• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Mabingwa 16 wa kwanza wa Riadha za Diamond League kujulikana leo Alhamisi

Mabingwa 16 wa kwanza wa Riadha za Diamond League kujulikana leo Alhamisi

Na GEOFFREY ANENE

KIVUMBI kinatarajiwa kwenye fainali ya kwanza ya Riadha za Diamond League ikifanyika mjini Zurich nchini Uswizi leo Alhamisi ambapo macho yatakuwa kwa nyota Beatrice Chepkoech (Kenya), Joshua Cheptegei (Uganda), Sifan Hassan (Uholanzi), Genzebe Dibaba (Ethiopia) na Nijel Amos (Botswana).

Mshikilizi wa rekodi ya dunia Chepkoech atapimwa kasi yake vilivyo na Wakenya wenzake Celliphine Chespol, Mercy Chepkurui, Daisy Jepkemei, Norahj Jeruto, Caroline Tuigong na bingwa wa dunia mwaka 2015 Hyvin Kiyeng.

Raia wa Amerika kwa jina Emma Coburn, Mganda Peruth Chemutai na Mjerumani Felicitas Krause pia wanatarajiwa kutoa ushindani mkali kwa Chepkoech ambaye anatetea taji.

Chepkoech anaongoza msimu kwa alama 31. Mpinzani wake wa karibu Chespol amezoa alama 18.

Wakenya Wycliffe Kinyamal, Emmanuel Korir na Ferguson Rotich watatifua vumbi katika mbio za mita 800.

Bingwa wa mwaka 2016 Rotich ataibuka mshindi wa msimu huu akimzima mfalme wa mwaka 2014, 2015 na 2017 Nijel Amos anayejivunia kasi ya juu mwaka huu katika kitengo hiki ya dakika 1:41.89. Amosa anashikilia nafasi ya pili kitengo hiki cha mizunguko miwili kwa alama 31, moja nyuma ya Mkenya huyo. Mshindi wa mwaka 2018 Korir na Kinyamal wamezoa alama 21 na 19, mtawalia. Jumla ya wakimbiaji tisa watashindana katika mbio za mita 800.

Winny Chebet atabeba matumaini yote ya Kenya katika mbio za mita 1,500 zilizovutia washiriki 15 wakiwemo wakali Sifan Hassan (Uholanzi), Genzebe Dibaba (Ethiopia) na Rababe Arafi (Morocco).

Chebet anashikilia nafasi ya 10 kwa alama tisa dhidi ya Gabriela Debues-Stafford kutoka Canada na raia wa Ethiopia Gudaf Tsegay, ambao wako sako kwa bako kileleni kwa alama 24 na pia watakuwa uwanjani.

Kenya itawakilishwa katika mbio za mita 5,000 za wanaume na wakimbiaji Nicholas Kimeli na Stanley Mburu. Jumla ya wakimbiaji 17 watashiriki kitengo hiki wakiwemo magwiji Cheptegei (Uganda) na raia wa Ethiopia akina Yomif Kejelcha na Selemon Barega, miongoni mwa wengine.

Barega yuko juu ya jedwali la alama la kitengo hiki. Amezoa alama 29. Yuko mbioni kutetea taji aliloshinda mwaka jana.

Mabingwa wa vitengo 16 watatuzwa katika fainali ya Zurich, huku wengine 16 wakifahamika katika fainali ya jijni Brussels nchini Ubelgiji mnamo Septemba 5.

You can share this post!

Madereva 25 tayari kuonyeshana ubabe KCB Nanyuki Rally

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Utaratibu katika ufunzaji wa...

adminleo