• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Polo arudisha watoto kwa wakwe zake

Polo arudisha watoto kwa wakwe zake

NA JOHN MUSYOKI

MASII, MWALA

KALAMENI wa hapa alishangaza wakazi wa eneo hili aliporudisha watoto wawili pacha kwa wakwe zake na kuwaambia hangelea wana wasio wake.

Duru za mtaani zinasema kwamba jamaa huyo alimuoa mkewe akiwa na watoto hao lakini baadaye akaanza kudai kwamba hakuwa na uwezo wa kuwalea watoto wasio wake.

Siku ya kioja, jamaa alifika kwa wakwe zake na kukiri kwamba gharama ya maisha ilikuwa juu na hangeweza kuwalea watoto ambao hawakuwa wake.

“Nimewaletea wajukuu wenu. Maisha yamekuwa magumu sana na siwezi kuwalea watoto hawa kwa sababu sio wangu. Itabidi waishi hapa na mimi niishi na mke wangu,” jamaa alisema.

Inasemekana wakwe wa jamaa huyo walipigwa na mshangao mkubwa. “Ala! Sisi tumekuwa wazee na hatuwezi kuwalea watoto hawa. Itakubidi uvumilie kuwalea hawa watoto kwa sababu ulipokubali kumuoa mama yao tulikueleza kwamba alikuwa na watoto,” wakwe walimwambia jamaa.

Hata hivyo jamaa alikanusha madai ya wakwe zake. “Nitawaacha hapa mpende msipende na mkishindwa kuwalea wapelekeni kwa baba yao. Kwa sasa mke wangu ni mjamzito na akijaliwa kuzaa mapacha tena mzigo wa ulezi utakuwa mzito kwangu. Sitaki presha kwa sasa, wacha nirudi kwangu,” jamaa aliwaambia wakwe na kuondoka.

Haikujulikana ikiwa jamaa alikuwa amezungumza na mkewe kabla ya kuwapeleka watoto hao kwa wakwe zake.

Kulingana na mdokezi, ilibidi wakwe wa jamaa huyo wawatuze wajukuu wao baada ya juhudi za kumshawishi jamaa huyo kuambulia patupu. Duru zinasema wazee hao hawakutaka kuwasiliana na binti yao kwa sababu alikuwa mjamzito.

You can share this post!

IPOA yachunguza kisa cha OCS kuuma sikio raia

TAHARIRI: Maswali mengine hayafai katika sensa

adminleo