Aomba talaka baada ya mume 'aliyekwepa majukumu' kutaka amegewe mahari ya binti yao
Na KATE WANDERI
MAHAKAMA ya Nakuru imeamua kwamba kesi ya talaka ya wanandoa itakilizwe baada ya juhudi za kuwataka waafikiane na kurejelea maisha yao kama mume na mke kugonga mwamba.
Hakimu, Yvonne Khatambi ameamua Alhamisi kesi baina ya Joel Lang ‘at, 72, na mkewe, Joyce Chemutai, 65, isikilizwe baada ya kushindikana wao kusuluhisha tofauti zao nje ya mahakama.
Wawili hao wanazozana kuhusu mahari ya binti yao.
Mlalamishi ambaye ni Bi Chemutai aliwasilisha kesi mahakamani akiomba talaka na mumewe ambaye wamekuwa wametengana kwa muda wa zaidi ya miaka 20.
Kupitia kwa wakili wake, mwanamke huyo ameieleza mahakama kwamba penzi lao lilikwishavurugika na hivyo ni muhimu kesi kusikilizwa na kuamuliwa.
Mahakama imeamua kesi itajwe kabla ya kusikilizwa ambapo itatoa nafasi kwa Bi Chemutai kumpa mumewe notisi ya kesi kwa sababu hakuwa mahakamani.
“Upande wa malalamishi umkabidhi mshtakiwa notisi na stakabadhi zingine muhimu za kesi kabla ya kesi kutajwa Agosti 27 ili kutoa mwelekeo wa kusikilizwa kwake,” mahakama imeamuru.
Bi Chemutai aliwasilisha kesi hiyo Oktober 2018 akilalamika kwamba mwanamume ambaye hakuwepo kumpa mwanawe wa kike matunzo, ametaka amegewe sehemu ya mahari.
Wanandoa hao walikuwa wamefanya ndoa yao rasmi Januari 31, 1992, kwa msajili wa ndoa, lakini wakatengana baadaye, kulingana na mlalamishi.
Kwao nyumbani ni Salgaa, Rongai, Kaunti ya Nakuru.
Mwanamume huyo naye alitaka Januari 2019 apewe muda zaidi kutatua suala hilo na mkewe.
Alidai, mke baada ya wao kukaa kila mmoja mbali na mwenzake, alikatiza mawasiliano muhimu na hivyo kumnyima fursa ya kuwashughulikia wanawe.