Ukumbusho wa umma wa kifo cha Mzee Kenyatta wafikia kikomo
Na IBRAHIM ORUKO na PSCU
RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza kufutiliwa mbali kwa ukumbusho wa umma wa kifo cha Hayati Mzee Jomo Kenyatta baada ya miaka 41.
Ni uamuzi aliosema familia ilifikia baada ya kushauriana.
Hii ina maana kwamba familia ya Mzee Kenyatta itakuwa ikiadhimisha siku hiyo faraghani.
Desturi kwa zaidi ya miaka 40 imekuwa ni kwamba kunaandaliwa misa katika Kanisa Katoliki la Holy Family Basilica, Nairobi na kuishia kuweka shada ya maua katika sehemu maalumu iliyotengwa katika majengo ya bunge yenye sanamu ya Rais wa kwanza wa Kenya huru.
“Hii ndiyo mara ya mwisho tunaadhimisha siku hii pamoja na umma wote,” amesema Rais Kenyatta.
Ukumbusho huo umekuwepo tangu kifo cha Mzee kitokee mwaka 1978.
Rais Kenyatta hata hivyo amesema Rais wa Pili wa Kenya Daniel arap Moi alizingatia sana kiasi kwamba kwa miaka 24 mamlakani, mara 21 alihakikisha kunaandaliwa misa kanisani.
Rais wa Tatu wa Kenya, Mstaafu Mwai Kibaki naye vilevile aliizingatia kwa muda wa miaka 10 akiwa uongozini naye Rais Kenyatta mwenyewe amefanya hivyo kwa kipindi cha miaka saba.
Kiongozi wa nchi ameshukuru kanisa la Holy Family Basilica – ambalo liko karibu na eneo alikozikwa Mzee Kenyatta – kwa kuiruhusu familia na umma kuandaa ibada kila mwaka wa ukumbusho wa kifo chake.
Rais ambaye alikuwa ameandamana na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta, aliyekuwa Mama wa Taifa Ngina Kenyatta na jamaa wa familia ya Kenyatta aliungana pamoja na Naibu Rais Dkt William Ruto katika misa hiyo ya ukumbusho.
Aidha, amewataka washiriki wa misa hiyo ya Alhamisi na Wakenya kwa jumla kuzingatia mazuri aliyotaka Hayati Kenyatta.