Jesse Were aongoza Zesco kutinga raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika
Na GEOFFREY ANENE
MSHAMBULIAJI Jesse Jackson Were alihakikishia timu yake ya Zesco United FC tiketi ya kushiriki raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kufunga bao lililozamisha Mamba FC kutoka Eswatini 1-0 katika mechi ya marudiano uwanjani Levy Mwanawasa nchini Zambia, Jumamosi.
Were, ambaye amerejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya kitakachopimana nguvu na Uganda mwezi ujao baada ya kukosa Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri, alipachika bao hilo muhimu dakika ya 16. Alivuta kiki nzito hadi wavuni. Zesco inaingia raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 3-0.
Timu ya Zesco, ambayo ilifika nusu-fainali ya Klabu Bingwa mwaka 2016, sasa itakutana na Young Africans (Yanga) ya Tanzania katika mechi yake ijayo.
Miamba wa Tanzania, Yanga, ambao majuzi walizamisha miamba wa Kenya, AFC Leopards 1-0 katika mechi ya kujiandalia mechi ya Klabu Bingwa, walichabanga Township Rollers 1-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.
Timu zingine ambazo zimeshaingia raundi ya kwanza ni JS Kabylie (Algeria), Al-Ahly (Misri), Kampala City Council Authority (Uganda), Cote d’Or (Ushelisheli), Wydad Casablanca (Morocco), TP Mazembe (DR Congo), Green Eagles (Zambia), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), FC Platinum (Zimbabwe), Etoile du Sahel (Tunisia) na mabingwa watetezi Esperance (Tunisia).