Makala

AKILIMALI: Kutana na mwinjilisti aliyebobea katika utaalamu wa zao la stroberi

August 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MARY WANGARI

MBALI na kuchunga nyoyo za waumini na kuwaelekeza katika ufalme wa mbinguni, Pasta Gitau ni mchungaji aliyepania kuwawezesha watu kuishi vyema duniani kwa kuwaelimisha kuhusu kilimo cha stroberi.

Pasta Gitau wa Kanisa la United Pentecostal Church lililo mjini Limuru, Kiambu, ni afisa aliyesajiliwa na serikali kuuza mbegu za stroberi mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 34 katika aina hiyo ya kilimo.

Aidha, hutoa mafunzo kwa wakulima au watu wanaotaka kujitosa katika kilimo hicho.

Kulingana naye, kilimo cha stroberi kina soko kubwa nchini na katika viwango vya kimataifa ambapo kikitiliwa maanani na kuwekezwa ipasavyo, kina uwezo wa kuletea taifa hili mapato ya kiwango cha juu mno ikilinganishwa na mazao mengine kama vile majani chai na kahawa, yanayouzwa katika mataifa ya kigeni.

Lakini licha ya manufaa yote ya stroberi ikiwemo soko pana nchini na kimataifa, matumizi mengi, na faida ya juu, ni kwa nini wakulima wengi bado wanachelea kujiunga nacho? Ni swali tulilomuuliza Bw Gitau ambaye hakusita kutujibu.

“Stroberi ni zao geni. Kwa kawaida Wakenya huwa na hulka ya kujaribu mambo mapya na ndiposa si watu wengi walio tayari kuanza kilimo cha stroberi licha ya faida yake,” alitueleza.

Jinsi ya kuhakikisha unapata mbegu halisi. Kulingana naye, changamoto kuu inayokabili ukuzaji wa stroberi ni ukosefu wa ardhi na kupata mbegu halisi za stroberi. Baadhi ya wakulima wamejipata wakikadiria hasara ambayo huzima matumaini yao kuhusu kilimo cha stroberi baada ya kutumia mbegu feki kutoka kwa mawakala.

“Tatizo kuu katika kilimo cha stroberi ni mbegu. Hatuna mbegu asilia na hivyo basi, hatuna budi kuagiza kutoka mataifa ya kigeni, hali ambayo huzua changamoto ikizingatiwa kuna aina 37 ya tunda hili nchini. Wakulima hushindwa kutofautisha na wanapotanabahi, huwa wamechelewa mno,” anaeleza.

Ni katika harakati za kutegua kitendawili cha mbegu halisi na zile feki na wakati uo huo kukabiliana na changamoto za kifedha, ambapo watu wengi huhadaiwa na mawakala.

Mhubiri huyu ambaye pia ni mtaalam wa Masuala ya Udongo na Ukuzaji Mimea, anawatahadharisha wakulima na mtu yeyote ambaye angependa kujihusisha na kilimo cha stroberi, kujiepusha na mawakala waliofurika soko na mimea feki inayouzwa kwa bei ya chini ili kuwalaghai wakulima wasio na habari.

“Stroberi hukuzwa kupitia vijisehemu vya mmea wake. Ikiwa unataka kuanza kukuza stroberi, unapaswa kuwaendea wauzaji mbegu waliopewa leseni na serikali ili kupata mimea mwafaka ya kukuza matunda hayo.

“Mimea halisi huuzwa kwa Sh30 kwa kila mmoja. Mawakala kwa upande mwingine huuza mimea yao kwa kati ya Sh3 hadi Sh5 kwa kila mmea ili kuwavutia wakulima,” anafichua, akieleza kwamba idadi kubwa ya wakulima hulaghaiwa kwa bei hiyo ya chini na kuishia kulia baadaye wanapopata mazao duni.

Taifa la Kenya lina mazingira mwafaka kwa ustawishaji wa stroberi inayonawiri katika maeneo yenye joto na baridi ambayo yanapatikana katika sehemu nyingi Kenya, jinsi Gitau anavyoeleza.

Hata hivyo, kulingana na mtaalam huyu, maadamu mtaji wa kwanza ndicho kizingiti kikuu kinachowazuia watu wengikujitosa kati ka ukuzaji wa stroberi, ni muhimu mno kufanya utafiti wa kina na kujihami kwa maarifa mwafaka yanayopatikana kirahisi katika afisi za kilimo katika ngazi ya kaunti.

“Ukiwa na mimea mwafaka ya kuanzia kupanda stroberi katika thumuni ekari ya ardhi (1/8) unaweza kuwa na hakikisho la kupata jumla ya kiasi Sh92,000 kila mwezi, hali inayomaanisha kuwa utakuwa umejilipa hela ulizotumia kuanza na pia kukuza mimea yako binafsi kwa shuguli nyinginezo za upanzi,” anasema.

Utunzaji wa stroberi ili kupata mazao mengi: Bw Gitau ambaye amekuwa akishiriki Maonyesho ya Kilimo nchini kila mwaka na kutoa mafunzo katika Vituo vya Mafunzo ya Kilimo (ATC) kote nchini kwa miaka 25, anakosoa kasumba potovu kwamba mimea ya stroberi, inayochukua muda wa miezi mitatu kukomaa na kuvunwa, inahitaji kiasi kikubwa cha maji ili kupata mazao mengi.

“Kinyume na wanavyofikiri watu wengi, mimea ya stroberi haihitaji maji mengi. Badala yake inahitaji maji mara kwa mara katika miezi ya kwanza. Katika mwezi wa kwanza, unafaa kuinyunyizia maji kila siku wakati wa jioni. Katika mwezi wa pili unapaswa kuinyunyizia mara mbili; asubuhi na jioni,” anafafanua.

Wadudu na maradhi

Isitoshe, ikilinganishwa na mazao mengine, stroberi ina kiwango cha chini cha wadudu na maradhi ambayo yanaweza kuzuiliwa kirahisi, jinsi anavyoeleza pasta Gitau.

“Unapaswa kuwa makini ili matunda ya stroberi yasiguse ardhi na hivyo kuoza. Ili kuzuia matuda yako kuoza yakiwa shambani, unapaswa kufunika ardhi kwa nyasi ya kawaida au mimea ya ngano. Pia epuka kupulizia stroberi dawa kiholela. Pulizia tu unapogundua tatizo kama vile majani yake kujikunja kutokana na kuchomwa na barafu na kadhalika,” anashauri.

Jambo lingine unalopaswa kuangazia ili kuhakikisha unapata mazao mengi kulingana na Bw Gitau, ni neti unayotumia kukinga mimea yako dhidi ya kuliwa na nyuni.

“Unahitaji kutumia aina maalum ya neti ambayo kando na kuruhusu mwangaza kupenyeza, pia ina vijitundu vyenye ukubwa wa kutosha maadamu stroberi huhitaji wadudu kama vile vyuki na vipepeo ili kueneza mbegu zake,” anasema.

Manufaa ya Stroberi: Manufaa ya stroberi ni chungu-nzima kama anavyosema Bw Gitau.

Kwa mfano matunda ya stroberi hupakiwa na kuuzwa kwa kati ya Sh300 na Sh400 kulingana na ubora wake.

Matunda ya stroberi yana soko kubwa nchini ambapo yanauzwa kwenye maduka ya jumla, hoteli za kifahari, kwa wauzaji wa mboga na matunda na kadhalika. Pia yanaweza kuuzwa katika mataifa ya kigeni ambapo yanazalisha mapato ya kigeni.

Zao la Stroberi pia lina manufaa ya ziada ambapo matunda yake pia yanweza kuuziwa viwanda vya kutengeneza maziwa mtindi (yorghut), uokaji keki na biskuti, utengenezaji wa mvinyo wa divai sharubati na matumizi mengine.