Michezo

MAJOGOO EPL HATARINI: Huenda timu kubwa zilizozoea kumaliza sita bora zikajikuta matatani

August 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

SIKU chache tu baada ya msimu wa ligi kuu ya Uingereza (EPL) kuanza, kuna madai kwamba huenda timu kubwa zilizozoea kumaliza katika nafasi ya sita bora zikajikuta matatani.

Kuna wale wanaozitupia macho timu za Leicester City, Wolves, na Everton ambazo zinanolewa na Brendan Rodgers, Nuno Espirito Santo na Marco Silva mtawaliwa.

Klabu sita kubwa zinazomaliza juu kwenye misimu ya soka, zikibadilishana namba mara kwa mara ni Manchester City, Liverpool, Chelsea, Tottenham Hotspur, Manchester United na Arsenal.

Timu hizo zimeshikilia nafasi hizo za juu kwa misimu mitatu mfululizo, lakini baadhi yao zina matatizo kwa sasa.

Kwa mfano, Chelsea ambayo imemuuza nyota wao Eden Hazard imezuiliwa kusajili wachezaji wapya, na huenda hilo likawatatiza kwa kiasi kikubwa hasa baada ya kuanza msimu vibaya.

Vijana hao chini ya kocha mpya, Frank Lampard walianza kwa kuchapwa 4-0 na Manchester United kabla ya kuagana 1-1 na Leicester City mwishoni mwa wiki.

Manchester City nao pia walimalizishwa sare ya 2-2 na Tottenham Hotspur katika mechi ambayo walicheza kwa kuchanganyikiwa.

Leicester wanapewa nafasi kutokana na walivyocheza mechi zao za marudiano msimu uliopita na kumaliza katika nafasi ya sita.

Huenda timu hii ikafanya maajabu kama ilivyofanya miaka minne iliyopita chini ya kocha Claudio Ranieri kwa kutwaa ubingwa wa EPL.

Ni kikosi kinachoelewana vyema, mbali na kuwa na wachezaji wengi walio na umri wa miaka 26 au chini ya umri huo.

Katika mechi 10 za mwisho, chini ya Rodgers, Leicester City walivuma pointi nyingi na kuwa na tofauti nzuri ya mabao.

Kwingineko, baada ya Wolves msimu uliopita kumaliza katika nafasi ya saba, kuna kila uwezo wa vijana hao kumaliza katika nafasi nzuri zaidi.

Msimu uliopita, Wolves walicheza vizuri zaidi dhidi ya timu kubwa zilizokuwa mbele yao, lakini ikalemewa na timu ndogo.

Kujipanga

Hata hivyo, itabidi wajipange vyema baada ya kufuzu kwa michuano ya Europa League ambayo huchosha wachezaji ambao hawajazoea michuano hiyo.

Everton walimaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita, lakini itakumbukwa walikuwa wakali sana katika mechi za mwisho waliposhangaza kwa kuwachapa Chelsea, Arsenal na hata Manchester United.

Klabu hii ya goodison Road imeondokewa na nyota wawili muhimu, Kurt Zouma aliyerejea Chelsea, Idrissa Gueye aliyejiunga na Paris St-Germain (PSG), lakini nafasi zao zimejazwa vyema.

Kwa klabu kubwa, huenda Arsenal ikacheza vizuri kuliko msimu uliopita baada ya kuwanasa Nicolas Pepe, William Saliba, David Luiz na Dani Ceballos.

Manchester United walianza kwa kishindo kwa kuwacharaza Chelsea 4-0, lakini bado wana kazi kubwa kwani hivyo ndivyo walivyoanza msimu uliopita.

Spurs walikuwa na mioto msimu uliopita, lakini wameonekana kuchoka sana msimu huu wa 2019/2010.