UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tofauti za utunzi wa kazi za fasihi kati ya waandishi wa sasa na kale
Na WANDERI KAMAU
KWA muda sasa, nimepata nafasi ya kutagusana na kazi za waandishi mbalimbali kupitia sehemu ya ‘Mapitio ya Tungo’ kwenye Jarida la ‘Lugha na Elimu’ ambalo huchapishwa na gazeti la Taifa Leo kila Jumatano.
Ni kitengo cha kipekee ambacho kimenisafirisha na kunizamisha vilivyo kwenye uwanda wa fasihi, hasa kazi za kubuni ambazo zimeandikwa na waandishi wa zamani na wa kisasa.
Ingawa hili halimaanishi kwamba sikuwa nikisoma kazi hizo kabla ya kuanzishwa kwa ukumbi huo, ila upekee wake ni kuwa huwa unatuwezesha kuzitalii kwa undani zaidi kuliko asomavyo msomaji wa kawaida.
Ni sawa na muuzaji awekavyo bidhaa zake kwenye mizani. Kwenye ukumbi huo (na mwenzangu Enock Nyariki) huwa tunaangazia kazi yoyote ile; iwe riwaya, tamthilia, diwani ya hadithi fupi, mashairi na wasifu.
Hadi sasa, kile nimejifunza ni kuwa kuna tofauti kubwa katika kazi za kubuni za waandishi wa zamani na wale wa kizazi cha sasa.
Nyingi za tofauti hizo zimejikita katika masuala manne makuu, yakiwemo: (a) kiwango cha utunzi (b) mwegemeo wa kifalsafa (c) matumizi ya lugha na (d) maudhui.
Kiwango cha utunzi
Katika kiwango cha utunzi, kazi za waandishi wa zamani zimejitokeza kuwa za hali ya juu. Mtiririko wa vitushi ni wa aina yake, huku ukiwa umepangwa na upekee wa aina yake. Kwa mfano, kwenye riwaya ‘Duniani Kuna Watu’ iliyoandikwa na marehemu Mohamed S. Abdulah, msomaji anaweza kufuata kwa urahisi mtiririko wa vitushi, unaomwandama kijana Karimu.
Mwandishi anamkuza kutoka utotoni hadi ukubwani kwa kurasa chache.
‘Ulezi’ huo unamwezesha msomaji kuwa na upana mkubwa wa kimawazo, kuelewa undani wa mazingira ya mwandishi pamoja na utamaduni wake.
Ulezi huu wa wahusika pia unaandamana na ukuzaji mzuri wa kimazingira, ambao pia unampa msomaji uelewa mpana wa mwandishi pamoja na hali zinazompa msukumo wa kindani kutunga kazi zake. Kiwango hiki cha utunzi pia kinajitokeza kwenye kazi nyingine aula kama ‘Kisima cha Giningi’, ‘Dunia Mti Mkavu’ kati ya kazi nyingine.
Kwa mtazamo wangu, upekee huu wa utunzi unakosekana sana katika vitabu vingi vya waandishi wa kisasa, hasa walioanza kuandika kazi zao mwanzoni mwa mwaka 2000.
Mwegemeo wa kifalsafa
Tofauti ya pili inayodhihirika ni mwegemeo wa kifalsafa. Tofauti na waandishi wengi wa kizamani, waandishi wengi wa kisasa hawana zingatio lolote la kifalsafa ambalo linawapa msukumo wa kuandika kazi zao.
Kwa mfano, Shaaban Robert anajitokeza kuwa mzingatiaji wa falfasa ya kimaadili kwenye kazi zake kama ‘Kusadikika’, ‘Wasifu wa Siti Binti Saad’ kati ya nyinginezo.
Mfano halisi wa mwegemeo huu ni mjengeko wa kitabia anaompa Siti, kwani anamchora kama mzingatiaji mkubwa wa maadili. Shaaban amefaulu sana katika kuwajenga wahusika wake wakuu kwa kutumia falsafa ya kimaadili. Maadili ndiyo maudhui makuu katika kitabu ‘Adili na Nduguze.’
Msingi huu ulimpa Robert msingi mzuri wa kuangazia nyanja mbalimbali ambazo alikuwa akizijenga katika uandishi wake. Msingi kama huu unadhihirika kwenye kazi za mwandishi William Shakespeare, ila mwegemeo wake mkuu umekuwa ni katika falsafa ya vita, ubaguzi na mafarakano.
Matumizi ya lugha
Jambo la tatu ni matumizi ya lugha.
Hapa, waandishi wengi wa kisasa wanaonekana kuwapiku watangulizi wao, ikizingatiwa kwamba Kiswahili kilikuwa kingali kichanga katika miaka ya 1950, 1960 na 1970 wakati kazi nyingi za kifasihi zilizoandikwa na Waafrika (hasa nchini Tanzania) zilipoanza kutokea.
Wakati huo, hakukuwa na mwongozo maalum kuhusu matumizi ya baadhi ya maneno; mwandishi alikuwa huru kutumia neno lolote aliloliona linafaa.
Kutokana na pengo hilo, kazi nyingi ziliathirika sana, hasa kutokana na mwingiliano wa Kiswahili halisi na athari za baadhi ya lahaja. Kinyume na hayo, hali ni tofauti sasa kwani kuna asasi maalumu kama CHAKITA (Chama cha Kiswahili cha Kitaifa), BAKITA (Baraza la Kiswahili la Kitaifa) kati ya nyingine ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa kwenye kanuni zitakazozingatiwa katika matumizi ya baadhi ya maneno.
Maudhui
Mwisho ni uangaziaji maudhui. Kinyume na zamani, waandishi wa sasa wana nafasi pana ya kuangazi maudhui anuwai, kutokana na mabadiliko kwenye mikondo ya maisha ya jamii.
Kwa mfano, vile mwandishi wa kizamani angeangazia nafasi ya mwanamke katika jamii ni tofauti na sasa, ambapo jamii nyingi zimeanza kutambua umuhimu wa kumshirikisha mwanamke katika mambo mbalimbali yanayoiathiri kila siku.
Kazi nyingi za kizamani ziliwasawiri wanawake kama viumbe duni, ambao hawakuwa na nafasi yoyote ya kufanya maamuzi muhimu yanayohusu maisha yao. Hata hivyo, kazi nyingi za kisasa ni ‘pinduzi.’
Mfano halisi wa hili ni riwaya ‘Kula kwa Mheshimiwa’ yake Juma Namlola, ambayo inamsawiri mwanamke kama mwanamapinduzi wa kimfumo katika jamii.
Bila shaka, hili ni dhihirisho kwamba bado kuna mengi ambayo tutashuhudia katika fasihi, kadri mfumo wa kimaisha unavyoendelea kubadilika katika jamii.