Mfyatukaji stadi Moraa afuzu Riadha za Dunia
Na CHRIS ADUNGO
BINGWA wa kitaifa katika mbio za mita 400, Mary Moraa amefuzu kushiriki Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 28 na Oktoba 6, 2019.
Moraa alijikatia tiketi ya kuwakilisha Kenya nchini Qatar baada ya kuandikisha muda bora wa sekunde 51.75 katika nusu-fainali ya Michezo ya bara la Afrika (AAG) inayoendelea kwa sasa jijini Rabat, Morocco. Nusu-fainali hiyo ilitawaliwa na Galefele Moroko wa Botswana kwa muda wa sekunde 51.54.
Moraa ambaye alipiku muda wastani wa kufuzu kwa mbio za mita 400 katika Riadha za Dunia (sekunde 51.83), kwa sasa anaungana na mshikilizi wa rekodi ya kitaifa katika mbio hizo, Hellen Syombua.
Syombua aliandikisha muda bora zaidi wa chini ya sekunde 51.83 mara tatu mwaka huu na alikuwa sehemu ya kikosi kilichokamilisha mchujo wa kufuzu kwa Mbio za Dunia za kupokezana vijiti mjini Iten mnamo Aprili 13, 2019. Kikosi hicho kiliweka rekodi ya muda wa sekunde 51.72.
Wakati wa mchujo wa kutafuta kikosi cha kupeperusha bendera ya Kenya katika Michezo ya AAG nchini Morocco mwaka huu, Syombua aliandikisha muda wa sekunde 51.66 mnamo Juni 21 kabla ya kuweka rekodi mpya ya kitaifa wa muda wa sekunde 51.09 katika fainali.
Syombua alitarajiwa kumenyana jana usiku na Galefele, Grace Obuor wa Ghana na malkia wa Nigeria, Favour Chukwuka katika fainali ya mbio za mita 400 jijini Rabat. Favour alikamilisha mchujo wake wa nusu-fainali ya pili jijini Rabat kwa muda wa sekunde 51.94 mbele ya Grace (52.14).
Kwa upande wa wanaume, Mkenya Alphas Kishoyian alifuzu pia kwa fainali ya mbio za mita 400 baada ya kusajili muda wa sekunde 46.61 katika nusu-fainali ya kwanza na kumaliza wa pili nyuma ya Ditiro Nzamani wa Botswana (46.23).
Mkenya Joseph Poghisio aliambulia pakavu baada ya kurushwa katika nafasi ya tano katika nusu-fainali ya pili iliyotawaliwa na Scotch Leungo wa Botswana kwa muda wa sekunde 45.52. Poghisio aliandikisha muda wa sekunde 46.69.
Katika mbio za mita 800, Wakenya Abel Kipsang na Cornelius Tuwei walifuzu kwa fainali iliyoandaliwa jana usiku baada ya kusajili muda wa dakika 1:47.91 na 1:48.35 mtawalia katika nusu-fainali ya kwanza iliyotawaliwa na Abdessalem Ayouni wa Tunisia kwa muda wa dakika 1:48.31.
Mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 5,000 Edwin Soi alionyeshwa vumbi katika fainali ya mbio za mita 10,000 mnamo Jumanne usiku. Mkenya huyo aliambulia nafasi ya nne baada ya muda wa dakika 28:05.70 nyuma ya Mwethiopia Jemale Yimer aliyeridhika na medali ya shaba kwa muda wa dakika 27:59.02.
Berehanu Wendemu wa Ethiopia alijitwalia dhahabu kwa muda wa dakika 27:56.81 mbele ya Aron Teklu wa Eritrea aliyejitwalia nishani ya fedha kwa muda wa dakika 27:57.79.