AKILIMALI: Wanafunzi wavalia njuga kilimo kwa faida ya shule yao
Na RICHARD MAOSI
SAFARI yetu mara hii inatufikisha katika Kaunti ya Samburu, ambayo inapatikana Kaskazini mwa Kenya ambako wakazi wengi ni wafugaji wa kuhamahama bila makazi ya kudumu.
Kutokana na hali halisi ya mambo, si rahisi kuwaona wakazi wakijishughulisha na kilimo cha mimea isipokuwa mifugo wanaopatikana kwa wingi, hii ni kutokana na hali mbaya ya anga isiyoweza kuhimili ukuaji wa mimea.
Licha ya changamoto nyingi, Akilimali, ilibahatika kujumuika na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Suguta Consolata wanaotunza mazingira licha ya uhaba wa maji. Wanafunzi hawa kadhalika wanakuza matunda katika mazingira magumu ya mawe.
Shule ya Suguta inapatikana katika kipande cha ardhi cha ekari tano hivi, ambapo usimamizi wa shule ulitenga nusu ekari ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa kupanda, kupalilia na kutunza mimea yao katika muda wao wa ziada.
Mpangilio mzuri wa mimea iliyojaa afya, matunda, miti na mchanga wenye rutuba ni baadhi ya mambo yaliyobainisha kuwa hawajavunjika moyo kupigana na ukame uliowakodolea macho tangu enzi za mababu zao.
Kulingana na mwalimu Burton Wefwafwa, mwalimu wa somo la Zaraa na msimamizi wa mradi wa kutunza mazingira, amejizatiti kuwafundisha wanafunzi wake jinsi ya kutumia malighafi haba ya maji yanayopatikana Samburu.
Anaeleza kuwa anatumia huduma za wanafunzi kutekeleza kila shughuli shambani wakati wao wa mapumziko, na hii ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wanatumia wakati wao vyema.
Licha ya wanafunzi wengi kukumbwa na changamoto ya mimba za mapema, wakazi kuibiana mifugo na ndoa za lazima, hizi zote ni kasumba zinazoendelea kupitwa na wakati.
Mwalimu Wefwafwa anasema wanafunzi kutoka Chama cha Mazingira shuleni (Enviromental Club) wamefanikiwa kushawishi shule zinazozunguka Consolata kutalii mazingira yao ya kilimo na kujifunza mengi.
Kutokana na mradi huo unaoshirikisha utunzaji wa mazingira, vibarua watatu wamefanikiwa kupata ujira, hususan wakati ambapo shule zimefungwa, kwani usalama unafaa kudumishwa.
Kwa kuwa wanafunzi wengi hapa wanatoka katika familia za wafugaji, upatikanaji wa mbolea ni jambo rahisi kwani wao hupata mbolea kutoka kwa mifugo wao wa nyumbani bila kugharimia.
Awali shirika la Maralal Caritas kutoka eneo la Maralal, liliwakabidhi wanafunzi pipa linaloweza kuhifadhi lita 10,000 za maji msimu wa mvua, ili yatumike kiangazi kinapokuja.
Licha ya changamoto za maji, wanaweza kunyunyizia mimea yao maji kupitia kwa mbinu ya unyunyiziaji wa matone (drip irrigation) ambapo maji hayawezi kuharibiwa wala kupotea.
Kutokana na machungwa na karakara (passion), shule hii huwalisha wanafunzi mara mbili kwa wiki kwa wiki 15 mfululizo zinazojaza muhula mzima na wakati mwingine zaidi.
Kwa hivyo, wanaweza kuokoa hadi Sh7,800 kila wiki ambazo ni takriban Sh32,000 kila mwezi wakati ambapo mavuno ni mazuri, na endapo makali ya jua hayatakausha mimea yao.
Kwa mfano msimu uliopita, Shule ya Consolata ilivuna matunda ya kutosha na hivyo basi hawakununua bidhaa hii kutoka sokoni.
Aidha, kuhusu mazao ya shamba kama vile sukuma wiki na spinachi, kwa wiki moja shule hii inaweza kuvuna hadi kilo 100 ambapo kilo moja huuzwa kwa Sh100 na kwa sababu hiyo wanaweka hadi Sh10,000 kila wiki.
Kwa jumla faida wanazopata wakulima wachanga katika Shule ya Msingi ya Suguta Consolata hutumika kukidhi mahitaji ya kimsingi kama vile kununua vitabu na kugharimia elimu ya wanafunzi wanaotoka katika familia maskini.
Mwalimu Wefwafwa anasema amekuwa akijaribu kuwahimiza wanafunzi kufahamu kuwa ni jukumu lao kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa faida ya kizazi cha baadaye.
“Kwa sababu wengi wao hawana ujuzi wa shambani, tunawahimiza kushirikiana katika makundi wakati wao wa mapumziko kutunza mimea yao,” akasema.
Dodi Lowapere, mwanafunzi wa darasa la nane, anatumai kuwa shule yake itaongeza nafasi ya kufanyia kilimo, ili wanafunzi zaidi waweze kushiriki.
Apata lishe mbadala
Anasema kulingana na desturi za jamii ya Wasamburu wamekuwa wakila nyama na maziwa kila siku lakini kila anapokuja shuleni amekuwa akipata lishe mbadala ya majani na matunda ambayo haijazoeleka sana katika jamii yao.
Anasema mradi wa kukuza mimea pia umewapa wanafunzi hamasa ya kuzingatia umuhimu wa kutunza mazingira kuanzia hatua ya utunzaji miche, kupanda na kuvuna.
Anasema licha ya changamoto za maji, ugumu umewafundisha kutumia malighafi haba kwa makini ili yaje kuwafaidi wao na wenzao.
Akilimali ilipata fursa ya kuzungumza na mtaalamu wa mimea kutoka eneo la Posta Lanet naye anasema ukulima katika maeneo kame unahitaji subira ya aina yake.
“Ili kutoa nafasi ya kurejesha virutubishi vilivyokuwa vimepotea ni lazima mkulima kuwa na subira ya hali ya juu,” akasema.
Tabitha anasema kuwa ingawa mboga za majani zinahitaji maji mengi, spishi ya spinachi inaweza kufanya vyema kwenye maeneo kame.
Aliongezea kuwa mkulima anayelenga soko la nje anaweza kupata hela nzuri, bora arekebishe kiwango cha asidi kwenye mchanga, kunyunyizia mimea yake maji na kutumia mbolea kwa wingi.