Habari

Hamasisho la umuhimu wa noti mpya laendelea

August 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na FADHILI FREDRICK, FARHIYA HUSSEIN na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK), Dkt Patrick Njoroge, amewaonya Wakenya na wageni wanaotumia pesa za Kenya kwamba ifikapo Oktoba Mosi noti za zamani za Sh1000 zitakuwa hazina thamani yoyote.

Dkt Njoroge akizungumza Ijumaa katika kampeni ya kufahamisha wakazi wa Kwale umuhimu wa noti mpya amewarai wajitolee kurudisha katika benki noti hizo wabadilishiwe mapema.

“Wakenya wote wanashauriwa kurudisha noti hizo kwani hakuna makataa yatakayoongezwa ifikapo mwisho wa Septemba. Wajitahidi vilivyo,” amesema Njoroge.

Ameongeza ni kama kwamba Wakenya wengi hawajatilia maanani suala hilo na ndio bado wanaendelea kutumia noti nzee huku akiwaonya ifikapo mwanzo wa mwezi wa Oktoba zitakuwa hazina thamani yoyote.

“Ni muhimu warudishe kwa mapema na pia kuwaambia wenzao walioko mashinani,” akaongezea.

Aidha, Wakenya wameelezwa jinsi watakavyoweza kutambua noti mpya kuwa ni za halali.

Wameelezwa jinsi tatu ambazo watatumia kutathmini noti halali na ambazo ni kugusa, kutazama na kupindua noti.

“Mkenya yeyote – hata yule ambaye hajaenda shuleni – akifunzwa jinsi hizo tatu ataweza kutambua ni noti ipi halali. Kwanza, anaweza kugusa na ataweza kutathmini. Jinsi ya pili anawezapia kutazama kwa mwangaza ambapo ule michoro wa simba huwaka; na mwisho ni kupindua na ataona ikibadili rangi yake,” akaeleza Bw Njoroge.

Akiandamana pamoja na mkuu wa fedha Kaunti ya Kwale, Bw Bakari Sebe pamoja na maafisa wake, wamezuru kati ndogo ya Lunga Lunga.

Noti hizo mpya zilizinduliwa wakati wa sherehe za Madaraka kwa lengo la kupunguza visa vya pesa bandia nchini.

Utasaidia pia kueleza umuhimu wake kwa wale ambao wako kwenye vikundi vya vyama vidogovindogo na kupunguza idadi ya watu wanaoficha pesa bandia nyumbani.

Maafisa wa benki kuu wakiongozwa na mkuu wao watazuru kaunti zote kuhakikisha na kufahamisha wakenya wote pamoja na walioko mashinani umihumu wa kuregesha noti mzee na kuanza kutumia zile noti mpya.

Hata hivyo, zipo changamoto. Ni miezi miwili baada ya CBK kuzindua sarafu mpya nchini, visa vya noti bandia vinaendelea kushuhudiwa.

Mnamo Juni 1, 2019, Njoroge alitangaza kuanza kubadilishwa kwa noti za zamani za Sh1,000, Sh500, Sh200, Sh100 na Sh50.

Pia, sarafu (coins), kuanzia ile ya Sh20, Sh10, Sh5, hadi Sh1 hadi zimebadilishwa.

CBK ilitoa makataa ya hadi Septemba 30, 2019, ambapo noti za zamani za Sh1,000 hazitatumika tena, watu wakitakiwa kuzibadilisha katika benki mbalimbali kupata zile mpya.

Sarafu za Sh500, Sh200, Sh100 na Sh50 na zile za chuma zitatumika za kitambo pamoja na zile mpya.

Aidha, CBK inasema mabadiliko hayo yanaenda sambamba na matakwa ya katiba ya sasa, iliyozinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

Kwa mujibu wa kipengele cha 231, benki hiyo inapaswa kubadilisha sarafu zote za Kenya na kuondoa sura yoyote iliyopo ya kuzibinafsisha.

Kifungu cha nne cha kipengele hicho kinasema noti na sarafu zinazotolewa na CBK ziwe na picha zinazoonesha au kuashiria maliasili ya Kenya, na zisiwe na picha yoyote ya mtu binafsi.

Licha ya juhudi za Benki Kuu ya Kenya, raia wameanza kulalamikia kuwepo kwa noti bandia.

Noti bandia

Baadhi ya wafanyabiasha kaunti ya Nairobi na Kiambu, waliozungumza na Taifa Leo kwa njia ya kipekee wanasema ‘noti mpya bandia’ zimeingizwa ‘sokoni’.

“Mnamo Jumatano, Agosti 7 mwendo wa jioni mteja alinunua maboga na viazi katika kibanda changu kwa noti ya Sh1,000. Nilipompa salio alinieleza anunue bidhaa zingine kwenye duka nikimfungia alizonunua kwangu, nisijue ulikuwa mtego. Niligundua baadaye noti aliyonipa ilikuwa bandia,” akalalamika mama mfanyabiashara eneo la Zimmerman, Nairobi.

Katika mtaa huo pia mhudumu wa duka la M-Pesa alisema amenusurika mara kadhaa kupokezwa pesa bandia.

“Kuna mteja mmoja ninayemfahamu alinipa Sh2,500 nimuwekee baadaye. Noti moja ya Sh1,000 na noti ya Sh200, zilikuwa ghushi. Bahati niliyoangukia sikuwa nimemtumia,” akasimulia mhudumu huyo.

Anasema baada ya kumfahamisha kuhusu pesa zake bandia, alikoma kuenda katika duka lake la M-Pesa.

Kilio sawia na cha wananchi hao kinaradidiwa na kadhaa mtaa wa Githurai 45.

Mchuuzi wa matunda alisema amepokea noti bandia kutoka kwa wateja wawili hasa majira ya jioni.

“Matapeli wengi wanatumia nafasi ya giza kutanda kupunja watu,” akaelezea mfanyabiashara huyo.

Mmiliki mmoja wa duka la M-Pesa, Bw Antony Kabue ambaye pia hufanya biashara ya bidhaa za kula anasema ameepuka hadaa za aina hiyo kwa kununua mashine maalum inayotambua noti bandia.

“Inauzwa kwa bei nafuu, yangu niliinunua Sh3, 000 na imeniepusha kukabidhiwa sarafu bandia,” akasema Bw Kabue.

Jumanne, Agosti 6, 2019, mshukiwa mmoja katika Kaunti ya Narok alikamatwa na maafisa wa polisi baada ya njama yake kuhadaa mhudumu wa M-Pesa kwa noti bandia zenye thamani ya Sh30,000 kutibuka.

Visa vya noti mpya bandia vinaonekana kuongezeka ambapo mjini Eldoret watu wawili pia walitiwa nguvuni baada ya kupatikana na noti zenye thamani ya Sh150,000 milioni, lakini pesa bandia.

Dkt Patrick Njoroge, gavana wa CBK, anahimiza wananchi kuchukulia hatua kali matapeli kwa kushirikisha maafisa wa usalama.

Pia, anashauri haja ya kuripoti visa vya aina hiyo katika tawi la CBK lililoko karibu nao.