Makala

John De' Mathew kuzikwa Jumamosi

August 21st, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa mwanamuziki wa mtindo wa Benga, John De’ Mathew wanatarajiwa kumiminika hadi nyumbani kwake kumzika Jumamosi katika kijiji cha Gathiruini kilichoko kaunti ndogo ya Gatanga.

Hii ni baada ya upasuaji wa mwili wake kutekelezwa Jumanne na ambapo ilibainika kuwa aliaga dunia baada ya kupata majeraha mabaya kichwani, kifuani na pia katika viungo vingine katika ajali ya barabarani Jumapili usiku.

Gari lake mwanamuziki huyu liligonga gari lingine mbele yake.

Kwa mujibu wa msemaji wa wanamuziki wanaoandaa mazishi hayo Peter Kigia, kamati zote nne ambazo zinahusika zimeafikiana kuwa azikwe Jumamosi.

Kamati hizo ni za waombolezaji wanaoukatana katika mikahawa ya Metrofill Thika, Blue Springs Kiambu, Gathiruini kwake nyumbani na Githingiri Thika alikokuwa na boma la bibi wake wa pili.

Aliaga dunia karibu na mji wa Thika baada ya gari alilokuwa akiendesha kugonga lori mwendo wa saa tatu na nusu usiku na akatangazwa mfu katika hospitali ya Thika Nursing muda mfupi baadaye, baada ya kuwasilishwa hapo na wasamaria wema.

Ni wazo la kujadilika kuwa De’ Mathew ndiye alikuwa mwanamuziki aliyefanikiwa zaidi kutoka jumuiya ya wenzake wa Mlima Kenya ikizingatiwa kuwa alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Dkt William Ruto na katika Kaunti ya Murang’a, hakuhitaji mwaliko rasmi ili kumuona Gavana Mwangi wa Iria.

Ni katika hali hiyo ambapo Rais Kenyatta, Ruto na Wa Iria waliongoza jamaa na marafiki kutuma salamu za pole kwa familia ya mwendazake.

Pia, Wa Iria tayari ametangaza kwamba Kaunti itamzika De’Mathew kama shujaa wa Kaunti ya Murang’a ambapo ni mzawa wa kaunti ndogo ya Gatanga.

Gatanga ni mji ambao umejipa sifa ya kuwa ngome ya vipawa tele hasa wasanii wa muziki.

Kabla ya kifo chake ambacho wengi wamekitaja kuwa cha ghafla na cha kushtusha, alikuwa ametunga na kuandika mamia ya nyimbo huku sokoni akiwa na awamu 50 za kanda zilizopakiwa kwa sauti na zingine zikiwa ni za video.

Wakati habari za kifo chake zilianza kusambaa mwendo wa saa nne usiku, umaarufu wake uliwezesha jumbe hizo kusambazwa kwa kasi kiasi kwamba kuna baadhi ya vituo vya redio – vinavyotangaza kwa lugha ya Gikuyu – ambavyo vilitenga vipindi vya kawaida ili kuwaongoza wenyeji wa Mlima Kenya kushiriki msiba.

De’ Mathew ambaye elimu yake ni ya kidato cha nne na ashawahi kuwa muuzaji wa mboga na viatu na alikuwa mwanamuziki ambaye alikuwa amejipa nembo ya ushujaa wa kipekee kiasi kwamba kwa wengi, alikuwa nabii wa kisiasa katika eneo hilo.

“Alikuwa mwanamuziki ambaye aligusia sana masuala ya kijamii, siasa na kusisitizia wenyeji wa Mlima Kenya umuhimu wa kubakia ndani ya umoja na maamuzi ya kufaa kesho ya watoto wao katika siku za usoni,” asema mwanamuziki John Wa Mumbe ambaye ndiye alimshika mkono De’ Mathew na kumwingiza katika taaluma ya muziki Desemba 1986.

Akiwa katika ndoa ya mitaala, De’Mathew ambaye ni wa nne katika familia ya watoto wanane alijulikana kwa nidhamu kuu ya kuchagua maneno ya kutumia ndani ya nyimbo zake na akaishia kuwa ambaye ufuasi wake haukuwa na ubaguzi kwa kuwa hata kwa makanisa ya Kikiristo eneo la Mlima Kenya, ngoma zake zilikuwa zinachezwa.

Hasa katika harusi, wimbo ‘Njata Yakwa’ yaani, Nyota yangu ulikuwa ukichezwa hata na mapasta, na ni wimbo ambao katika video yake, Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a bungeni Bi Sabina Chege ndiye huonekana akielekezewa mistari mikali ya kimapenzi.

Wakati huo, Bi Chege alikuwa mtangazaji katika kituo cha redio cha Kameme FM.

Kwa ufanisi wake katika sekta ya Kimuziki, De’ Mathew alikuwa akiorodheshwa kama mwanamuziki ghali zaidi eneo la Mlima Kenya ambapo katika hafla za burudani, alikuwa akitoza ada ya Sh100,000 na Sh200,000 kwa wateja wa kampuni katika shoo kwa umma, burudani yake ikiwa ni ya muda wa saa mbili tu.

Wengi kama Gachathi wa Thuo wanamuenzi De’ Mathew kama aliyewaunga mkono kwa hali na mali hadi wakawa maarufu.

“De’ Mathew hakuwa mchoyo na ukarimu wake unajiangazia kwa wengi wetu kutoka Gatanga na kwingineko. Aliwasaidia wengi kwa pesa na ushauri ili kuingiza maguu ndani ya taaluma ya muziki,” anasema Thuo.

Jina lake kamili likiwa ni John Mwangi Ng’ang’a, mwaka wa 2017 alikuwa amekiri kuwa “imani yangu kwanza ni kwa Mungu.

Pia alisema anatambua mchango mkubwa wa mamake mzazi katika maisha na hata na hata kuongeza anavyoionea fahari asili yake ya kuwa wa kabila la Kikuyu au Gikuyu.

Alikuwa akishinikiza serikali ya Kaunti ya Murang’a kuorodhesha muziki miongoni mwa “mimea ya faida” huku akiwa mstari wa mbele katika kukemea wenye tabia ya kutekeleza uhalifu na wenye maono potovu ya kisiasa katika jamii yake ya Agikuyu.

Mwaka wa 2013 alishtakiwa kwa madai ya kueneza chuki katika wimbo wake wa ‘Mwaka wa Hiti’ yaani Mwaka wa Fisi na ambapo katika wimbo huo, alikemea vikali kwa maneno ya mafumbo wote ambao walikuwa weakipinga ari ya rais Uhuru Kenyatta kutwaa uongozi wa nchi.

Kwa wakati huo, Uhuru alikuwa akishiriki kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu katika mahakama ya kimataifa (ICC) na ambapo De’ Mathew alifananisha wale waliokuwa wakitegea Uhuru ahukumiwe ndio wapate uongozi.

Wale walionekana katika wimbo huo wakielekezewa miale ya moto na De’ Mathew ni pamoja na Raila Odinga, Peter Kenneth na Martha Karua.

Aliwafananisha na jinsi fisi hufuata binadamu kwa kuwa “anamuona akining’iniza mikono yake na kwa fikira za fisi, mikono hiyo itaanguka aigeuze kuwa mlo.”

Hata hivyo, hakimu Ellena Nderitu alitupilia mbali mashtaka hayo na kuamua kuwa upande wa mashtaka haukudhihirisha kuwa usanii huo ulikuwa na ujumbe wa chuki.

Hadi kifo chake, alikuwa mwenyekiti wa ushirika wa wanamuziki nchini kwa jina Talented Musicians and Composers (Tamco) na ambapo alikuwa akilenga kuwajumuisha wanamuziki katika umoja wa akiba na mikopo kujijenga.

Alikuwa amejishindia usaidizi wa rais, Dkt Ruto na wa Iria pamoja na wanasiasa wengine wengi wa Mlima Kenya ambao walikuwa wamechangia kifedha ushirika huo.

Aliaga dunia wakati alikuwa katika harakati za kuzuru Kaunti zinazoorodheshwa kama ngome za Jubilee ndani ya Mlima Kenya na nje, akieneza ujumbe kwamba ni lazima “tuwajibikie deni letu la kisiasa.”

Deni hilo, akisema, lilikuwa kwa Dkt Ruto ambaye “alitufaa tukiwa katika dhiki ya 2013 na 2017.”

Alikuwa tayari amezuru Kaunti ya Embu na alikuwa katika mipango ya kuzuru Kaunti ya Nakuru Agosti 30 ya mwaka wiki mbili zijazo.

Alikuwa ameachilia ngoma ‘Twambe Turihe Thiiri’ (Kwanza Tulipe Deni) na ambapo katika video ya ngoma hiyo, anaonya kuwa “hata ikiwa tunamkaribisha ‘baba’; baba ikiwa na maana Raila Odinga, ndani ya boma, tuchunge tusiwe tumebeba mzinga ukiwa umejaa nyuki hadi ndani ya nyumba na cha mno, tusisahau kuwa tuko na deni la Ruto.”

Kwa ufupi, alikuwa kiungo na tegemeo ndani ya mrengo wa ‘Tangatanga’ na ambapo mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro katika salamu zake za pole alisema kuwa “tumepoteza kiungo thabiti; mtu wa kujituma katika maono yetu ya ufaafu wa Dkt Ruto kama Rais wetu wa mwaka 2022.”