimia 36), Trans Nzoia (asilimia 34) na Bungoma (asilimia 34). Na kaunti zilizo mdogo zaidi ni Garissa (asilimia sita), Murang’a (asilimia tano), Meru (asilimia tano), Homa Bay (asilimia nne) na Busia (asilimia mbili).

Ripoti hiyo pia ilielezea kuwa miji na masoko katika kaunti 21, hakuna mfumo wowote wa kupitisha na kusafisha kinyesi na maji taka. Aidha asilimia 84 ya wakazi wote katika maeneo ya miji nchini huwa hawategemei mifumo ya kupitisha maji machafu na kinyesi ila hutumia matangi (septic tanks), mashimo na vyoo vya kisasa ambavyo huwa havitumii mfumo huo.

Hata hivyo, kuwepo kwa mfumo wa kupitisha maji taka sio dhamana ya usafi kamili nchini. Kwa mfano, Jijini Nairobi, ni asilimia 41 pekee ya maji taka na kinyesi ambayo hufika katika kiwanda cha kusafisha maji machafu na kinyesi cha Ruai. Isitoshe, ni asilimia 29 pekee ya uchafu huo ambayo husafishwa, kulingana na Caroline Kabaria, mtafiti wa shirika la Africa Population and Health Research Centre (APHRC), aliyezungumza wakati wa warsha hiyo mjini Nakuru.

Aidha jijini Nairobi, asilimia tisa ya maji taka na asilimia 30 ya kinyesi huwa haiwasilishwi ili kusafishwa. Asilimia 15 ya kinyesi hutiririka bila kudhibitiwa (kuhifadhiwa kwa matangi au mashimo) na kati yake ni asilimia tatu pekee ambayo huzolewa na kumwagwa katika maeneo yanayofaa.

Licha ya asilimia 31 ya kinyesi kudhibitiwa (katika matangi na mashimo), ni asilimia 27 pekee ambayo humwagwa.

Kulingana utafiti wa Benki ya Dunia 2015, asilimia 12 ya maji taka ambayo huwasilishwa ili kusafishwa huwa hayasafishwi, na asilimia 12 ya kinyesi huachiliwa kwenye mazingira bila kusafishwa. “Ni asilimia 34 ya maji taka na kinyesi, ambayo husafishwa kikamilifu Nairobi ilhali asilimia 66 sio safi,” akasema Bi Kabaria.

Kadhalika ripoti hiyo ya APHRC, inasema licha ya kuwa idadi ya wasiotumia vyoo imepungua nchini, asilimia 12 bado huenda haja kubwa nje.

Bi Guchu alielezea hofu yake kwamba kiwango kikubwa cha maji taka au kinyesi hakijulikani kilipo, kumaanisha kuwa huwa hakisafishwi, hali ambayo inazidisha kiwewe kuhusu kuzuka kwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

“Uchafu huo hauko kwenye mabomba wala ardhini. Lakini sharti upo mahali fulani; baadhi ya watu husema upo mitoni na si ajabu kuwa katika baadhi ya maeneo, mito hiyo hujulikana kama ‘sewage’. Tunahitaji kusemezana wazi na kuambiana ukweli, tunajua hali ni mbaya na tunahitaji kukabiliana nayo haraka iwezekanavyo,” akasema, na kuongeza kuwa uchafu hugharimu serikali Sh27 bilioni kila mwaka.

Kenya iliweka azimio la kuhakikisha asilimia 40 ya uchafu wa kinyesi unakusanywa na kusafishwa katika maeneo ya miji na asilimia 10 katika maeneo ya mashambani kufikia 2015, lakini miaka minne baadaye, bado ni ndoto.

Kulingana na WASREB, maeneo ambako nyumba zimejengwa kiholela, na yale ambayo matumizi ya maji yamo chini, ni vigumu sana kuwa na mfumo wa kupitisha maji machafu.

Pia, kulingana na ripoti hiyo, kuna maeneo ambayo kuna mfumo wa kupitisha maji taka lakini watu wengi hawajaunganishwa kwa sababu ya gharama kubwa ya kudumisha mfumo huo au mfumo wenyewe umeharibika.

Kudhibiti majitaka

Aidha WASREB inasema, huenda huduma za kusafisha maji taka na kinyesi hazishughulikiwi nchini kwa sababu uchafu huo huaminika unatokana na maji ya kawaida.

“Ni kawaida kwa mabomba ya maji taka kuvuja katika miji mingi na kusababisha mikurupuko ya magonjwa kama vile kipindupindu,” inasema ripoti hiyo.

Kulingana na shirika hilo, ukosefu wa mabomba na mifumo ya kupitisha maji taka unahatarisha maji yaliyoko ardhini na kuchafua vyanzo vya maji.

Hali itakuwa mbaya zaidi kutokana na ongezeko la miji mikuu na idadi ya watu nchini. “Tunahitaji kuwa wabunifu zaidi kuhusu jinsi tunavyokabiliana na maji taka. Kuna haja kubwa ya kusafisha maji hayo na kinyesi karibu na yanakotoka, hasa jijini Nairobi kwa sababu mfumo uliopo umeshindwa kusuluhisha changamoto inayotukabili,” akasema Bi Guchu.

Kwa sasa, maji taka husafishwa mbali na makazi, umbali wa kilomita kadhaa, kabla ya kuachiliwa kujiunga na mikondo ya maji.

Kulingana na Bi Guchu, ikiwa shughuli za kusafisha majitaka na kinyesi zinaweza kuletwa karibu na maeneo yanakotoka, huenda hali ikadhibitiwa.

“Ikiwa tunaweza kudhibiti majitaka kuanzia Ngong kupitia katikati mwa jiji mpaka mahali ambako Mto Nairobi unajiunga na Mto Athi, tutafaulu,” akaongeza.

“Serikali ya Kaunti ya Nairobi inafanya kazi nzuri kuondoa takataka Mto Nairobi, lakini pia tunahitaji kuhakikisha kuwa maji taka hayachanganyikani na maji safi mtoni,” akasema na kutoa wito kwa serikali za kaunti kuiga mfumo unaotumiwa na kampuni ya Maji na Usafi ya Nakuru.

Ikilinganishwa na mfumo wa kawaida ambao ujenzi uhitaji sehemu kubwa ya ardhi na na kuchukua miaka kadhaa, mfumo unaotumiwa Nakuru umejengwa katika nusu ekari pekee na ujenzi ulimalizika katika kipindi cha miezi mitatu pekee.

“Tukipata mifumo midogo kama hiyo katika maeneo yote ya miji, tunaweza kuwa tumepata suluhu katika kudhibiti maji taka na kuzuia maji hayo kuingia katika mikondo ya maji safi,” akasisitiza na kuongeza kuwa maji taka yaliyosafishwa yanaweza kutumiwa tena nyumbani na shambani.

Alisema serikali ya kitaifa itazisaidia serikali za kaunti kujenga mifumo kama hiyo kwa kutoa wataalamu na muundo msingi ili kusaidia kutimiza malengo ya usambazaji wa mfumo wa kupitisha maji taka mijini kufikia 2030.

You can share this post!

KIPAJI: Aanzisha shule ya kutoa mafunzo ya usanii

ATHARI ZA PLASTIKI: Walaji samaki wa baharini wanajaza...

adminleo