Michezo

'Sensa kuwanyima wapenzi wa kabumbu mechi ya Arsenal dhidi ya Liverpool'

August 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na GEOFFREY ANENE na MWANGI MUIRURI

TANGAZO la Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuwa baa zitafungwa Agosti 24 na Agosti 25 kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi halijapokelewa vyema na mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sensa itafanyika kutoka Agosti 24-31, 2019. Kinachozungumziwa sana kote nchini wakati huu ni shughuli hii inayofanyika kila baada ya miaka 10.

Zisalia siku chache zoezi hilo lianze, mijadala imechacha, na mashabiki wa EPL hawajaachwa nyuma.

Mmoja wa waandishi wa makala hii alitumia garimoshi linalohudumu barabara ya Ruiru hadi jijini Nairobi kufika kazini Alhamisi na wengi wa mashabiki wa ligi hiyo walisikika wakilalamika.

“Mechi kati ya Arsenal na Liverpool ni mojawapo ya mechi kubwa katika kalenda ya soka ya Uingereza, ambayo tunaienzi. Sijui mbona Waziri aliamua kuweka kafyu hiyo akifahamu vyema mashabiki wengi kama sisi hutegemea kuona mpira kwenye sehemu za burudani kama baa. Tunapenda kuona mechi za EPL pamoja katika maeneo haya,” walisikika wakisema, huku baadhi yao wakitoa sababu nyingi tu za kuchekesha.

“Serikali haijui kuwa katika mabaa ingepata watu wengi zaidi na hata ingepata habari muhimu zaidi kutoka kwa waliolewa. Kwa mfano, habari ambazo mlevi ameficha kuhusu idadi ya mabibi wa pembeni anao na hata watoto waliozaa nje ya ndoa,” mmoja alisema.

“Hiyo kafyu haitafua dafu nikiwa katika shughuli ya chumbani. Shughuli hiyo ni muhimu kuliko shughuli zote na siwezi kuikatiza,” mwingine aliongeza.

“Kuwepo kafyu ama la, mimi lazima nitafute mahali pa kuona mechi za EPL za siku hiyo. Siwezi kukosa kutazama timu yangu ya Arsenal ikicheza,” alisema bwana mmoja ambaye alidokeza huenda kuna maeneo ya burudani yatakayokiuka kafyu hiyo kupeperusha mechi hizo.

Ripoti moja ya idadi ya baa jijini Nairobi ya mwaka 2016 ilidai kuwa kuna maeneo 12,500 ya burudani jijini humu.

Idadi kubwa ya mabaa hayo yalisemekana kuhudumu kinyume cha sheria ndiposa Kaunti ya Nairobi imekuwa ikitafuta njia ya kuyapunguza hadi 3,000.

Mechi tisa za EPL zitasakatwa katika siku hizo mbili ambapo si mashabiki wa Arsenal pekee wataathirika.

Manchester United, ambao pia inashabikiwa na Wakenya wengi, itavaana na Crystal Palace saa kumi na moja jioni Agosti 24.

Mashabiki wa Manchester City watakuwa wameona nusu ya kwanza dhidi ya Bournemouth zoezi hilo litakapoanza, nayo mechi inayokutanisha Liverpool na Arsenal uwanjani Anfield itaang’oa nanga saa moja na nusu usiku siku hiyo ya kwanza ya kuhesabiwa.

Sensa hukusanya data ambayo inatumiwa na serikali kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo. Sensa ya mwaka 2009 ilibainisha kuwa Kenya ina watu 38.6 milioni. Idadi hii inaaminika imefika 45 milioni. Kupitia sensa, idadi kamili ya watu wote nchini Kenya itajulikana. 

Kwa kawaida mashabiki wa timu ya Arsenal nchini Kenya hujulikana kwa msimamo wao ngangari.

Mwenyekiti wa mashabiki hao katika Kaunti ya Murang’a Bw James Nduati anawataka wenzake waendelee kuonyesha mapenzi kwa timu hiyo yao.

Nduati ambaye huongoza ushirikisho wa zaidi ya mashabiki 1,200 akizungumza na Taifa Leo kabla msimu mpya kuanza alisema, “Hatubanduki kutoka ufuasi wa timu hii yenye ufuasi mkubwa Kenya hii na Afrika kuliko nyingine yoyote.”

Alisema zuri lao ni kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani.

Mwenyekiti wa mashabiki wa Arsenal katika Kaunti ya Murang’a Bw James Nduati. Picha/ Mwangi Muiruri

“Sisi mashabiki wa Arsenal tunaelewa kuwa tunaweza katika kila mechi ama tukashindwa, tushinde au tutoke sare,” anasema Bw Nduati.

Alisema kuwa ligi hiyo ikiwa na timu 20 na kila moja ya hizo zote ikilenga ushindani wa kupata ushindi, Arsenal ikipata leo, ipoteze kesho na tena ipoteze ikitarajia kupata sio hali isiyo ya kawaida.

Akasema: “Mpira ukidunda na ukukatae, hata ufanye nini huwezi ukajinusuru. La muhimu ni kukubali. Huo ndio ujumbe wangu mkuu kwa leo.”

Anasema fahari yao kuu ni kumaliza juu ya wapinzani wa jadi Manchester United katika jedwali.

“Hata wakati mambo yamekuwa mabaya zaidi katika ulingo wa EPL bora tu Man United iwe nyuma yetu, hata tushushwe daraja tukiwa nambari 19 na Man United iwe nambari 20 katika jedwali, sisi tuko sawa,” akasema.