Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mbinu za sanaa katika Kiswahili

August 15th, 2019 3 min read

Na MARY WANGARI

[email protected]

Majazi

MAJAZI ni pale ambapo tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.

Kwa kawaida mbinu ya majazi huhusisha kumpa mhusika jina rasmi au jina la kuzaliwa linaloambatana na tabia, mienendo au sifa zake.

Kwa mfano msichana anaweza kupatiwa jina Rehema kwa maana ya kuwa msichana mzuri, mtulivu na mpenda amani.

Mhusika kwa jina Bahati anaweza kuashiria mtu mwenye nyota ya jaha.

Mwandishi pia anaweza kutumia mhusika Mzee Tumbo Kubwa kuashiria mtu anayependa kula sana kana kwamba hashibi.

Lakabu

Hii ni mbinu inayotumika wakati mhusika hupachikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia au sifa zake,

Lakabu inaweza kufafanuliwa pia kama majina yanayobandikwa watu kutokana na sifa zao, maumbile, hulka au mambo yanayowahusu.

Kwa mantiki hii, tunaona kwamba pana tofauti kuu kati ya lakabu na majazi ambapo majazi ni jina halisi la mtu ilhali lakabu ni jina la kupachikwa.

Mfano mzuri wa mbinu ya lakabu unajitokeza katika riwaya ya ‘Siku Njema’ ya mwandishi Ken Walibora ambapo mhusika mkuu, Msanifu Kombo, hubandikwa jina la “Kongowea Mswahili” kwa kufanya bidii sana na kubobea katika lugha ya Kiswahili.

Mhusika Mama Rita naye anapenda kuongea sana hivyo basi wanakijiji wakampachika lakabu ya kasuku.

Uzungumzi Nafsia (Monologue)

Katika mbinu hii, mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.

Aidha, uzungumzaji nafsia (nafsia) ni pale mhusika hujizungumzia mwenyewe kana kwamba anaongea na mtu mwengine. Mbinu ya uzungumzi nafsiya aghalabu hutumika kuonyesha mtiririko wa mawazo katika akili ya mhusika.

Kwa mfano:

“Sasa hata nikiwaambia ukweli hawataniamini. Lakini nikiwadanganya na wajue, watanichinja. Sijui nifanyeje?”

Ritifaa

Hii ni mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe. Kwa mfano: “Baba ooh Baba, mbona umeniacha nikihangaika? Ulipokuwa hai nilikula na kushiba, nilivaa vizuri lakini sasa tangu uende ninateswa na kukandamizwa. Tafadhali baba rudi. Toka kaburini uniokoe,”

Utohozi

Neno utohozi linatokana na kitendo cha lugha fulani kukopa maneno kutoka lugha nyingine katika juhudi za kurahisishia wenyeji matamshi pasipo kutafsiri. Ni mbinu inayohusisha uwasilishaji wa maneno ya lugha nyingine kwa njia inayoyafanya yatamkike kama ya Kiswahili.

Kwa minisketi kumaanisha miniskirt, blauzi kwa maana ya blouse, skrini kwa maana ya screen na kadhalika.

Kuchanganya ndimi

Hii inahusu hali ya kutumia zaidi ya lugha moja katika mawasiliano. Mbinu hii hujitokeza wakati sentensi moja au mzungumzaji anatoka kidogo katika lugha moja na kuingilia nyingine kisha akarejelea lugha ya awali.

Mbinu hii pia inaweza kufasiriwa kama kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili.

Kuhamisha ndimi

Hii ni mbinu inayohusu kubadilisha mkondo wa mazumgumzo kutoka lugha moja hadi nyingine ambapo msemaji ana umiliki wa zaidi ya lugha mbili.

Ni mbinu ya kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili.Ni bayana kwamba pana tofauti kati ya mbinu ya kuchanganya ndimi na mbinu ya kuhamisha ndimi. Huku mbinu ya Kuchanganya ndimi ikihusisha mwndishi kuchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu.

Methali (Proverb)

Methali zinaweza kufafanuliwa kama semi fupifupi za kimapokeo zenye kueleza fikira, maarifa, hekima na mafunzo yanayotokana na uzoefu wa jamii mahususi.

Aidha, methali ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa ambayo mhusika au mwandishi wa fasihi anaweza kuitumia kupitisha ujumbe fulani.

Taharuki (Suspense)

Hii ni mbinu ya kusimulia au kuandika kazi za fasihi andishi kama vile tamthilia, riwaya na kadhalika. Lengo kuu la taharuki ni pamoja na:

i. Kuifanya hadhira au wahusika wajawe na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye

ii. Kuibua hamu ya kutaka kuendelea kusoma au kusikiliza miongoni mwa hadhira

Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha hadhira yake ijijazie au ibaki ikijiuliza maswali.

Sadfa (Coincidence)

Hii ni mbinu inayoashiria hali ya mambo mawili yanayohusiana kutokea kwa wakati mmoja kana kwamba yalikuwa yamepangwa, japo hayakuwa yamepangiwa.

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania.” Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991) “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studie Ghent