Ni kivumbi Kenya na Uzbekistan zikiumiza nyasi
Na GEOFFREY ANENE
SAA chache kabla ya timu za soka za Olimpiki za Kenya na Uzbekistan kupimana nguvu, kambi zote mbili zimeapa kuonyeshana kivumbi Machi 23 na Machi 26, 2018.
Kipa wa Ulinzi Stars, Timothy Odhiambo, ambaye ni nahodha wa timu ya Kenya, amenukuliwa na Shirikisho la Soka la Uzbekistan (UFF) akisema, “Hatuko hapa kutalii, bali tunataka kurejea jijini Nairobi na ushindi. Lengo letu ni kubwaga Uzbekistan.”
“Tulikuwa na habari finyu kuhusu timu ya Uzbekistan hadi pale iliposhinda taji la Bara Asia mapema mwaka huu,” Odhiambo aliongeza na kushukuru wananchi wa Uzbekistan kwa mapokezi mema.
Mvamizi wa Uzbekistan Bobur Abdukhalikov amebashiri kwamba michuano hiyo ya kirafiki ya Under-23 haitakuwa rahisi.
Katika mahojiano na UFF, mshambuliaji huyu wa klabu ya Nasaf amesema, “Mechi dhidi ya Kenya si rahisi. Hata hivyo, tutajikakamua kuweka tabasamu katika nyuso za mashabiki wetu.”
Kocha mkuu wa Uzbekistan, Ravshan Haydarov anaamini vijana wake wamejiandaa vyema. “Tuna mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu ya Olimpiki ya Kenya. Tumechukulia maandalizi yetu kwa uzito mkubwa. Tutajaribu kufurahisha mashabiki wetu kwa kutandaza soka safi na pia kupata ushindi,” Haydarov amesema.
Kenya, ambayo inanolewa na kocha Francis Kimanzi, na Uzbekistan zinajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020. Droo ya michujo hiyo bado haijatangazwa.