• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Kivumbi kinatarajiwa Kenya ikichagua wakimbiaji wa Riadha za Dunia wa mita 10,000

Kivumbi kinatarajiwa Kenya ikichagua wakimbiaji wa Riadha za Dunia wa mita 10,000

Na GEOFFREY ANENE

MFALME wa Riadha za kilomita 21 duniani mwaka 2014, 2016 na 2018 Geoffrey Kamworor na malkia wa Riadha za Dunia, Jumuiya ya Madola na Bara Afrika katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri ni baadhi ya wakimbiaji watakaotifua vumbi juma lijalo katika mashindano ya kitaifa uwanjani Nyayo jijini Nairobi.

Wakimbiaji hawa nyota watashiriki mbio za mita 10, 000 katika mashindano hayo ya kuunda timu itakayowakilisha Kenya katika Riadha za Dunia mnamo Septemba 27 hadi Oktoba 6 mwaka huu jijini Doha nchini Qatar.

Kamworor, 26, ambaye alimaliza Riadha za Dunia za mwaka 2017 katika nafasi ya sita katika mbio za mita 10, 000, atapigania tiketi dhidi ya bingwa wa dunia wa mbio za mita 10, 000 za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2018 Rhonex Kipruto pamoja na Stanley Waithaka aliyezoa medali ya fedha kwenye Riadha za Dunia za Under-20 nchini Finland katika mbio za mita 5,000 mwaka jana.

Mashindano haya kitaifa yataanza Agosti 20 na kutamatika Agosti 22. Katika mashindano haya, mbio za mita 10, 000 pekee ndizo zitakuwa na tiketi ya kuelekea Doha, huku mchujo wa vitengo vingine vyote ukiandaliwa Septemba 3 uwanjani humu.

Wakimbiaji kadhaa tayari wameshajikatia tiketi kuwa kwenye Riadha za Dunia wakiwemo Kipruto, Kamworor na Waithaka na kile wanahitaji ni kumaliza mashindano ya juma lijalo katika nafasi tatu za kwanza.

Kulingana na afisa mmoja mkuu katika Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Barnabas Korir, wakimbiaji watatu wa kwanza kukamilisha mbio watanyakua tiketi ya kuenda Doha mwisho wa mwezi ujao muradi tu wawe wametimiza muda unaohitajika. Korir alisema kuwa hata wanariadha wanaoelekea katika Riadha za Bara Afrika, wako huru kujaribu bahati yao kabla ya kuelekea mjini Rabat nchini Morocco.

“Sababu yetu ya kuamua kuwa na mchujo wa mbio za mita 10, 000 mapema ni kupatia wakimbiaji watakaokuwa wamenyakua tiketi muda wa kupata nafuu kwa wakati ufaao. Tarehe ya kufuzu ni Septemba 3 kwa hivyo kuchelewesha mchujo kutaathiri baadhi ya wakimbiaji ambao pengine wangemaliza katika nafasi tatu za kwanza,” alisema Korir.

Muda wa kufuzu katika mbio za mita 10, 000 za wanaume ni dakika 27:40.00. Ushindani, hasa katika kitengo cha wanaume, unatarajiwa kuwa mkali zaidi, huku chipukizi na wakimbiaji wazoefu wakiwania tiketi tatu za kuelekea Doha.

Kamworor, Kipruto and Waithaka watalazimika kujiandaa vyema ili kuwalemea wakimbiaji kama Charles Muneria, Wilfred Kimitei na Peter Emase kutoka Idara ya Magereza.

Alfred Barakach, Vedic Cheruiyot na Alex Oloitiptip kutoka Idara ya Jeshi, Josphat Kipchirchir, Cosmas Birech na Gilbert Kimunyan (Central Rift), Edwin Kosgei, Bernard Kibet na Albert Tonui (South Rift) ni baadhi ya wakimbiaji ambao pia hawawezi kupuuzwa.

Wakimbiaji 10 wanawaume tayari wana muda unaohitajika kuwa Doha, lakini tiketi zilizoko mezani ni tatu kwa hivyo lazima wazipiganie.

Obiri pamoja na bingwa wa zamani wa Mbio za Nyika Duniani Agnes Tirop na mshindi wa zamani wa Bara Afrika Alice Aprot ni baadhi ya majina makubwa yatakayotoana jasho katika mbio za wanawake za mita 10, 000.

Obiri ataongoza wanajeshi wenzake Irene Kamais na Monica Chirchir naye Tirop atakuwa mstari wa mbele kupeperusha bendera ya Idara ya Polisi akishirikiana na Stacy Ndiwa na Edith Chelimo.

Aprot na Monica Wanjiru watabeba matumaini ya Idara ya Magereza.

Wanariadha wengine wanaotarajiwa kupigania vilivyo tiketi ni Irene Cheptai, Brilliant Jepkorir na Nancy Jelagat (North Rift), na Sandra Chebet, Gladys Cherono na Everlyn Chirchir (South Rift).

Muda wa kufuzu kwa wakimbiaji wa kike katika mbio za mita 10,000 ni dakika 31:50.00. Obiri, Ndiwa na Wanjiru ni baadhi ya wakimbiaji saba wanawake tayari wametimiza muda huu, lakini lazima wajitahidi kumaliza katika nafasi tatu za kwanza.

You can share this post!

Starlets kujiandalia mchujo wa Olimpiki dhidi ya Ethiopia

DAU LA MAISHA: Sio muuguzi ila wengi wapona kupitia kwake

adminleo