Michezo

Balozi wa Amerika nchini Kenya awakosha mashabiki wa michuano ya Super 8

August 23rd, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHABIKI wa soka katika Kaunti ya Nairobi wamefurahia baada ya Balozi wa Amerika hapa nchini Kyle McCarter kuwatembelea wakati wa pambano la Super 8 Premier League kati ya wenyeji Kawangware United na Jericho All Stars.

Katika mechi hiyo iliyochezewa Riruta Stadium, Jericho waliibuka na ushindi wa 3-0 mbele ya mashabiki wengi waliofurika uwanjani humo.

Mwanasoka Kevin Ndungu (kushoto) wa Jericho All Stars akabiliana na mchezaji wa Kawangware United wakati wa pambano la Super 8 Premier League katika uwanja wa michezo wa Riruta ambapo Jericho walishinda 3-0. Picha/ John Ashihundu

McCarter ambaye alikuwa mgeni wa heshima alitoa zawadi za mipira kwa timu husika huku akiahidi misaada zaidi kutoka kwa Ubalozi huo.

“Nimefurahia kuona vijana wakishindana kupitia michezoni, wakati huu dunia nzina inapiga vita uhalifu miongoni mwa vijana. Nawapongeza Extreme Sports kwa juhudi zao za kuhakikisha vijana wanatunzwa kupitia kwa kandanda ili wawe viongozi wema siku za usoni,” alisema McCarter.

“Nimeridhika na kiwango cha vijana waliopepetana hapa leo (juzi) na nina hakika baadhi yao watajipata katika timu ya taifa siku zijazo,” aliongeza.

Kwa niaba ya Extreme Spaorts, Afisa Mkuu wa kampuni hiyo Hussein Mohammed alisema anafurahia ari ya taifa la Amerika kusaidia vijana kupalilia vipaji vyao kupitia michezoni.

Mbali na matokeo ya mechi hiyo ya Riruta. Matokeo yote kwa ufupi yalikuwa MASA 2 TUK 3; Guthurai All Stars 3 Shauri Moyo Sportiff 2; Lebanon 0 Meltah Kabiria 2, Team Umeme 1 Rongai All Stars 0, Dagoretti Former Players FC 1 Mathare Flames 0, Metro Sports 0 Mathare Flames 0.

Mechi ya Super 8 Premier League kati ya NYSA na Huruma Kona. NYSA walishinda 3-0. Picha/ John Ashihundu