Habari

SENSA MWAKA 2019: Naibu Rais, viongozi kadhaa tayari wamehesabiwa

August 24th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MUDA wa saa kadha baada ya shughuli ya kitaifa ya kuhesabu watu, maarufu sensa kuanza rasmi Jumamosi saa kumi na mbili jioni, Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ni miongoni mwa viongozi wakuu nchini ambao tayari wamehesabiwa.

Wengine ni Rais Mstaafu Daniel arap Moi na Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Mutahi Kahiga (Nyeri), Anne Waiguru (Kirinyaga), Martin Wambora (Embu) na James Ongwae (Kisii).

Rais Mstaafu Daniel Arap Moi (kushoto), Seneta wa Baringo Gideon Moi (kati) na mjumuishaji wa data za sensa Bw Paul Tuitoek katika makazi ya kiongozi wa zamani wa nchi yaliyoko Kabarak, Kaunti ya Nakuru mnamo Agosti 24, 2019. Picha/ John Njoroge

Gavana Oparanya ambaye ni mwenyekiti wa baraza la magavana (CoG) amehesabiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Emabole, eneobunge la Butere, Kaunti ya Kakamega.

Dkt Ruto amehasabiwa akiwa katika makazi yake rasmi ya mtaani Karen pamoja na familia yake ambapo picha iliyotumwa kwa vyombo vya habari inaonyesha Mkurugenzi wa Ubora na Mbinu wa Shirika la Ukadiriaji Ubora, Bi Mary Wanyonyi akiongoza shughuli hiyo katika familia ya kiunguzi huyu.

Bw Odinga naye amehesabiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Karen akiwa pamoja na familia yake vilevile.

Naye Mzee Moi amehesabiwa nyumbani kwake Kabarak katika eneobunge la Rongai, Kaunti ya Nakuru; shughuli iliyoongozwa na Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Erustus Mbui. Hapo amekuwepo mjumuishaji wa data za sensa Bw Paul Tuitoek.

Kufikia saa moja na dakaki 45 usiku Jumamosi, hakuna visa vyovyote vya utovu wa usalama vilikuwa vimeripotiwa.

Hata hivyo, kumekuwepo na madai kuwa baadhi ya raia jijini Nairobi na mji wa Kilgoris, Kaunti ya Narok walikuwa wamejifugia ndani ya baa na vilabu vya burudani wakibugia pombe na kutazama mechi za kandanda ya timu za Ligi Kuu ya Uingereza.

Zaidi ya maafisaa 200 wa polisi walikuwa wakizunguka mjini Kiligoris kuwafurusha wananchi kutoka baa kadhaa.

Na katikati mwa jiji la Nairobi, wachuuzi walikuwa wangali wakiendesha biashara zao, taswira ambayo ilishuhudiwa pia katika mji wa Kisumu.

Rais Uhuru Kenyatta ametarajiwa kuhesabiwa saa nne na nusu za usiku katika Ikulu ya Nairobi.