• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
Kitany azidi kumwanika Linturi

Kitany azidi kumwanika Linturi

Na RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Meru, Mithika Linturi Jumatano aliendelea kuanikwa katika kesi ya talaka inayoendelea kati yake na Maryanne Kitany.

Mahakama iliambiwa kuwa mjakazi wao alifariki muda mfupi baada ya kupiga simu na kumweleza Bi Kitany kwamba Seneta Linturi alikuwa akiwapeleka wanawake wengine nyumbani kwao Igembe, Kaunti ya Meru.

“Mjakazi wangu aliyekuwa akiwatunza watoto nyumbani Meru alinipigia simu akitaka kuzugumza nami. Nilimweleza nitaenda kumtembelea wikendi hiyo kwa vile Bw Linturi alikuwa anasafiri hadi Uswizi. Usiku huo ndio mjakazi wangu alifariki. Sikuenda kumuona kwa sababu alifariki,” alisema Bi Kitany.

Akitoa ushahidi, Bi Kitany alisema sababu kuu zilizomfanya kuwasilisha kesi hiyo ya talaka ni Bw Linturi kutisha kumuua pamoja na kughushi hatimiliki za mashamba ya Kitany pamoja na kupokea mikopo ya mamilioni ya pesa kutoka benki kadhaa bila kumhusisha.

Alisema Bw Linturi alimfukuza yeye na watoto katika makazi yao ya Riverside jijini Nairobi kisha akapiga ripoti kwa polisi kuwa magaidi walikuwa wanaishi kwake.

Wakili Dunstan Omari akimskiza mteja wake Maryanne Kitany Agosti 28, 2019. Picha/ Richard Munguti

“Bw Linturi alisafirisha wahuni kwa basi wakiwa na mbwa na panga kututimua kutoka kwa nyumba yetu Nairobi. Nimemsaidia kujenga makazi yetu na ya wazazi wake Meru,” alisema Bi Kitany.

“Mume wangu Bw Mithika alisusia majukumu ya mume, alitoroka makazi yetu ya kifahari ya Nairobi na kujificha Meru. Alidai watu wangu walifanya njama ya kuiba kampuni zake,” Bi Kitany alimweleza Hakimu Mkuu Peter Gesora.

Mahakama ilifahamishwa kuwa kila wakati Bw Linturi alipoulizwa na mkewe sababu ya kutotekeleza majukumu ya mume alikuwa akitoroka na kuishi katika hoteli jijini.

Bi Kitany alisema Bw Linturi alimchapa wakiwa nyumbani kwao Meru na kwamba alikuwa akimnyima haki ya ndoa.

Hakimu Gesora aliamua kuwa vikao vya kesi hiyo sasa vitasikizwa faraghani ili kutoa nafasi ya kueleza kwa undani masuala yaliyovuruga ndoa yao.

You can share this post!

Utaratibu wa uteuzi wa Mkaguzi Mkuu mpya kuanzia Septemba 23

ODM yatema 9 Kibra huku Jubilee na ANC zikijitosa kwa...

adminleo