• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kenya Lionesses yaruka Fiji katika viwango vya dunia

Kenya Lionesses yaruka Fiji katika viwango vya dunia

Na GEOFFREY ANENE

LIONESSES ya Kenya imeingia mduara wa 25-bora kwenye viwango bora vya dunia vya raga ya wanawake ya wachezaji 15 kila upande vilivyotangazwa Jumatatu.

Kenya imeruka Denmark, Fiji na Jamaica baada ya kuwa na ziara ya kufana kwenye mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mjini Johannesburg ilikolipua Madagascar 35-5 na Uganda 37-5 kabla ya kuzidiwa ujanja na wenyeji Afrika Kusini 39-0 katika fainali Agosti 17.

Lionesses ya kocha Felix Oloo, ambayo ilirejea nchini Jumapili jioni, inasalia ya pili barani Afrika nyuma ya Afrika Kusini ambayo haijasonga kutoka nafasi ya 11 duniani licha ya kuaibisha Uganda 89-5 na Madagascar 73-0 katika mechi zake zingine za mchujo wa Afrika ulioanza Agosti 9.

Warembo wa kocha Oloo, ambao sasa watalazimika kushinda mchujo wa dunia utakaoleta pamoja timu kutoka Amerika Kusini, Ulaya, Asia na Oceania mwaka 2020 ili kuingia Kombe la Dunia mwaka 2021 nchini New Zealand, wameimarisha alama zao kutoka 46.46 hadi 46.72 kwenye viwango hivyo vya mataifa 55.

Denmark, Fiji na Jamaica zimeteremka nafasi moja kila mmoja hadi nambari 25, 26 na 27, mtawalia.

Zambia inasalia ya tatu barani Afrika na 35 duniani. Inafuatiwa na Namibia (39 duniani) nazo Zimbabwe na Botswana zimenufaika na masaibu ya Madagascar kuruka juu nafasi moja hadi 41 na 42 duniani, mtawalia.

Madagascar imeshuka kutoka 41 hadi nambari 43. Sare ya 15-15, ambayo Uganda ililazimisha dhidi ya Madagascar katika mechi ya kutafuta nambari tatu mjini Johannesburg, ilitosha kuiweka salama katika nafasi ya 45 duniani.

Hakuna mabadiliko mengine kwenye jedwali hili, huku New Zealand, Uingereza, Ufaransa, Canada na Marekani zikishikilia nafasi tano za kwanza duniani.

You can share this post!

Odhiambo atia saini kandarasi ya miaka miwili KCB

Bwana harusi akata tamaa ya kuishi baada ya mlipuko kuwaua...

adminleo