Makala

KILIMO NA MAARIFA: Vyakula vinavyoweza kukuokoa dhidi ya kansa

August 15th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HUKU maradhi ya kansa yakizidi kukithiri, tafiti kadhaa zimeonyesha kwamba chakula tunachokula kinachangia pakubwa kuenea kwa aina mbalimbali za kansa.

Mojawapo ya njia ambazo zimeonekana kutia sumu kwenye chakula tunachokula ni kemikali zinazotumika katika ukuzaji vyakula vikiwa shambani.

Hii ni mojawapo ya mambo yaliyomsukuma Bi Felister Kimotho kujitosa katika ukulima wa vyakula pasipo matumizi ya viuadudu vilivyo na kemikali kali almaarufu organic farming.

Kwa miaka miwili sasa, Bi Kimotho amekuwa akiendesha kilimo hiki katika eneo la Kinangop, Kaunti ya Nyahururu ambapo anajivunia kupanda mboga za aina tofauti ikiwa ni pamoja na sukumawiki, spinachi na kabichi miongoni mwa zingine.

Kinachofanya kilimo hiki kuwa maalum ni kwamba badala ya kupanda mimea shambani, anazikuza kwenye magunia huku mimea kadhaa ikipandwa kwa kila mfuko.

Aina hii ya bustani inafahamika kama multi-storey garden kwa Kiingereza.

Bustani hii inaundwa kwa kutumia gunia la kawaida, mchanga, mbolea na mawe.

Kwa kawaida wao hutumia magunia yaliyokuwa yamehifadhiwa chakula cha kuku.

“Pia sisi hutumia mifuko ya kisasa kwa jina real ipm ambayo imesanifiwa kwa minajili ya upanzi wa aina hii kwani ina mashimo kila upande,” aeleza.

Kulingana na Bi Kimotho, hatua ya kwanza ni kulijaza gunia kwa mchanga, mbolea na mawe.

Mawe huhakikisha kwamba maji yanasambaa katika sehemu zote kwenye mfuko huo na hivyo kuhakikisha kwamba mimea yote inapata unyevunyevu,” aeleza.

“Kisha hatua inayofuatia inahusisha kupanda miche ya mboga kisha kuinyunyizia mbolea asili (mboji) zinazotokana na taka ya wanyama na mimea. Mbolea inawekwa mara moja pekee hadi mazao yatakapovunwa,” aeleza.

“Mbolea hii asili hasa hujumuisha mchanganyiko wa kinyesi na uchafu wa kuku ambao sisi hupata kutoka kwa wafugaji kuku eneo la karibu,” asema.

Aidha, anasema kwamba mbali na mbolea zinazopatikana kiasili, wao pia hutumia mbinu asili za kukabiliana na wadudu, kwa mfano kupanda mimea kama vile vitunguu, giligilani, Mexican gold na pareto ambazo hufukuza wadudu.

“Kwa kawaida, maji hunyunyiziwa mara moja kwa wiki hadi mimea itakapokomaa, ambapo mara nyingi huwa muda wa miezi mwili,” aeleza.

Mfuko mmoja unachukua nafasi ya mita moja mraba, kumaanisha kwamba unaweza kuwa na magunia kadha kwenye kipande kidogo cha ardhi.

Aidha, kwa kawaida gunia moja la real ipm limeundwa kumudu miche 50. “Hii ni sawa na gunia moja la kawaida, ambalo pia linamudu idadi sawa ya miche,” aeleza.

Kulingana na Bi Kimotho kwa kawaida huchukua siku moja na kupanda miche kisha miezi miwili kusubiri kwa mazao kuwa tayari kwa matumizi.

“Gunia moja la kawaida laweza kugharimu Sh2,000 kuliandaa, lakini kwa upande mwingine litakupa fursa ya kuvuna angaa Sh500 kila wiki, kwa muda wa mwaka mmoja. Hii ni sawa na Sh24,000 katika kipindi hiki,” anaeleza.

Kubadilisha

Ili kuimarisha mazao, anasisitiza kwamba mkulima anapaswa kubadilisha mchanga na mbolea kila baada ya mwaka mmoja.

Bi Kimotho alianza masuala ya kilimo miaka miwili iliyopita, wakati huo akiwa mwanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Naivasha Girls ambapo alikuwa mwanachama wa Young Farmers Club.

“Kutokana na penzi langu kwa ukulima pia nilipokea mafunzo kadha kuhusiana na aina hii ya kilimo kisichohusisha matumizi ya viuadudu vya kemikali kali. Pia, kutokana na kuwa wazazi wangu ni wakulima, penzi lao kwa shughuli hii lilinisukuma pia kujihusisha. Aidha, mafunzo niliyokuwa nikipata mtandaoni yaliongeza ari yangu,” asema.

Kutokana na manufaa haya, ameendeleza ujuzi wake miongoni mwa wanachama wa kikundi cha vijana cha Murungaru, eneo hilo. Pamoja wamekuwa wakieneza ujuzi huu kwa wakulima wengine katika eneo hilo.

Kikundi hiki ambacho kwa sasa kina wanachama watano kimetoa mafunzo kuhusu aina hii ya kilimo, ambapo tayari wakulima 20 kutoka eneo hilo wamenufaika na pia wameanza kujihusisha.

Kwa sasa ndoto yake ni kuongeza idadi ya mfuko hii sio tu nyumbani kwao, bali katika Kaunti nzima ya Nyahururu, na hata maeneo mengine nchini.