MAPISHI: Jinsi ya kuandaa kebab
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa kupika: Dakika 20
Walaji: 4
Vinavyohitajika
- Minofu ya kuku; kiasi cha nusu kilo
- Kitunguu maji 1, kata vipande vidogo
- Giligilani ya unga kijiko ½
- Pilipili manga kijiko ¼
- Garam masala kijiko 1
- Juisi ya limau kijiko 1
- Tangawizi kijiko 1
- Kitunguu saumu kijiko 1
- Yai 1
- Mafuta ya kupikia
- Chumvi kijiko 1
Maelekezo
Safisha nyama ya kuku kisha kausha maji yaishe. Kama nyama haina mafuta, unaweza kuongeza kijiko kimoja cha mafuta ya kupikia kwenye nyama.
Menya kitunguu na kisha saga kwenye blenda. Toa kitunguu, chuja maji yote kisha rudisha kwenye blenda. Ongeza pilipili, majani ya giligiliani, chumvi, tangawizi, kitunguu saumu, bizari, na limau na kisha giligilani.
Saga mchanganyiko hadi uchanganyikane vizuri ila hakikisha unabaki na minofu ya kuku kwa umbali.
Weka mchanganyiko kwenye bakuli safi. Pasua yai, mimina kidogo kidogo kwenye bakuli lenye mchanganyiko wa nyama huku ukikoroga.
Mchanganyiko ukianza kuwa mwepesi, acha kuweka yai.
Funika bakuli, weka kwenye jokofu kwa muda wa saa mbili na mchanganyiko ushikane ili iwe rahisi kutengeneza umbo unalotaka.
Ukiwa tayari kupika, tengeneza maumbo yanayokupendeza. Hakikisha una maji pembeni. Nawa mikono, chovya kwenye maji kiasi na kisha tengeneza umbo unalohitaji.
Weka kikaangio mekoni. Paka mafuta kwenye kikaangio. Yakishachemka vizuri, panga kebab na pika kwa dakika 10 au zaidi.
Pika huku ukigeuza kila upande kuhakikisha zinaiva na kupata rangi ya kahawia.
Pakua upendavyo na ufurahie.