• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Chapa Dimba Season 3 yatazamiwa kuzua msisimko mkali

Chapa Dimba Season 3 yatazamiwa kuzua msisimko mkali

Na JOHN KIMWERE

MICHUANO ya kuwania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Three imepangwa kuanza mwezi ujao kote nchini. Kipute cha msimu huu kinatazamiwa kushuhudia ushindani mkali kinyume na ilivyokuwa muhula uliyopita.

Mashindano hayo ambayo hushirikishi wachezaji chipukizi wavulana na wasichana kwa wasiozidi umri wa miaka 20 huandaliwa na kufadhiliwa na kampuni ya Safaricom.

Ngarambe ya msimu huu inatazamiwa kuvutia zaidi ya timu 3000 kutoka mikoa nane kote nchini ambapo mabingwa wa kitaifa (wavulana na wasichana) kila moja itatia kibindoni kitita cha Sh 1 milioni.

Kando na tuzo za kitaifa mabingwa wa kila Mkoa hupokea zawadi ya Sh 200,000 huku mshindi wa pili akituzwa Sh100,000 bila kusahau zawadi za kibinafsi kwa wachezaji wale hufana kwenye mashindano hayo.

Kama ilivyokuwa kweney mashindano yaliyopita muhula huu Safaricom ikishirikiana na Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) pia itaandaa semina kuhusu mchezo huo kwa makocha wa timu zote zitakazoshiriki kipute hicho.

Kitale Queens waliotwaa ubingwa wa Chapa Dimba muhula uliopita. Picha/ John Kimwere

”Chapa Dimba ni mradi wa kukuza talanta za wachezaji chipukizi mashinani ambapo hatuna shaka kuishukuru Safaricom kwa kujitolea kudhamini makala mengine.

“Sina hofu kutaja kuwa tutaendelea kuinga mkono inakozidi kukuza vipaji vya wachezaji wazuri mashinani,” rais wa FKF, Nick Mwendwa alisema kwenye uzinduzi wa kipute cha msimu huu wa 2019/2020.

”Chapa Dimba inatoa matumaini ya maisha mazuri kwa vijana wengi nchini maana baada ya kugundua umuhimu wa spoti tumeamua kuwasaidia kukuza talanta zao ili kupata ajira na kujikimu kimaisha,” ofisa mkuu wa Safaricom kitengo cha wateja, Sylvia Mulinge alisema.

Mkoa wa Nairobi na Mombasa inaorodheshwa kati ya maeneo yaliyofurika wachezaji chipukizi wengi tu lakini kwa mara mbili mfululizo hawakufanikiwa kufanya kweli.

Kwenye mechi za makala zilizopita msimu wa 2017/2018 taji hilo liliendea waliokuwa wawakilishi wa Mkoa wa Nyanza, Kapenguria Heroes na Plateau Queens (wavulana na wasichana) mtawalia huku Mkoa wa Nairobi ukiambulia patupu.

Sahib Jamal wa Al- Alhy FC (kulia) akishindana na Kepha wanjala wa South B United(kushoto) akijaribu kumkwepa kwenye nusu fainali ya wavulana kuwania ubingwa wa kitaifa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two Uwanjani Kinoru Stadium Meru. Picha/ John Kimwere

Msimu wa 2018/2019 wavulana wa Manyatta United (Mkoa wa Nyanza) na vigoli wa Kitale Queens (Mkoa wa Bonde la Ufa) walibeba ubingwa huo.

Je raundi hii chipukizi wa Nairobi na Mombasa watazinduka na pengine kubeba mojawapo ya mataji hayo? Kwenye makala ya Season One, Nairobi iliwakilishwa na  mojawapo kati ya timu bomba nchini, Gor Mahia Youth lakini ilikosa maarifa mbele ya Kapenguria Heroes (Nyanza) ilipolazwa mabao 3-0 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika fainali Ugani Bukhungu Stadium, Kakamega.

Nao vigoli wa Beijing Raiders (Nairobi) walilazwa magoli 7-1 na Bishop Njenga (Magharibi) kwenye robo fainali.

Fainali za makala yaliyopita ziliandaliwa Kinoru Stadium, Meru ambapo kwa mara nyingine wawakilishi wa Nairobi walionyoshwa kivumbi. Wavulana wa South B United walizabwa mabao 3-2 na Al-Ahly ya Bonde la Ufa kwa mikanju ya penalti kwenye nusu fainali.

Nayo Acakoro Ladies ilibugizwa magoli 4-2 na Kitale Queens (Mkoa wa Bonde la Ufa) kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 katika fainali.

”Kitale Queens ni kisima cha kukuza soka ya wasichana ambapo imejiandaa kutetea taji lake ililoshinda muhula uliyopita,” anasema kocha wake, Justine Okiring na kuongeza kuwa shughuli zitakuwa moto zaidi.

Naye kocha wa Manyatta United, Isaya Opiyo alidokeza kuwa ana imani wavulana wake watatesa zaidi na kuhakikisha wamenyakua tuzo ya Sh1 milioni moja.

You can share this post!

Shauri Moyo Sportiff yalenga Nane Bora

Mbunge ahimiza wakazi kujitokeza wahesabiwe

adminleo