Watu kadha waugua kipindupindu Mandera
Na MANASE OTSIALO
WATU sita wametengewa sehemu maalumu kutibiwa kipindupindu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Takaba, Kaunti ya Mandera.
Afisa wa Afya, Bi Rahama Abdullahi amesema sampuli nne zilizopelekwa katika maabara ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiafya Nchini (Kemri) zilibainisha ugonjwa wa kipindupindu.
“Wagonjwa wanne walilazwa Ijumaa wiki jana katika hospitali ya Takaba, sampuli zao zikafanyiwa uchunguzi na kubainika ni kipindupindu. Tayari wanaendelea kupokea matibabu,” akasema Bi Abdullahi.
Mnamo Jumapili, kituo hicho cha afya kiliwapokea wagonjwa wengine wawili wenye dalili za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Bi Abdullahi, wanashuku vyanzo vya maji katika vijiji vya Bula Elwak na Dikduro vilivyoko Mandera Magharibi vimekuwa ni kitovu kikuu cha kusambaa kwa ugonjwa huo.
“Tunashuku chanzo cha maji Bula Elwak na bwawa huko Bula Dikduro limechafuliwa. Hata hivyo, timu ya uangalizi iko nyanjani,” amesema.
Afisa wa Afya ya Umma Mandera Magharibi Bw Ibrahim Karim kupitia ilani ya umma Agosti 11, alifunga maeneo ya vyakula; hasa magengeni.
Pia maduka ya kuuza miraa, maziwa, na nyama yamefungwa.
“Ninawashauri wale wote wanaosafiri ama kwa kuingia au kutoka mjini Takaba kuchukua dawa za kinga dhidi ya kipindupindu katika kituo cha afya kilicho karibu,” inasoma sehemu ya notisi hiyo iliyotiwa saini na Bw Karim.
Mwaka 2016 ndio ulikuwa mbaya zaidi Mandera pale Juni 2016 kipindupindu kilisababisha vifo vya watu 19 na wengine 1,200 wakaambukizwa.