Michezo

Ulinzi Stars yakamilisha michezo ya majeshi kwa kulima Rwanda

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WAWAKILISHI wa Kenya katika soka ya mashindano ya Muungano wa Afrika Mashariki (EAC) ya majeshi, Ulinzi Stars walikamilisha kampeni kwa kuchapa Rwanda 1-0 uwanjani Kasarani mnamo Agosti 23, 2019.

Bao tamu la Oscar Wamalwa kutoka nje ya kisanduku lilitosha kupatia Ulinzi ushindi huo uliohakikisha inajiondolea aibu ya kupoteza taji ambapo sasa imemaliza katika nafasi ya pili.

Rwanda ilipokonya Kenya taji kwa kuzoa alama tisa katika mashindano ya mzunguko ya soka yaliyokutanisha mataifa matano. Kenya na Uganda zilimaliza soka kwa alama saba kila mmoja, ingawa wenyeji walifunga mabao mengi.

Tanzania ilikamIlisha ziara yake katika nafasi ya nne kwa alama sita nayo Burundi ikavuta mkia bila alama.

Kenya ilikamilisha mpira wa vikapu katika nafasi ya tatu nyuma ya washindi Rwanda na nambari mbili Uganda.

Wenyeji waliridhika katika nafasi ya pili kwenye mpira wa pete nyuma ya Uganda nayo Tanzania ikafunga mduara 3-bora katika fani hii.

Uganda, Rwanda na Kenya zilikamilisha voliboli katika nafasi tatu za kwanza mtawalia.

Wakenya walijiliwaza na mataji ya mbio za nyika walizotawala katika vitengo vyote vya wanaume na wanawake.

Matokeo ya soka ya michezo ya majeshi (EAC)

Agosti 13

Kenya 4-0 Burundi

Agosti 14

Uganda 0-1 Rwanda

Agosti 15

Tanzania 7-3 Burundi

Agosti 16

Kenya 0-0 Uganda

Agosti 17

Rwanda 3-0 Burundi

Agosti 19

Tanzania 2-1 Kenya

Agosti 20

Burundi 0-3 Uganda

Rwanda 3-1 Tanzania

Agosti 22

Uganda 2-0 Tanzania

Agosti 23

Rwanda 0-1 Kenya