Michezo

Nairobi Water watwaa taji la WASCO

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Nairobi Water imehifadhi taji la Water Services Companies Sports Organisation (WASCO) kwa kupiga Kakamega Water mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penalti katika fainali iliyopigiwa Chuo Kikuu cha Embu, mjini humo.

Nairobi Water ambayo imeshiriki mashindano hayo mara kumi imeweka rekodi ya kushinda taji hilo mara nane. Aidha Nairobi Waterilichangia idadi ya wachezaji kumi kati ya wanasoka 22 walioteuliwa katika kikosi cha taifa kitakaowakilisha Kenya kwenye mashindano ya Afrika Mashariki nchini yatakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Uganda.

Nairobi Water chini ya kocha, Dennis Mambo ilitwaa ushindi huo baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida. Awali kwenye mechi za makundi, Kakamega Water ilinyorosha Nairobi Water kwa magoli 3-1.

”Bila shaka nashukuru vijana wangu kwa kuhifadhi taji hilo lakini wafahamu lazima wajiandae vizuri kukabili wapinzani wao kwenye mashindano ya muhula ujao,” meneja wa Nairobi Water, Dennis Ndichu alisema.

Kwenye nusu fainali, Nairobi Water kupitia mipigo ya matuta ilibamiza Embu Water kwa mabao 4-2 nayo Kakamega ilisajili mabao 2-0 dhidi ya Nakuru Water.

Kwenye mechi za nane bora Nairobi Water ililaza Eldoret Water kwa magoli 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kuagana sare tasa. Orodha ya wachezaji kumi walioteuliwa inajumuisha: Peter Odoyo, Mohammed Kai, Mark Okumu, Michael Ochieng, Kelvin Were, Moses Shisia, Brian Otiato na Elijah Tsavai kati ya wengine.