Makala

Kuondoka kwa Msimamizi wa Bajeti Agnes Odhiambo

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

KIPINDI cha kuhudumu cha Bi Agnes Odhiambo kama Msimamizi wa Bajeti (CoB) kilikamilika Jumanne, Agosti 27, 2019, baada ya kufanya kazi kwa miaka minane.

Kulingana na Katiba, mshikilizi wa ofisi hii huhudumu kwa muhula mmoja wa miaka minane ambao hauwezi kuongezwa hata kwa siku moja.

Bi Odhiambo ambaye ni Mhasibu na Mwanachama wa Taasisi ya Wahasibu Nchini (ICPAK) amekuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa rasilimali na pesa za umma zinatumika kama ilivyopangwa katika bajeti; katika Serikali ya Kitaifa na serikali za kaunti.

Afisa hiyo hutoa ushauri kuhusu utekelezaji wa bajeti katika ngazi za serikali ya kitaifa na vilevile serikali za kaunti.

Odhiambo pia amekuwa mhusika mkuu katika kamati nyingi za kutatua mivutano kuhusu masuala ya bajeti baina ya na kati ya ngazi hizi mbili za serikali, kwa lengo la kuhakikisha inatatuliwa kwa haraka na kwa njia inayoridhisha pande zote.

Isitoshe, ofisi ya Msimamizi wa Bajeti huhakikisha kuwa fedha zilizotengewa wizara,idara na mashirika ya serikali zinatumika kwa kuzingatia taratibu maalum zinazokubalika kulingana na mahitaji ya taaluma ya uhasibu.

Japo ofisi hiyo ni huru, kikatiba, kwa mara kadhaa Bi Odhiambo alijipata katika moto wa siasa akilaumiwa kutokana na baadhi ya maamuzi aliyotoa kuhusu masuala nyeti ya matumizi ya fedha za umma.

Mfano mzuri ni wakati mgogoro kuhusu matumizi ya pesa za Eurobond na waliotia sahihi kuidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) jijini New York, Amerika.

Aliitwa kujibu maswali kuhusu suala hilo, mwaka 2018, mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) ambapo aliiambia kamati hiyo kwamba ofisi yake haikuwa imeidhinisha kutolewa kwa pesa hizo.

Lakini baadaye, baada ya madai kwamba alisukumwa na wanasiasa wenye ushawishi serikalini, Bi Odhiambo alibadilisha msimamo kuwa japo hakuhusishwa katika utoaji wa pesa hizo, alikubaliana na maelezo yaliyotolewa na serikali kuhusu mkopo huo wa kiasi cha Sh215 bilioni.

Ofisi kufahamu

Bi Adhiambo aliiambia kamati ya PAC ambayo wakati huo ilikuwa ikiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo kwamba ofisi yake ilifahamu kuhusu suala hilo wakati Hazina ya Kitaifa ilikuwa ikitayarisha rekodi zake za uhasibu.

Alisema kuwa pesa ambazo zilikuwa zimewekwa katika “akaunti maalum” katika benki za kigeni chini ya jina la Hazina ya Kitaifa ziliidhinishwa na stakabadhi zenye sahihi ya “watu wasiojulikana na Ofisi ya Msimamizi wa Bajeti”.

Kwa msingi huu, huku Bw Stephen Masha ambaye alikuwa naibu wa Bi Odhiambo, akianza kuchapa kazi katika ofisi hii, sharti awe tayari kukumbana na mzozo kama hii itakayomgonganisha na maafisa na wanasiasa wenye ushawishi serikalini.

Bw Masha, anapaswa kuwa mkakamavu katika uendeshaji wa shughuli za ofisi hizo ili kusitokee visa ambapo pesa za serikali zinatolewa kwa matumizi bila idhini ya afisi yake.

Hata hivyo, alipokuwa akiondoka Bi Odhiambo alisema hivi: “Ninapoondoka naacha ofisi thabiti ambayo itaendelea kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Kenya; kwa muda mrefu.”

Kwenye ripoti yake iliyotathmini utendakazi wake kuanzia mwaka wa 2011 hadi 2019, Bi Odhiambo anaungama kuwa japo aliandikisha ufanisi wa kiwango fulani, kuna changamoto kadha zilizoathiri uwezo wa afisi yake kutenda kazi nzuri.

Miezi mitatu

Bw Masha ambaye aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa Kaimu Msimamizi wa Bajeti anatarajiwa kushikilia wadhifa huo kwa kupindi cha siku 90 kabla ya uteuzi wa mshikilizi kamili kufanywa kuwa mujibu wa sehemu ya 4 ya Sheria kuhusu Afisi ya Msimamizi wa Bajeti ya 2016.

Kulingana na ibara ya (1) ya sheria hiyo mshikilizi wa wadhifa huo kwa muda atakuwa na mamlaka kamili ya Msimamizi wa Bajeti.

Kwa hivyo, inatarajiwa kuwa afisi hiyo inadumisha moyo wa ugatuzi kwa kuhakikisha kuwa pesa za kutosha zinaelekezwa kwa miradi ya maendeleo wala sio matumizi ya kila siku.

Kwa mfano, katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019 ilibainika kuwa zaidi ya serikali 24 za kaunti zilitumia chini ya asilimia 20 ya fedha zilizotengewa kwa miradi ya maendeleo; hali ambayo inakwenda kinyume na Katiba na sheria husika.

Kulingana na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM Act) serikali za kaunti zinafaa kutenga angalau asilimia 30 ya mgao wao wa fedha kwa miradi ya maendeleo.

Kwa hivyo, Bw Masha pamoja na mtu mwingine ambaye atateuliwa kwa wadhifa huo, sharti wahakikishe kuwa ajenda ya maendeleo inaendelezwa katika ngazi za serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Kabla ya kuteuliwa kwa wadhifa huo na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Bi Odhiambo alikuwa akihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) kuanzia 2009 hadi 2011.

Kabla ya kujiunga na bodi ya CDF Bi Odhiambo alihudumu kama mhasibu katika kampuni ya uhasibu wa Deloitte and Touch, kampuni ya kutengeneza sigara, BAT Kenya, kampuni ya Unga Group, kampuni ya Metro Cash and Carry na Benki ya Post Bank.