PAC yailaumu NCPB kwa kutoelezea jinsi Sh440m zilitumika katika ununuzi wa magunia
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wameilaumu Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kwa kutowajibikia matumizi ya Sh440.1 milioni zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa magunia ya kuhifadhi mahindi katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2017.
Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) Alhamisi ilielezwa kwamba bodi hiyo ilitumia jumla ya Sh841.6 milioni kwa ununuzi wa magunia lakini ni Sh401.5 milioni pekee ambazo matumizi yazo yaliwajibikiwa.
Katibu wa Wizara ya Kilimo Profesa Hamadi Boga aliyefika mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, alikabiliwa na wakati mgumu kueleza ni kwa nini wizara yake haikutoa maelezo kuhusu jinsi ambavyo Sh440,092,022 zilizosalia zilitumika.
Hii ni baada ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, kwenye ripoti yake ya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika NCPB mwaka huo, kusema bodi hiyo haikutoa stakabadhi kuhusu namna kiasi hicho cha fedha kilitumika.
“Tofauti ya Sh440 milioni inajitokeza. Hii ina maana kuwa NCPB haikutoa maelezo kuhusu namna pesa hizo zilitumika kwa shughuli iliyokusudiwa ya ununuzi wa magunia ya mahindi,” Bw Ouko akasema katika ripoti yake.
Lakini Profesa Boga aliwaambia wanachama wa kamati ya PAC kwamba hitalafu hiyo ilitokana na changamoto inayokabiliwa NCPB katika mfumo wa sasa wa “usimamizi na uhifadhi wa nafaka”.
“Hii ndio maana mwaka huu 2019, tumeamua kutekeleza mageuzi katika nyanja hii ili kupunguza gharama ya uhifadhi wa mahindi kwa kuimarisha mfumo mzima wa usimamizi wa nafaka katika NCPB,” akasema.
Profesa Boga pia alikabiliwa na wakati mgumu kuelezea tofauti katika bei ya magunia ya mahindi kwa waliopewa zabuni ya kuwasilisha magunia hayo.
Ilibainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliuza magunia hayo kwa Sh38.28 kila moja huku wengine wakiwasilisha bidhaa hiyo kwa NCPB kwa bei ya Sh28.08 kwa kila gunia.
Katibu huyo wa Wizara aliiambia kamati ya PAC kwamba kampuni za Rai Ply woods, Texplast Industries na Trans Global Distributors zilipewa zabuni ya kuwasilisha magunia 525,000 ya uzani wa kilo 50 ya aina ya Polypropylene, kwa gharama ya Sh15,4 milioni.
Tofauti
Profesa Boga alitakiwa kueleza ni kwa nini kampuni ya Rai Plywoods iliwasilisha magunia kwa bei ya Sh38.28 kila moja ilhali ile ya Trans Global Distriubutors iliwasilisha magunia yayo hayo kwa bei ya Sh28.08.
Kampuni ya Texplast Industries iliwasilisha shehena moja ya magunia kwa NCPB kwa bei ya Sh30,74 na nyingine kwa bei ya Sh28.08 kwa kila gunia.
“,Mbona kampuni ya Rai Plywood ilipewa zabuni ya kuiuzia NCPB magunia 45,000 kwa bei ya Sh38.28 huku kampuni ya Trans Global Distributors ikiuza magunia 20,000 kwa bei ya Sh28.07 kwa kila gunia.
“Huu ununuzi wa magunia ulifanywa na NCPB umegeuka kuwa sakata kubwa ambayo sharti tuchunguze kwa kina ili kubaini ukweli kuhusu namna watu fulani walikula njama ya kupora pesa za umma,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Busia katika Bunge la Kitaifa Bi Florence Mutua.
Hata hivyo, Profesa Boga aliiambia kamati hiyo kwamba majibu kamili na ya kuridhisha kuhusu suala hilo yanaweza tu kutolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NCPB Joseph Kimote, afisa wa ununuzi na meneja mkuu anayesimamia masuala ya fedha.
“Mengi ya maswali haya yanaweza kujibiwa kikamilifu na Mkurugenzi Mkuu wa NCPB, afisa wake wa idara ya ununuzi na meneja anayesimamia masuala ya fedha,” akasema.
Hapo ndipo mwenyekiti wa PAC Bw Wandayi aliamuru kwamba usimamizi wa NCPB ufike mbele yake wiki ijayo kutoa ufafanuzi kuhusu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Bw Ouko kuhusu ununuzi wa magunia ya kuhifadhi mahindi katika matawi kadha ya bodi hiyo humu nchini.