• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
‘Ninachotaka tu ni familia yangu’

‘Ninachotaka tu ni familia yangu’

Na MARY WANGARI

[email protected]

MWANAMKE Mkenya asiye na makao nchini Uingereza ameacha wengi na masikitiko baada ya kusimulia masaibu yake huku akilia akitaka kuunganishwa na mama na kaka zake watatu.

Kupitia video iliyochapishwa katika ukurasa mmoja katika mtandao wa kijamii wa Facebook, na iliyoonekana na Taifa Leo, mwanamke huyo aliyejitambulisha kama Peggy, anasema alizaliwa Kenya na ni kifungua mimba miongoni mwa watoto wanne.

“Mimi ni kifungua mimba wa watoto wanne. Nina kaka watatu – Steven, George na Kevin – na mama asiye na mume aliyetutunza. Nilizaliwa Kenya, mamangu hufanya kazi kwa bidii sana. Amepitia mateso mengi maishani. Nilifahamu haya kupitia duru ambazo hata sitaki kuzijua. Si vyema lakini sasa niko hapa,” aliandika Peggy.

Peggy ambaye bila shaka anaonekana mwanamke mchangamfu na aliyeelimika, anasema ana binti mwenye umri wa miaka 11 kwa jina Peggy Junior.

Upendo wake kwa familia yake ulikuwa dhahiri jinsi uso wake ulivyochanua tabasamu na sauti yake kubadilika kwa bashasha alipopata fursa ya kuwatumia salamu.

“Hujambo mwanangu, Hi mami, Hi Steven, Hi George na Kevin. Ningali hali licha ya yote,” alisema huku akisita ghafla kwa huzuni.

Alisimulia jinsi mamake ambaye ni mfanyabiashara shupavu anayethamini elimu, alivyowaelimisha watoto wake katika shule za kimataifa.

“Mamangu ni mfanyabiashara. Sote tulienda shule. Tulielimishwa katika shule za kimataifa. Mimi nilienda Uingereza, Steven akaenda Amerika, Kevin alienda Manchester, alikuwa hapa nami naye George akaenda Malaysia.”

“Mamangu si mpumbavu, ni mfanyabiashara wa kimataifa. Alianzia chini kabisa, hakupatiwa chochote lakini alijitahidi sana. Kwake elimu ni kila kitu,” alisema.

Alisema kwamba familia yake ni kila kitu kwake na anachotamani tu ni kuunganishwa nao.

“Furaha yangu ya kwanza ni familia yangu. Sina baba, nina mama, kaka, na mtoto. Huo ndio ulimwengu wangu wote. Mandhari haijalishi, kinachojalisha ni uliye naye. Maisha yangu ni furaha yangu ya kwanza, mamangu na kaka zangu,” alisema kwa hisia.

Alikumbuka kwa masikitiko jinsi alivyowasili Uingereza kusomea shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Leicester, licha ya mamake kumkataza.

“Nilikuja kusomea shahada ya Uzamili katika Taaluma ya Mauzo Kimataifa, lakini kipindi kilikuwa kifupi sana. Niliporejea nyumbani mamangu alinisihi nisirejee lakini nikasisitiza kwenda. Sikuelewa wakati huo lakini kuna kitu hakikiwa sawa,” alisema.

Mamlaka kukataa kumsaidia

Alisimulia mashaka yake kama mtu asiye na makao Uingereza baada ya mamlaka kukataa kumsaidia, ambapo hata alinusurika kubakwa wakati mmoja wahuni.

“Walisema hawawezi kunisaidia kwa sababu mimi si kichaa, sina ulemavu, sina rekodi ya uhalifu, sina madeni. Niliwaambia mimi ni mwanamke, na mama, wakakataa,”

“Usiku mmoja nilivamiwa na kundi la wahuni. Walitaka kunibaka, walikuwa na sindano za kujidunga mihadarati. Mimi sifanyi hivyo,nilijawa na hofu. Haya ndiyo yanayoendelea mitaani. Huwa sitangamani na wahuni. Tutasemezana nini nao ikiwa hatuwezi kuwasiliana.

“Kwa nini unanilazimisha kutangamana na watu kama hao? Kwa nini unanitupa chini chooni? Siwezi kukubali haya. Mamangu ni mtu mwadilifu, Si sawa sisi wanawake kufanyiwa hivi na hatuwezi kusema lolote kwa kuwa hakuna mwanamme wakutuwakilisha.

Tuna watoto wetu binafsi, mbona unajaribu kutufanya wanyama, mimi ni binadamu si mnyama. Nimeenda shuleni, mama aliwekeza kwangu na haya ndiyo malipo aliyopata,” alilia kwa uchungu.

Kulingana na Peggy, anachotaka tu ni familia yake ili kusonga mbele na maisha yake.

“Nipatieni virago vyangu nitoweke. Mimi ni mama na dada. Ninachotaka tu ni binti yangu,mamangu na kaka zangu. Hao ndio uhai wangu.,” alisema Peggy huku akilia katika video iliyowaacha wengi wakijizuia kububujikwa na machozi.

You can share this post!

Ingwe kuchuana na Yanga kirafiki

Onkar Rai, wengine sita wajiondoa duru ya KCB Kilifi Rally

adminleo