• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Eliud Kipchoge kuwekewa kasi na ndugu watatu kutoka Norway

Eliud Kipchoge kuwekewa kasi na ndugu watatu kutoka Norway

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Eliud Kipchoge atawekewa kasi na ndugu watatu kutoka Norway – Henrik, Filip na Jakob Ingebrigtsen – atakapojaribu tena kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa 2:00:00 jijini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 12, 2019.

Mkenya huyo, ambaye ni bingwa wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume ya saa 2:01:39, alikosa kwa sekunde 25 kutimka umbali huo chini ya saa mbili mjini Monza mwezi Mei mwaka 2017.

Katika jaribio lake la kwanza mjini Monza nchini Italia, Kipchoge, 34, aliwekewa kasi na gari pamoja na wakimbiaji ili kuzuia upepo kupunguza kasi yake.

Usaidizi huo ulimaanisha kuwa muda wake wa saa 2:00:25 haukuweza kutambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kama rekodi ya dunia. Rekodi yoyote itakayopatikana Vienna pia haitatambuliwa na IAAF.

Rekodi ya mwaka 2018

Rekodi ya dunia inayotambuliwa na IAAF ni saa 2:01:39 ambayo Kipchoge alitimka akishinda mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2018.

Henrik Ingebritsen, 28, alinyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Bara Ulaya mwaka 2012.

Filip, 26, alishinda nishani ya shaba katika mbio hizo za mizunguko mitatu katika Riadha za Dunia mwaka 2017.

Naye Jakob, 18, tayari ni bingwa mara mbili wa Bara Ulaya baada ya kutwaa mataji ya mbio za mita 1,500 na mita 5,000 jijini Berlin mwaka 2018.

Kipchoge pia aliibuka mfalme wa mbio za London Marathon nchini Uingereza mwezi Aprili 2019.

Ameshinda marathon 11 kati ya 12 ameshiriki tangu ajitose katika mbio za kilomita 42 mwezi Aprili mwaka 2013.

Alimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Mkenya mwenzake Wilson Kipsang’ katika Berlin Marathon mwaka 2013.

You can share this post!

MAPISHI NA UOKAJI: Jinsi ya kuandaa tosti zenye ndizi

KILIMO: Upanzi wa mchicha

adminleo