Michezo

Macho kwa Chager madereva 23 wakiwania taji la Kilifi Rally

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

DEREVA Baldev Chager atalenga kuendeleza ubabe wake Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) zitakapoingia duru ya nne Agosti 16, 2019.

Ingawa dereva Onkar Rai ameorodheshwa kuondoka jukwaani wa kwanza katika duru hii ya KCB Kilifi Rally, Chager, ambaye alinyakua mataji ya duru mbili zilizopita za KCB Kajiado Rally na Safari Rally, ndiye anapigiwa upatu mkubwa kutifulia wenzake vumbi.

Chager alikuwa amejawa na tabasamu katika mahojiano kabla ya Kilifi Rally. “Naingia duru ya Kilifi nikiwaheshimu wapinzani wangu, licha ya kuwa nilibeba mataji ya duru mbili zilizopita. Mimi na mwelekezi wangu (Ravi Soni) tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kufanya vyema,” alisema Chager, ambaye kwa kawaida huendesha gari la aina ya Mitsubishi Evolution 10.

Hata hivyo, Chager, ambaye ana nafasi kubwa ya kuongeza mwanya wa alama kati yake na mpinzani wake wa karibu Carl Tundo, alikiri kuwa magari ya Skoda Fabia R5s yatatoa ushindani mkali sana. Tundo hatakuwa Kilifi.

“Mimi na Tundo tulibahatika kumaliza Safari Rally mbele ya Manvir Baryan baada ya gari lake la Skoda kuvuta vumbi naye Onkar alipata ajali. Ukweli ni kuwa magari ya R5s yatakuwa bora kuliko Mitsubishi,” alisema.

Onkar alishinda duru ya ufunguzi mwezi Februari mjini Nakuru wakati Chager akimaliza wa tatu na hawezi kupuuzwa.

Atashirikiana na mwelekezi wake Gareth Dawe katika gari la aina ya VW Polo R5.

Onkar ataondoka jukwaani katika kampuni ya Mombasa Cement saa moja asubuhi Ijumaa. Chager ataanza katika nafasi ya pili akifuatiwa na Tejveer Rai akishirikiana na Gavin by Laurence katika gari la aina ya R4 Mitsubishi Evolution 10.

Bingwa mpya wa Bara Afrika, Manvir Baryan atakuwa wa nne kuanza mashindano akisaidiwa na mwelekezi wake kutoka Uingereza Drew Sturrock.

Baryan atakuwa akijaribu gari lake la Skoda Fabia R5. Bado Baryan anatafuta ushindi wake wa kwanza katika mashindano ya KNRC yanayojumuisha duru nane.

Dereva huyu, ambaye hakushiriki duru ya Nakuru, alipitwa na Chager katika sehemu ya mwisho ya Safari Rally wakati gari lake lilivuta vumbi katika eneo la Kedong. Pia, alishindwa na Chager kwa sekunde 36 katika duru ya Kajiado.

Duru ya Kilifi itaanza na mkondo maalum wa kilomita 21.31 Ijumaa usiku na kisha kuendelea na mikondo mingine minane Jumamosi.

Chager anaongoza msimu kwa alama 81 akifuatiwa na Tundo (71), Baryan (48), Tejveer (36) na Onkar (25) katika nafasi tano za kwanza.

Orodha ya washiriki:

Onkar Rai/Gareth Dawe (VW Polo R5)

Baldev Chager/Ravi Soni (Mitsubishi Evolution 10)

Tejveer Rai/Gavin Lawrence (Mitsubishi Evolution 10)

Manvir Baryan/Drew Sturrock (Skoda Fabia)

Jasmeet Chana/Ravi Chana (Mitsubishi Evolution 10)

Izhar Mirza/Kavit Dave (Mitsubishi Evolution)

Ammar Haq/Victor Okundi (Mitsubishi Evolution 10)

Sohanjeet Puee/Adnan Din (Subaru Impreza)

Paras Pandya/Falgun Bhojak (Mitsubishi Evolution 10)

Pietro Canobbio/TBA (Mitsubishi Evolution 10)

John Ng’ang’a/George Njoroge (Subaru Impreza)

Issa Amwari/Job Njiru (Mitsubishi Evolution 10)

Minesh Rathod/Sameer Yusuf (Mitsubishi Evolution 10)

Karan Patel/James Mwangi (Subaru Impreza)

Raaji Bharij/Rajay Sehmi (Porsche 911)

Hussein Malik/Linet Ayuko (Mitsubishi Evolution 10)

Adil Mirza/Guveer Pandhal (Mitsubishi Evolution 8)

Nashad Kara/Kailesh Chauhan (Subaru Impreza)

Evans Kavisi/Absolom Aswani (Subaru Impreza)

Daren Miranda/Wayne Fernandes (Subaru Impreza)

Geoff Mayes/Suzanne Zwager (Land Rover)

Amit Vaja/Willy Kibata (Subaru Impreza)

Arjun Patttni/Dinesh Varsani (Subaru Impreza)