• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 9:41 AM
AKILIMALI: Kwake mbuzi wa maziwa wana faida tele

AKILIMALI: Kwake mbuzi wa maziwa wana faida tele

Na PHYLLIS MUSASIA

MUDA wake mwingi mfugaji Clement Ocharo wa kutoka Borabu, Kaunti ya Nyamira huutumia malishoni na mbuzi wake ambao pengine ndio marafiki wake wakubwa kwa sasa.

Anasema hupata raha kila wakati anapowaona wakikimbia hapa na pale na kuruka; hasa wanambuzi.

“Mara nyingi utanipata nikiwa nimewalea au kuwabeba kila wakati wanaponikaribia. Nimewalea kama wanangu na pia marafiki wakuu kwenye maisha yangu kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini,” anasema Bw Ocharo.

Kulingana naye, ufugaji wa mbuzi wa maziwa una manufaa mengi na ndio sababu tangu aanze mradi huo, ameamua ni kwenda mbele bila kurudi nyuma.

“Mwanzo, nilifuga mbuzi wa kawaida ikizingatiwa kuwa eneo hili liko kwenye mpaka baina ya Kaunti za Nyamira na Bomet na kwamba lilikuwa na sifa mbaya ya wizi wa mifugo,” akaeleza Bw Ocharo.

Anakiri wezi waliiba mbuzi wake hata akaanza kuwa na wazo la kuacha.

Mwaka wa 2008 Bw Ocharo anasema alibadilisha nia na kutaka kuwafuga mbuzi wa kisasa.

“Nilianza kutafuta mafunzo kuhusu njia bora za kuwatunza mbuzi hao kabla ya kuwanunua,” anasema.

Anaongeza kuwa, maafisa wa idara ya mifugo walimweleza ubora wa maziwa yatokanayo na mbuzi wa kisasa ilikilinganishwa na mbuzi wa kawaida.

“Maziwa ya mbuzi wa kisasa yana madini muhimu kwa mwili wa binadamu na pia ni dawa inayoweza kumsaidia mtu kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa,” anaeleza.

Kwa sababu ya bidii na ukakamavu wake, Bw Ocharo anasema kuwa aliwashawishi watu wengine na kwa pamoja wakaunda kikundi kimoja kwa jina la Nyainogu.

Kikundi hicho baadaye kiliwawezesha kupata mbuzi taribani 10 kupitia mradi wa serikali wa kuwawezesha wakulima wadogowadogo.

Malengo ya mradi huo ilikuwa ni kuwasaidia wakulima wadogo kunufaika kiuchumi na kuongeza hadhi yao ya maisha.

“Tulipata mbuzi wa kisasa aina ya ‘Kenyan Alpine’ na ‘Toggenberg’ ambao tumekuwa kwa muda wa miaka 10 sasa,” akasema.

Na kwa sababu ya maarifa aliyopata kwenye warsha na semina za mafunzo ya mara kwa mara, Bw Ocharo anasema mbuzi hao pamoja na wale wa kawaida, mbegu zao za uzazi zimechanganwa na sasa matokeo ni mbuzi wengine wa aina tofauti na ambao ni bora zaidi.

“Unapata kuwa kupata aina tofauti ya ng’ombe ambaye umemkutanisha na mwingine huchukua muda mrefu sana, hata miaka kumi. Lakini mbuzi wamenichukua muda mfupi wa miaka mitatu tu kupata aina tofauti na bora zaidi,” akasema kwa tabasamu.

Nyumbani kwake, ametengeneza kizimba cha mbuzi wake kwa kutumia mbao na magogo.

Kwa jumla, ana mbuzi wazima 34 na hadi tukichapisha makala hii, ana wanambuzi tisa.

Changamoto anazopitia mkulima huyo ni ugumu wa kupata mbegu bora za kutungisha mimba mbuzi wake wa kike.

Anasema kuwa ile ambayo inapatikana ni ghali mno.

“Kuna aina moja ya mbuzi wa kisasa wa kiume ambao wanamilikiwa na idara ya mifugo na mbuzi mmoja unaweza kumpata kwa Sh10,000 au hata zaidi,” anaeleza.

Changamoto nyingine anasema ni magonjwa na hali za kiafya kama vile pumu na homa kali itokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.

Magonjwa na hali hizi huwazidia hasa mbuzi ambao ni ama wadogo au ni wageni.

 

Bw Clement Ocharo akiwa nyumbani kwake Borabu – katika mpaka baina ya Kaunti za Nyamira na Bomet. Yeye ni mfugaji wa mbuzi wa maziwa. Picha/ Phyllis Musasia

Kulingana naye, mbuzi wana faida kwa mfugaji baada ya muda mfupi.

“Ninapata faida nyingi kutokana na maziwa ya mbuzi ambapo kila lita moja mimi huuza kwa Sh120,” akasema.

Anapouza mbuzi mmoja wa kike, yeye hupata zaidi ya Sh15,000 na yule wa dume ni Sh10,000 ikiwa amefikisha umri wa miezi sita kuendelea.

“Ufugaji wa mbuzi ni rahisi ikilinganishwa na ng’ombe kwani mbuzi huitaji nafasi ndogo tu. Chakula chao ni nyasi, majani na maji safi,” akaongeza.

Kwa wakati huu anapata maziwa lita nne kila siku kutoka kwa mbuzi watatu.

 

Bw Clement Ocharo akiwa nyumbani kwake Borabu – katika mpaka baina ya Kaunti za Nyamira na Bomet. Yeye ni mfugaji wa mbuzi wa maziwa. Picha/ Phyllis Musasia

Alisema kuwa ana maono ya kuogeza idadi ya mbuzi wake ili kuafikia soko la humu nchini ambapo watu wengi wameonekana kufurahishwa na aina ya kisasa ya mbuzi anaofuga.

“Sijuti kubadilisha mbuzi wa kawaida na mbuzi hawa ninaowafuga kwa sasa. Karibuni ninatarajia kuwafuga mbuzi idadi maradufu ya hawa walioko kwa sasa,” akasema wakati wa mahojiano.

Mtaalamu wa maswala ya kilimo cha mifugo katika Kaunti ya Nakuru Bw Joseph Amuyunzu anasema kuwa inakuwa rahisi kwa mkulima na mfugaji iwapo amepata mafunzo yanayohitajika.

“Changamoto huja wakati ambapo mkulima au mfugaji ni mgeni kwenye mswala haya, lakini pindi tu anapopata uzoefu, hali inakuwa rahisi,” akasema Bw Amuyunzu.

Anawahimiza wafugaji wengine ambao labda wanahisi kuwa wanapata changamoto kufuga mifugo kama vile ng’ombe, kuku wa mayai na nyama, wajaribu mbinu mbadala na wasisahau kujisajili kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu.

You can share this post!

KILIMO NA MAARIFA: Vyakula vinavyoweza kukuokoa dhidi ya...

Aomba talaka baada ya mume ‘aliyekwepa...

adminleo